Elizabeth Hombo, Dodoma |
Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inatarajia kuwaajiri wataalamu wa kutosha katika fani ya umwagiliaji.
Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Waziri wa wizara hiyo, Isaac Kamwelwe wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond ambaye alihoji iwapo kuna mpango wowote unaotekelezwa wa kuwapata wataalamu wa umwagiliaji katika muda mfupi.
Akijibu swali hilo, Kamwelwe amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Rais- Menejementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ajili ya kupata kibali cha kuajiri wataalamu wa kutosha katika fani ya umwagiliaji.
“Pamoja na hayo halmashauri ambazo hazina wataalam wa umwagiliaji zinashauriwa kuajiri watalaamu wa fani hizo,” amesema.