28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Tizeba aikosoa TRA

                   Na DERICK MILTON, BARIADI

WAZIRI wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kubadilisha mfumo wanaoutumia katika kukusanya kodi kwa wafanyabiashara kutokana na kutokuwa rafiki kwao.

Alisema mfumo ambao TRA imekuwa ikitumia katika kukusanya kodi mbalimbali hapa nchini, umekuwa si rafiki kwa wafanyabiashara na kusababisha baadhi yao kukimbia biashara zao.

Dk. Tizeba alitoa kauli hiyo alipotembelea banda la TRA katika maonesho ya viwanda vidogo (SIDO) kitaifa yanayofanyikia viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Alisema moja ya mfumo huo ni ule ambao mfanyabiashara anatakiwa kulipa kodi ndani ya siku 90 kutoka siku ya kwanza aliyoanza kufanya biashara yake, ambao alisema hauwatendei haki wafanyabiashara.

“Kwanini huyu mfabyabiashara anapoanza biashara yake asiachwe kwanza mpaka mwaka mzima ndipo aweze kulipa hiyo kodi, maana akifanya biashara mwaka mzima atakuwa tayari amepata faida na atalipa kodi, hawezi kukimbia maana amepata faida.

“Lakini kwa mfumo huu, miezi mitatu anatakiwa kulipa kodi haujui kama amepata faida au hajapata, mimi siukubali hata kidogo, hauko rafiki sana na wakulima wetu na wafanyabiashara, unawafanya kuacha na kukimbia bishara zao,” aliongeza Dk. Tizeba.

Hata hivyo waziri huyo alipatiwa majibu ya jambo hilo kutoka kwa Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka mamlaka hiyo, Gabriel Mwangosi kwamba sheria iliyopitishwa na Bunge ndiyo inataka hivyo.

Waziri Tizeba alikataa majibu hayo kwa kueleza kuwa mbali na sheria kupitishwa na wabunge, wanaoanzisha sheria ili iweze kutungwa ni wataalamu kutoka katika mamlaka hiyo.

Meneja huyo alimweleza Waziri Tizeba kuwa mfumo huo ulipendekezwa na kuonekana sahihi kwa wafanyabiashara ili wasiweze kukwepa kodi kama wangelitakiwa kulipa mwisho wa mwaka.

Mbali na hilo, Meneja huyo alieleza kuwa sheria ndivyo inavyotaka wao kama mamlaka kukusanya kodi kwa mfumo huo.

Akiwa katika banda la Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Waziri Tizeba alizitaka mamlaka hizo kugeukia vyakula wanavyopika wananchi kila siku katika meneo yao.

Alisema mamlaka hizo zimejikita sana katika vyakula vinavyotoka nje ya nchi na vile vilivyofungashwa kwenye mifuko na makopo, wakati vyakula vinavyotumika kila siku na wananchi vikiwa haviangaliwi ubora wake.

“Kwenye sekta yangu ya kilimo mazao yake mengi hayana ubora, chakula cha mifugo nacho hakichunguzwi na mamlaka hizi, tubadilike, tuchunguze pia hata chakula wanachotumia majumbani wananchi kila siku,” alisema Tizeba.

Akiongelea maonesho hayo, Dk. Tizeba aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuhakikisha wanajifunza zaidi, teknolojia mbalimbali za ujasiriamali katika kuongeza uzalishaji kwenye bidhaa zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles