NI mfululizo wa ukatili wa kutisha kati ya wakulima na wafugaji! Juzi tena mtu mmoja alinurika kifo baada ya kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya  shingo.
Mbali na ukatili huo, watu wengine wanane walijeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea kijiji cha Dodoma Isanga juzi.
Mapigano hayo yalikuja siku mbili baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, kuonya kuhusu Taifa kunyemelewa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.
Kwamba hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje.
Mtu aliyekumbwa na mkasa huo ni Agustino Mtuti ambaye juzi saa tano asubuhi alipatwa na mkasa huo baada ya kuibuka mapigano makali.
Kwamba alisikia kelele zikipigwa na watu ambao wanaomba msaada baada ya wananchi kulalamikia kitendo cha wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba yao ya mahindi.
Baada ya Mtitu kufika eneo la tukio na kuhoji sababu za wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima, mmoja wa  wafugaji hao alimchoma mkuki mdomoni ambao ulitokea upande wa pili wa shingo.
Baada ya tukio hilo, wafugaji walikimbia na kuacha ng’ombe wao shambani  ambao walichukuliwa na wananchi.
Baada ya muda mfupi, wafugaji walirudi kuwachukua ng’ombe wao ndipo mapigano makali yakazuka, huku wakulima wakijeruhiwa vibaya.
Â
Tunamuunga mkono
Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule (Chadema), ambaye amelaani   vikali tukio hilo na kuiomba Serikali kufanya kazi  ya ziada ili kupugunguza mapigano hayo.
Tunasema lazima Serikali iweke  miundombinu sahihi kwa kila kundi ili kuepuka mwingiliano, na hata mapigano yanayoweza kuzuilika kati ya wakulima na wafugaji.
Tunasema kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro, iliilazimu Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuunda kamati maalumu ya wataalamu ili kuweza kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Timu hiyo ilihakiki mipaka ya vijiji sita ambavyo vina migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji na kusababisha maafa wilayani humo.
Vijiji vilivyozungukiwa na timu hiyo ni Bonde la Mpunga la Mgongola ambavyo ni Hembeti, Dihombo, Mkindo Sindoni, Mkindo kwa Boma, Kambala na Kikundi.
Hata mapigano ya kila wakati yamekuwa yakiripotiwa na kusabisha mauaji na mifugo baina ya wakulima na wafugaji.
Tunasema sasa uchunguzi utoe ilichokigundua na suluhusho la kukomesha kabisa mapigano haya ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kilosa na Bonde la zima la mto Kilombero.
Tunasema Serikali sasa ikomeshe kabisa mauaji haya ambayo yamekwisha kuwachosha Watanzania.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, alishuhudia mifugo iliyouawa wakati akiwa Waziri wa Mifugo.
Tunasema sasa ni waziri anayedhibiti vyombo vya ulinzi, sasa naye asaidie kuona kuwa mauaji haya yanakoma kabisa nchini.