25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Mpango atoa maagizo Tamisemi

Na Clara Matimo,  Mwanza

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, ameziagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kuandaa mpango mkakati utakaoainisha namna ya kufanya uwekezaji na kuendeleza fukwe zilizopo nchini.

Amesema asilimia kubwa ya fukwe zilizopo nchini hazijaendelezwa na zinakabiliwa na changamoto ya uharibifu wa mazingira kutokana na shughuli za kibinadamu zinazofanywa kando kando ya fukwe hizo.

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, akiagana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, baada ya kumaliza kufungua kongamano hilo.

Dk. Mpango ametoa agizo hilo leo Novemba 23, 2022 jijini Mwanza wakati akifungua Kongamano la Jukwaa la Maendeleo Endelevu lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi ambalo mada kuu itakayojadiliwa ni Usimamizi Madhubuti wa Fukwe kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii nchini Tanzania.

“Nataka kazi hiyo ikamilike haraka na nipatiwe taarifa ya mipango hii haraka iwezekanavyo ni matumaini yangu kongamao hili litajadili kwa kina na kuja na mapendekezo mazuri ya namna ya kuboresha mifumo ya usimamizi, ulinzi na uwekezaji ili tuweze kutoka hapa tulipo.

“Nia ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha maendeleo endelevu ya taifa letu kwa kuzingatia malengo na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2025 inayolenga kufikia uchumi jumuishi wa taifa ikiwa na kipato cha kati na maisha bora kwa kila mwananchi ili kufikia malengo hayo  uwekezaji katika fukwe hatuwezi kuuacha nyuma.

“Tubadilike tuwe wabunifu zaidi na tutumie rasilimali tulizopewa na Mungu kujiletea maendeleo lakini kwa kuzingatia matumizi bora na uendelevu wa ardhi na utunzaji wa mazingira kwa faida ya kizazi chetu na kijacho,”ameeleza Dk. Mpango.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Meja Jenerali Suleiman Mzee, amesema mkoa huo umejipanga kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa kuimarisha viwanda, kilimo, biashara na kuongeza juhudi katika kuhifadhi mazingira kwani hadi sasa ni miongoni mwa mikoa ambayo inafukwe nzuri za kuvutia ukiwa na jumla ya fukwe 31 ambazo zinatembelewa na wenyeji na wageni kutoka nje ya mkoa na nchi.

“Kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 wananchi wenyeji na wageni kutoka nje wapatao 11,280 walitembelea fukwe hizo na kipindi cha  mwaka wa fedha 2022/2023 hadi Novemba wananchi wenyeji pamoja na wageni kutoka nje zaidi ya 5,243 wameishatembelea fukwe hizo.

“Manufaa ya fukwe zilizopo mkoani hapa ni pamoja na kuwa ni eneo la kivutio kwa wageni pia jamii inapata eneo la kupumzikia na hivyo kuimarika kwa uchumi wa mkoa huu,”amesema Meja Jenerali Suleiman Mzee .

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo, amesema lengo la kongamano hilo  la siku mbili ambalo litahitimishwa Novemba 24, 2022 ni kuhamasisha maendeleo jumuishi na endelevu yanayozingatia uzuri wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za fukwe kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Akitoa wasilisho kuu la  kongamano hilo mbele ya Mgeni Rasmi Dk. Mpango, Profesa Ali Namangaya kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi alisema uendelezwaji wa fukwe unakabiliwa na changamoto ya uratibu dhaifu na kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwa wadau kwenye kuwekeza na kupanga matumizi ya fukwe hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles