KUNA mkanganyiko unafukuta chini kwa chini Marekani baada ya Rais Donald Trump kufutilia mbali mwongozo wa Serikali iliyopita ya Barack Obama, kuidhinisha wanafunzi wenye mwelemeo wa jinsia mbili kutumia maliwato wanayojisikia katika shule za umma kwamba watakaokataa kutii agizo hilo watachukuliwa hatua ikiwamo kunyimwa mgao wa fedha za uendeshaji kwa kuwa zitakuwa zinakiuka haki za kimsingi za kibinadamu.
Hivyo ndivyo maagizo ya Serikali ya Obama yalivyobainisha na kupokelewa kwa shangwe na watu wenye jinsia mbili kwamba ni ushindi kwa haki zao kutambuliwa, lakini Rais Trump ameamua kufuta amri hiyo licha ya kwamba kuna kesi katika mahakama kuhusiana na ubishani juu ya agizo la Serikali ya Obama kwamba kila shule ina haki ya kuamua kuhusu matumizi ya maliwato kwa wanafunzi wake wa jinsia tofauti, tayari mkanganyiko huo umesababisha figisu kutokana na amri ya Rais Trump. Takribani watu 200 walijikusanya mbele ya Ikulu ya Marekani kupinga amri hiyo ya Trump wakihanikiza kauli mbiu: "Hatutaki chuki, hatutaki kihoro, wanafunzi wenye jinsia mbili wanakaribishwa!"
Waandamanaji hao walipeperusha bendera yenye rangi za upinde wa mvua ambayo hutumiwa nao kujitambulisha kuwa ‘LGBT’ (lesbians, gays, bisexual na transgender) yaani wanawake na wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wenye mtazamo wa jinsia mbili na wanaojihusisha na mapenzi na jinsia zote wanazolingana na wasizolingana nazo.
Kuna mvutano mkubwa kuhusu suala hilo na msingi wa haki za binadamu kwa kuwa Obama alitoa agizo lake kwa ajili ya kutetea haki sawa kwa Wamarekani wote, lakini Trump mhafidhina wa maumbile ya asilia ya kibinadamu anapongezwa na wahafidhina wenzake wanaomsifu kwa kuharamisha mwongozo wa maliwato ya jinsia mbili uliotolewa na Serikali iliyopita kwamba amerejesha thamani ya utu halisi, pia kutengua hulka ya Obama aliyetumia mamlaka yake kupitisha amri alizotaka kwa ajili ya manufaa ya mustakabali wake kisiasa bila kupitia kwenye Bunge.
Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu alibainisha kuwa kulikuwa na ulazima wa kuchukua hatua katika kusubiri uamuzi wa mahakama kuu, ambapo kijana mwanafunzi Gavin Grimm amewafungulia mashtaka wasimamizi wa shule ya Glouster County waliomkatalia kutumia maliwato ya wavulana kutokana na kujiakisi kwake kuwa mtu mwenye jinsia mbili, lakini pia mashtaka hayo yanahusisha madai ya kutaka wenye jinsia mbili kutajwa na kutambuliwa kwa majina wanayotaka kuyatumia na kulindwa dhidi ya vitendo vya unyanyaswaji kutoka kwa wanafunzi wengine.
Ni mkanganyiko unaosababisha mvutano wa pande mbili dhidi ya wahafidhina na wanaotetea haki za ‘LGBT’ ambapo majimbo yapatayo 13 yakiongozwa na Texas ambayo awali yalipinga kutekeleza agizo la Obama, lakini sasa inavyoelekea Trump ambaye wakati wa kampeni zake za kuingia Ikulu alionesha kuwaunga mkono watu wenye jinsia mbili sasa amewageuka kwa kubinya haki zao wanazozitaka nao wanamlalamikia na kumkumbusha kuwa hata yeye ana marafiki wengi miongoni mwa ‘LGBT’ wakiwamo nyota wakubwa wa burudani duniani.
Unaweza kuhisi kuwa matumizi ya maliwato kwa mgawanyiko wa kijinsia si jambo linalopaswa kuzua mkanganyiko mkubwa kiasi hicho, lakini katika nchi za Magharibi maana ya haki za kibinadamu ni pamoja na kutokuwapo kwa ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwa raia wake wakiwamo wenye kujitambulisha kwa jinsia tofauti na walizozaliwa nazo, kwa aina ya mavazi na hulka wanazojiakisi nazo lakini pia wapo wanaofikia hatua ya kufanya upasuaji kujibadili jinsia ili kuridhisha nafsi zao kufuata matakwa ya wanavyojisikia.
Wapo pia wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja lakini pia wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia mbili kwa nyakati tofauti, makundi yote manne yana vyama vyao vya kutetea haki za kutambuliwa kwao katika kuhakikisha wanaishi bila kubaguliwa na kunyanyaswa na watu wengine wanaoishi maisha ya kawaida ya asili ya ama kuwa mwanaume anayejitambua hivyo au mwanamke anayejitambua kwa jinsi alivyo.
Trump amewaweka njia panda ‘LGBT’ kutokana na amri yake mpya iliyoharamisha amri ya Obama, akiwahamanisha kutokana na agizo lake jipya. Si ndani ya Marekani tu lakini hata nje ya nchi hiyo vyama vya ‘LGBT’ vimemjia juu Trump aliyewaunga mkono lakini sasa amewageuka, ikiwamo taasisi ya Stonewall iliyopo Uingereza ambayo imeanza kujihusisha na ‘LGBT’ nje ya Uingereza takribani miaka miwili iliyopita, katika nchi ambazo watu wa aina hiyo wanakabiliwa na unyanyaswaji wa kiwango cha juu. “Kwa kukataa kulinda haki za ‘LGBT” kutumia maliwato na mabafu kwa jinsi wanavyojitambua, Rais Trump amekengeuka katika kutetea mwelekeo chanya wa kutambua haki za wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, wenye jinsia mbili, pia wenye kujihusisha na jinsia zote mbili kimahusiano.
Hivyo kuanzisha mwelekeo mbaya wa kukiukwa kwa haki zao kutokana na amri mpya ya Serikali ya Marekani!” Stonewall wanamkumbusha Trump juu ya ahadi zake alizotoa awali za kutetea na kulinda haki za ‘LGBT’ lakini Trump na Serikali yake wakibainisha kuwa watafumua mambo yote ambayo Obama aliyasimika kibabe kwa kutumia mamlaka ya Urais.