Na RAMADHAN HASSAN, DODOMA
WAZIRI wa Madini, Angela Kairuki amesema Serikali inaendelea kudhibiti utoroshaji wa madini katika maeneo ya mipaka.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa katika Wiki ya Azaki wakati akifungua jukwaa la sekta ya uziduaji wa madini iliyoandaliwa na Haki Rasilimali.
Waziri huyo alisema Serikali inaendelea kudhibiti utoroshaji wa madini katika maeneo ya kutokea nchini.
Pia alisema wizara yake ipo katika hatua nzuri ya kukamilisha ujenzi wa vituo saba vya mfano kwa ajili ya mafunzo ya uongezaji thamani madini, uchimbaji salama na kuongeza uzalisaji na tija ili kukuza mapato kwa wachimbaji wadogo na Serikali.
“Wizara ya Madini imeweka vipaumbe ambavyo vitawezesha sekta ya madini nchini kuimarika na kunufaisha Watanzania wote.
“Vipaumbele hivyo ni pamoja na uwajibikaji katika sekta ya madini na uziduaji kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali ya madini,” alisema.
Alisema katika kufanikisha hilo, tayari Serikali inayo mikakati madhubuti ya kuimarisha ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na ya uchimbaji mdogo ili kupata taarifa sahihi za maeneo ya uwekezaji, uzalishaji, mauzo na kodi mbalimbali.
Kairuki alisema vipaumbele vingine ni kuimarisha ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwanda, kufuatilia taarifa za ununuzi na uuzaji kwa wafanyabiashara wa madini na kufuatilia wadaiwa wa tozo mbalimbali za madini kwa mujibu wa Sheria.
“Na kuhakikisha kuwa tunadhibiti uchimbaji haramu wa madini, kuboresha na kuimarisha mfumo wa utoaji wa leseni na madini na kutunza taarifa zake.
“Pia tutawaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini katika kuhakikisha wanaendelea kutoka hatua waliopo sasa na kuwa wachimbaji wa kati na hatimaye wakubwa.
“Wizara imetenga jumla ya maeneo manne nchini kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuendelea kutenga maeneo hayo na kabla ya kugaiwa yatabainishwa ili kuepusha kufanya uchambuzi kwa kubahatisha,” alisema.