30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kuiongezea bilioni moja Halmashauri ya Bukoba

Na Nyemo Malecela, Kagera

Serikali imeahidi kuongeza Sh bilioni moja kwa Halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya kuweka vifaa na kuongeza wodi za watoto katika hospitali ya Halmashauri ya wilaya hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh bilioni 1.8.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa (TAMISEMI), Seleman Jaffo alipofika Bujunangoma ilikojengwa hospitali hiyo baada ya kuridhishwa na kiwango kilichofikiwa katika ujenzi wa hospitali hiyo na kuongeza kuwa inapaswa kuwa na vifaa vya kutosha ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Lakini Halmashauri hii imekaa kama mbaramwezi, kuna upande mwingine wa halmashauri hawatanufaika na hospitali hii, kwa hiyo tutakachokifanya kama serikali tutajenga kituo cha afya cha kisasa ili wananchi wote wapate huduma bora,” alisema.

Naye,Naibu Waziri wa Nishati, Adv. Stephen Byabato aliagiza shirika la umeme nchini (TANESCO) kupitia upya eneo la mradi ili kupunguza gharama za kuweka umeme katika hospitali hiyo.

“Nafahamu kwamba umeme haujaingia katika majengo yetu na mliletewa bili ya shilingi milioni tisa, ikiwezekana kabla ya Februari iwe imejulikana hatua gani zitatuchukuliwa ili majengo haya yawekewe umeme na kuanza kuhudumia wananchi ipasavyo,”amesema Adv Byabato.

Wakati huo Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti aliahidi kusimamia ipasavyo miradi yote inayotekelezwa katika Mkoa wake ili kuhakikisha inaendana na thamani ya fedha zinazotolewa.

“Sitakuangusha wewe, sitamwangusha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli na wala sitaiangusha serikali yangu kwa ujumla, kwa kuwa tumefanya vizuri katika mradi huu tuna imani tutaletewa miradi zaidi kwa manufaa ya Wanakagera,” amesema.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Murshid Ngeze aliomba kupewa magari ya kutosha ya wagonjwa, ili yasaidie kusafirisha wagonjwa kutokana na jiografia ya halmashauri hiyo kukaa vibaya.

“Tukipata magari ya wagonjwa yatasaidia sana maana yatakuwa yanasomba wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo tarafa ya Rubale, tarafa Bugabo hata Maruku na kuwezesha hospitali hii kufanya kazi yenye tija,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles