|Susan Uhinga, Tanga
Serikali imesema itaendelea kutenga fedha kwa ajili kuwajengea uwezo wataalamu wa wizara na halmashauri wanaotekeleza mpango wezeshi wa kukuza ubia wa sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili waweze kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akifungua mafunzo ya siku tano ya maofisa wa wizara na halmashauri kutoka wilaya 60 nchini, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga, Injinia Zena Saidi, amesema licha ya serikali kuandaa muswada kwa ajili ya kusimamia mfumo wa PPP, lakini pia itaendelea kutoa fedha za mafunzo.
“Mafunzo mnayoyapata leo ni muendelezo wa mafunzo kama haya yaliyofanyika mwaka 2004 na wataalamu wapatao 500 walipatiwa mafunzo hivyo serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ili mpango huo uweze kutekelezwa kwa mafanikio,” amesema Katibu Tawala huyo.
Aidha, amesema Juni 29 mwaka huu muswada wa sheria kwa mpango huo ulisomwa kwa mara ya kwanza bungeni na kwamba utapelekwa utapelekwa tena kabla haijawa sheria lengo ikiwa ni kusimamia mpango wezeshi kwa miradi ya PPP na wawe tayari kutoa maoni yao.
Katibu Tawala huyo amesema utaratibu wa mfumo huo ni utekelezaji unaotoa fursa nzuri kwa miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa jamii na wabia ambapo nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara imeweza kutekeleza miradi ipatayo 383 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 69.
Naye Kamishna wa PPP Wizara ya Fedha na Mipango, Dk. John Mboya amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji wa halmashauri hizo na wale wa wizarani kuendeleza miradi ya PPP na inayotekelezwa na Serikali.