SERIKALI IZIME MAUAJI YA WAKULIMA, WAFUGAJI

katuni-pg-6NI mfululizo wa ukatili wa kutisha kati ya wakulima na wafugaji! Juzi tena mtu mmoja alinurika kifo baada  ya  kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya  shingo.

Mbali na ukatili huo, watu wengine wanane walijeruhiwa vibaya na  kulazwa katika Hospitali  ya wilaya  ya Kilosa mkoani Morogoro kutokana na mapigano  ya  wakulima  na  wafugaji yaliyotokea kijiji cha Dodoma  Isanga juzi.

Mapigano hayo yalikuja siku mbili baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, kuonya kuhusu Taifa kunyemelewa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.

Kwamba hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje.

Mtu aliyekumbwa na mkasa huo ni Agustino Mtuti ambaye juzi saa tano asubuhi alipatwa na mkasa huo baada ya kuibuka mapigano makali.

Kwamba alisikia  kelele zikipigwa na watu ambao wanaomba msaada baada ya wananchi kulalamikia kitendo cha  wafugaji  kuingiza  mifugo  katika  mashamba  yao ya mahindi.

Baada  ya Mtitu kufika eneo la tukio na kuhoji sababu za wafugaji  kuingiza mifugo kwenye mashamba  ya wakulima, mmoja wa  wafugaji hao alimchoma  mkuki mdomoni ambao ulitokea upande  wa  pili  wa  shingo.

Baada ya tukio hilo, wafugaji  walikimbia  na kuacha ng’ombe wao shambani  ambao walichukuliwa  na wananchi.

Baada ya muda mfupi, wafugaji walirudi kuwachukua  ng’ombe  wao ndipo mapigano makali yakazuka, huku wakulima wakijeruhiwa vibaya.

 

Tunamuunga mkono

Mbunge  wa Mikumi, Joseph  Haule (Chadema), ambaye  amelaani    vikali  tukio hilo na kuiomba  Serikali  kufanya  kazi  ya ziada ili  kupugunguza  mapigano hayo.

Tunasema lazima Serikali iweke  miundombinu  sahihi  kwa  kila  kundi  ili  kuepuka  mwingiliano, na hata mapigano yanayoweza kuzuilika kati ya wakulima na wafugaji.

Tunasema kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro, iliilazimu Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuunda kamati maalumu ya wataalamu ili kuweza kufanya uchunguzi wa suala hilo.

Timu hiyo ilihakiki mipaka ya vijiji sita ambavyo vina migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji na kusababisha maafa wilayani humo.

Vijiji vilivyozungukiwa na timu hiyo ni Bonde la Mpunga la Mgongola ambavyo ni Hembeti, Dihombo, Mkindo Sindoni, Mkindo kwa Boma, Kambala na Kikundi.

Hata mapigano ya kila wakati yamekuwa yakiripotiwa na kusabisha mauaji na mifugo baina ya wakulima na wafugaji.

Tunasema sasa uchunguzi utoe ilichokigundua na suluhusho la kukomesha kabisa mapigano haya ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kilosa na Bonde la zima la mto Kilombero.

Tunasema Serikali sasa ikomeshe kabisa mauaji haya ambayo yamekwisha kuwachosha Watanzania.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba,  alishuhudia mifugo iliyouawa wakati akiwa Waziri wa Mifugo.

Tunasema sasa ni waziri anayedhibiti vyombo vya ulinzi, sasa naye asaidie kuona kuwa mauaji haya yanakoma kabisa nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here