Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali imesema kuwa kuwepo kwa vikao na wadau ni ishara kuwa ina nia na dhamira njema kwa sekta ya habari nchini.
Hayo yameelezwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye wakati wa kikao chake na wadau hao kilicholenga kupokea maoni yao.
“Kuwepo kwa vikao na wadau ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ina nia na dhamira njema kwa sekta ya habari. Niwahakikishie kuwa serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inayo nia ya dhati katika jambo hili,” amesema Waziri Nape
Aidha, Waziri Nape amewahakikishia Wadau wa Sekta ya Habari kuwa Serikali imepokea maoni yao kuhusu marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.
“Nimekuja mwenyewe kuwasilikiliza na imani yangu ni kuona sekta inaendelea kukua” ameongeza Waziri Nape.
Wadau walioshiriki kikao nicho ni pamoja na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama wa Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) na MISA- Tanzania.