30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

USAFIRI WA MWENDOKASI KUSUKWA UPYA (3)

*Wafanyakazi vituoni wachota mamilioni, utata wa majina waibuka

*UDART yakusanya fedha bila ulinganisho wa fedha, Serikali yaja juu


Na BAKARI KIMWANGA-DAR ES SALAAM

WIZI wa kutisha. Ndivyo unaweza kusema baada ya kubainishwa kwa wizi wa mamilioni ya shilingi katika vituo vya mabasi ya mwendokasi yanayoendeshwa na Kampuni ya UDART.

Uchunguzi wa MTANZANIA umebaini kuwepo kwa mwingiliano wa majukumu katika ukusanyaji wa fedha vituoni kati ya Kampuni ya UDART na Maxcom ambao ndiyo wenye jukumu la ukusanyaji wa fedha kwa mujibu wa sheria.

Mgogoro kati ya kampuni hizo mbili umesababisha zifikishane mahamakani huku UDART wakitaka kuachiwa majukumu yote ya uendeshaji, likiwamo la  ukusanyaji wa fedha wakati hawana teknolojia ya kisasa  ya ukusanyaji wa nauli na matumizi  ya tiketi za kieletroniki.

 

UPIGAJI WA MAJINA

Uchunguzi wa MTANZANIA umebaini kuwepo upotevu mkubwa wa fedha; Mei 11, mwaka huu, baadhi ya wakusanya nauli katika vituo hivyo wamebainika kuiba fedha kwa kutumia waingiaji watatu katika mashine moja kwa nyakati tofauti (Ticketing office machines).

Kwa mujibu wa uchunguzi, watumishi hao huingia asubuhi kwa jina jingine, mchana kwa jina jingine na jioni kwa jina jingine na wakati wa kuwasilisha fedha, huwasilisha zile tu walizokusanya kwa jina moja na kiasi kingine walichokusanya  kwa majina mengine mawili, huwa hawaziwasilishi.

Msingi wa tatizo hili ni muingiliano wa majukumu kati ya UDART na Maxcom hali ambayo hutoa mwanya kwa watumishi kutumia udhaifu uliopo kujitengenezea utaratibu wa kuiba fedha nyingi.

Katika uchunguzi wake, MTANZANIA limebaini kwamba katika kituo kimoja cha Ubungo Maji, zaidi ya Sh. milioni 11 ziliibiwa kwa siku moja.

Hilo limezua maswali kadhaa; kwa mfano, Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ina vituo zaidi ya 27, kwa wizi unaofanyika ni kiasi gani cha fedha kitakuwa kinapotea?

Na je, fedha zinazopotea ni nani atakayewajibika kuzilipa kwa utaratibu unaoendelea sasa chini ya UDART wa kukusanya fedha kiholela?

Serikali haini kuwa itapata hasara kwenye mradi kutokana na wizi huu unaosababishwa na mgongano wa UDART na Maxcom?

 

MAAMUZI YA VIKAO

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya DART kimeliambia MTANZANIA kuwa, mamlaka za juu za wakala huyo ziliingilia kati suala kwa kutoa agizo la kuheshimiwa kwa maamuzi ya vikao mbalimbali ambavyo pia, Serikali ilishiriki ikiwakilishwa Msajili wa Hazina.

 

Tayari zimeundwa kamati mbili zilizo chini ya Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambapo pamoja na mambo mengine zilipata kutoa agizo la kutaka huduma vyingine kwenye mradi huo zitolewe kama ilivyokuwa awali, wakati taratibu za makabidhiano zikiendelea.

UBABE WA UDART 

Katika hali ya kushangaza, wakati wakusanya nauli waliopewa kazi hiyo, Kampuni ya Maxcom wakifanyakazi yao ya kukusanya kwa mfumo wa kisasa wa kutumia rekodi zilizorithiwa na DART, kwa upamde mwingine watumishi wa UDART huingia na magari yao na kukusanya fedha hizo kutoka kwa wakusanya nauli wa vituoni bila kufanya ulinganisho wa kiasi ambacho anakabilidhiwa na mtumishi husika.

 

UAMUZI WA WAKALA

Kwa mujibu wa barua ya Mtendaji Mkuu wa DART, ya Mei 11, mwaka huu kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa UDART Plc, alieleza kusikitishwa na hali hiyo huku akihoji hatua ya makabidhiano kwenye makaratasi jambo ambalo halitoshi kupata ukweli wa kiasi cha fedha kilichokusanywa.

Katika barua ambayo MTANZANIA inayo nakala, yenye Kumb. Na BA.32/291/01-F/6 iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Ronald Lwakatare, alihoji hatua ya ukusanyaji wa fedha unaofanywa na UDART huku maofisa wa Maxcom wakiwa hawajashirikishwa kwa hatua yoyote.

Katika barua hiyo, Lwatakate anaeleza wazi kuwa hali hiyo ndiyo inayosababisha watumishi kujichotea fedha kana kwamba hazina mwenyewe.

“Tunafahamu kwamba watumishi hawa wamesoma na wanaona fursa hizi zinazojitokeza na hivyo wanazitumia kwa maslahi yao na kulitia hasara taifa. Wakala wa Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka ndiyo unaoratibu zoezi hili.

“Nachukua fursa hii kukuagiza uache mara moja kwenda kukusanya fedha hizo kwenye vituo na kuiacha kazi hii ifanywe na Kampuni ya Maxcom kama ilivyokuwa awali hadi hapo taratibu rasmi za makabidhiano zinakapokamilika.

“Nakukumbusha na kukutaka kurejea kwenye maazimio ya kikao chetu kilichofanyika chini ya usimamizi wa Msajili wa Hazina (9/5/2018) ambacho ulishiriki na kusikia maagizo yote.

“Kwa barua hii, Maxcom atasimamia huduma zote kuanzia ukataji tiketi hadi uwasilishaji wa fedha benki, hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo. Ninaamini na wala sitarajii kuona unaendelea kulazimisha kuchukua fedha vituoni.

“Tuliache jukumu hili mikononi mwake ili awepo mtu wa kubeba mzigo wote wa hasara itakayojitokeza endapo kutakuwa na ulegevu katika usimamizi au kutokea upotevu,” inasomekana baria ya Mhandisi Lwakatare kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa DART.

Nakala za barua hiyo imepelekwa kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Mhandisi Mussa Iyombe.

 

UTETEZI TATA UDART

Katika kile kinachoonekana kuficha ukweli wa kilicho nyuma ya mgomo wa wafanyakazi wanaokatisha tiketi vituoni, Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Deus Bugaywa alisema busara ndiyo iliyowatuma kutoa usafiri bure.

Alisema kampuni hiyo imekosa mapato yanayokadiriwa kuwa kati ya Sh milioni 70 hadi Sh milioni 90 kwa siku, lakini iliona ni busara kutoa huduma ya usafiri bure kuliko wananchi kukosa huduma hiyo.

“Kusafirisha abiria bila malipo ni hasara kubwa kwa kampuni, lakini tumezingatia umuhimu wa safari za abiria wetu na heshima ya mradi huu ambao umekuwa ukisifika kimataifa. Hasara iliyopatikana haizidi madhara ya kusimama kwa huduma,” alisema

Hatua ya kugoma kwa wafanyakazi hao imetokana na UDART kushindwa kuwalipa mishahara  ya Aprili na Mei, baada ya kumalizika kwa mkataba ambapo wao waliahidiwa wangeingia kwenye mkataba na wafanyakazi hao.

Kutokana na kutokuwepo kwa wafanyakazi hao wanaokatisha tiketi, wakazi zaidi ya 70,000 wa Jiji la Dar es Salaam walisafiri bure kuanzia Ijumaa wiki iliyopita hadi jana.

 

HALI ILIVYOKUWA

Suala la tiketi lilianza kuzua taharuki tangu wiki iliyopita katika baadhi ya vituo.

Wasafiri wanaotumia mabasi hayo walifurahia kusafiri bure kwani ili kupata huduma hiyo hawakuhitaji kupanga foleni kama ilivyo siku nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles