31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAKULIMA WASHINDWA KUIONGEZEA THAMANI KAHAWA

Na UPENDO MOSHA-MOSHI 


WAKULIMA wengi wa kahawa mkoani Kilimanjaro wameshindwa kunufaika na zao hilo kutokana na kujihusisha zaidi na uzalishaji na kushindwa kujiingiza kwenye usindikaji ili kuiongeza thamani na kuingia kwenye ushindani wa soko la kitaifa na kimataifa. 

Zao hilo, ambalo katika Mkoa wa Kilimanjaro linaonekana kulimwa zaidi na wanawake, halijaonyesha mafanikio makubwa ya maendeleo kwa wakulima hao, jambo ambalo linaelezwa kuchangiwa na wengi wao kujikita kwenye uzalishaji na wengine kulima kwa mazoea.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Tanzania Women in Coffee Association (Tawoca), Fatma Faraji, wakati wa kujifunza namna ya kutengeneza kahawa kupitia mashine ya expesso ili kuiongeza thamani. 

“Wapo watu wengi wanalima kahawa hapa nchini na asilimia kubwa ni wanawake, lakini wakulima hawa wamekuwa hawanufaiki na kujikomboa kiuchumi kupitia zao hilo, kutokana na kuzalisha kwa wingi, lakini hawajihusishi na shughuli za kusindika, au kuingia kwenye mnyororo wa thamani pamoja na kuipeleka sokoni, hili ni jambo ambalo linawarudisha nyuma wengi,” alisema.  

Aidha, alisema ili wakulima waondokane na dhana hiyo ya kulima kahawa pasipo kuziongezea thamani, ni vema wakulima wapewe elimu ya usindikaji bora wa kahawa ili kilimo hicho kiweze kuwanufaisha kiuchumi. 

Alisema kadri wanawake watakapoelimishwa kuhusiana na mnyororo wa thamani, usindikaji na masoko, zao hilo ambalo limedorora katika mkoa huo litakua kwa kasi tofauti na ilivyo sasa. 

“Wadau wa kahawa mkoani Kilimanjaro pamoja na wanawake kwa ujumla wanatakiwa kuelimishwa juu ya kuongeza thamani katika kahawa ili waweze kunufaka na zao hilo moja kwa moja na kuona umihimu wa kulima kahawa bora,” alisema. 

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TAWOCA, Ida Mkamba, alitoa rai kwa wanawake wote wanaojishughulisha na kilimo cha kahawa kutumia fursa hiyo kuwa wajasiriamali kwa kuanzisha migahawa midogomidogo kwa lengo la kujiongezea kipato. 

“Ni kweli kahawa haimnufaishi mkulima moja kwa moja kutokana na changamoto tunazopitia, lakini nitoe wito kwenu muache kuuza kahawa yote mnayozalisha na mjiongeze kwa kuanzisha migahawa midogomidogo ambayo itawasaidia kuongeza kipato chenu,” alisema.

Mratibu wa kahawa Wilaya ya Moshi, Violeth Kisanga, alisema wamekwisha kuanzisha vikundi zaidi ya 200 vya wanawake wanaojishughulisha na kilimo hicho kwa mikoa yote inayolima kahawa ambayo ni Kagera, Arusha, Tanga, Morogoro, Ruvuma, Tabora, Katavi,  Iringa na Kigoma. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles