25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI ILIVYOMBEBA LISSU USHINDI TLS

Na ELIZABETH HOMBO


SIKU chache kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Machi 18, mwaka huu taifa liliingizwa kwenye mjadala ambao haukutarajiwa.

Waliosababisha mjadala huo ni Serikali yenyewe aidha kwa kujua au kutokujua kwani ilianza kuonyesha woga au ubaguzi kwa TLS baada ya kuona Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amechukua fomu ya kugombea urais wa chama hicho.

Rais John Magufuli mwenyewe alianza kwa kutanabaisha kuwa hawezi kuchagua jaji kutoka katika chama hicho kwa sababu kina mlengo wa kisiasa.

Akihutubia sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria kwenye Uwanja wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alikilaumu TLS kwa kujigeuza kuwa chama cha siasa badala ya kufuata weledi wa taaluma yao.

“Serikali yangu haitashirikiana na TLS inayosukumwa na upinzani. Nitapata shida sana kuteua Jaji kutoka Tanganyika Law Society kama mtakuwa mnafanya mambo yenu kwa kutumiwa. Niwaambie kwamba mtafanya kazi zetu bila kujali masilahi ya taifa, mtashindwa,“ alionya Rais Magufuli.

Sababu nyingine iliyoleta mjadala mkubwa ni kutokana na kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe aliyoitoa Februari 15, mwaka huu mjini Dodoma pale aliposema kwamba serikali haiwezi kuona TLS inajiingiza katika siasa na kama watataka hivyo, hatasita kuifuta Sheria ya TLS sura ya 307 iliyosababisha kuanzishwa kwa chama hicho.

Baadaye Lissu aliibuka na kusema kauli ya Rais Magufuli ni sababu ya msingi iliyomsukuma kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo.

Hatua hiyo ndiyo iliyochagiza hamasa kwa wanachama wa TLS na wananchi nje ya taaluma ya sheria na ndiyo maana uchaguzi wa mwaka huu uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Arusha (AICC) ulikuwa na mvuto wa aina yake kuliko chaguzi zote zilizopata kufanyika huko nyuma.

Tofauti na mwaka huu, uchaguzi wa TLS wa miaka iliyopita haukuwa na hamasa na wala haukujulikana na wengi wakati ulipokuwa ukifanyika.

Ingawa TLS ni miongoni mwa taasisi kongwe hapa nchini iliyoanzishwa mwaka 1954, haikuwa ikijulikani sana miongoni mwa Watanzania.

Hamasa hii ilitokana na nini?

Kabla ya uchaguzi huu, TLS ilionekana kama imelala lakini tangu ijulikane Lissu anagombea, vyombo vya habari vimekuwa vikiandika huku mijadala ikitawala kwenye mitandao ya jamii. Hilo pia limewafanya Watanzania wengi waanze kukifahamu chama hicho.

Mbali na hilo, ni jambo lililo wazi kwamba hamasa ya uchaguzi wa mwaka huu kwa kiasi kikubwa imesababishwa na kauli ya Rais John Magufuli pamoja na Dk. Harrison Mwakyembe aliyetishia kuifuta TLS.

Hamasa nyingine ambayo inatajwa kuchangia uchaguzi huu ni asilimia kubwa ya mawakili kuwa na imani na Lissu kuwa anaweza kuitoa TLS hapo ilipo kwa sababu ilionekana kama imepoteza mwelekeo na inatokana na ukweli kwamba Lissu amekuwa na misimamo dhabiti katika sheria.

Aidha kitendo cha Lissu kukamatwa mara kwa mara na huku akisimama mwenyewe kujitetea na baadaye mahakama kutoa hukumu zinazoonesha hana hatia, inadhihirisha kwamba wakili huyo machachari ataleta mabadiliko ndani ya chama hicho.

Lissu alikamatwa mara kadhaa ikiwamo Februari 6, mwaka huu wakati anahudhuria vikao vya Bunge mjini Dodoma kwa agizo la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam bila sababu inayoonekana kuwa ya msingi.

Ilidaiwa kuwa alikamatwa ili achelewe kuchukua na kurudisha fomu za kuwania nafasi hiyo.

Machi 16, mwaka huu pia alikamatwa nyumbani kwake mjini Dodoma akiwa anajiandaa kwenda Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam akidaiwa kutotii sheria.

Alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alikosomewa mashitaka matano ikiwamo kutoa maneno ya uchochezi yenye hisia za kidini.

Lissu alifikishwa mahakamani hapo, ikiwa ni siku moja kabla ya uchaguzi huo kufanyika na kulikuwa na taarifa kwamba pengine asingeweza kushiriki, lakini baadaye taarifa zilisema taratibu na kanuni za TLS zinaruhusu mgombea kuchaguliwa hata kama hayupo katika ukumbi wa kupigia kura.

Lakini baada ya kuachiwa kwa dhamana, alisafiri kwa ndege ya kukodi na kuwasili Arusha jioni na kwenda moja kwa moja ukumbini.

Kingine kinachotajwa ni kitendo cha Lissu kujitolea kuwatetea vijana ambao wamekuwa wakikamatwa kwa uchochezi.

Na kitendo cha Rais Magufuli kutoa kauli kwamba mawakili ambao wamekuwa wakiwatetea wahalifu nao wakamatwe, imechangia hamasa ya uchaguzi huo.

Kwamba kisheria Mahakama ndiyo inayotoa hukumu kwa mtuhumiwa na kwamba ni haki ya wakili yeyote kumtetea mteja wake hadi pale Mahakama itakapotoa hukumu.

Sababu nyingine ni kitendo cha baadhi ya wabunge na viongozi wengine wa upinzani kukamatwa kwa uchochezi na kuwekwa ndani huku wakinyimwa dhamana wakati masharti ya dhamana yako wazi.

Sababu zingine ambazo zimembeba Lissu ni pamoja na idadi kubwa ya vijana wa TLS ambao wanampenda mwanasiasa huyo na kutaka kuionyesha serikali kuwa chama hicho ni huru.

Ni dhahiri kwamba wanasheria hao vijana wamekuwa na mwelekeo wa kutaka mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa taasisi hiyo na kwamba wamemwona Lissu ni mtu pekee anayeweza kuwakilisha taswira hiyo.

Nyingine ni kitendo cha mawakili Godfrey Wasonga na Onesmo Mpinzile ambao ni wanachama wa TLS, kufungua kesi Dar es Salaam na Dodoma wakipinga uchaguzi huo, ambazo zilitupwa na mahakama.

Kwanini serikali inamhofia Lissu?

Majukumu ya TLS ni kulinda na kukuza viwango vya taaluma ya sheria na mwenendo wa wanasheria nchini, kuwezesha upatikanaji wa maarifa ya kisheria kwa wanachama wake na watu wengine.

Mengine ni kuisaidia serikali na mahakama katika mambo yote yanayohusu sheria, utawala wa sheria na utekelezaji wa sheria.

Pia kulinda na kuusaidia umma wa Watanzania yanayohusu au kuendana au kutokana na sheria, kuchangisha au kukopa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli zake.

Majukumu mengine, kujihusisha na uwekezaji wa fedha au rasilimali nyingine kama TLS itakavyoona inafaa, kufanya kitu kingine chochote kila kinachoendana au kuwezesha kutekeleza malengo yake.

Kutokana na majukumu hayo ambayo TLS imepewa kwa mujibu wa sheria pamoja na jinsi inavyomfahamu Lissu pengine ndiyo sababu ambayo inaipa hofu serikali, kwamba haitoweza kuiyumbisha.

Mambo anayotakiwa kuyafanya Lissu

Ni dhahiri kwamba Lissu wa sasa katika TLS anatakiwa kupunguza au kuacha kabisa kuingiza harakati za kisiasa katika chama hicho kwa sababu ameaminiwa na wenzake ambao kwa asilimia kubwa si wanasiasa.

Kutokana hilo, wapo ambao wanamshauri Lissu kwamba ili aitumikie vyema nafasi yake ya kitaaluma, anatakiwa ajiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema ili chama chake kiweze kuibua kipaji kingine kama ilivyokuwa kwake.

Pia ajiuzulu nafasi yake ya uwaziri kivuli bungeni ili hoja zake za kisheria bungeni zitazamwe kwa jicho huru na wabunge wa pande zote.

Lakini anaweza kutumikia vyeo vyote kwa pamoja kama ataweza namna ya kutenganisha mwingiliano katika mambo hayo kama ambavyo wanachama na wanataaluma wenzake ndani ya TLS wanavyoamini ndiyo maana wakampigia kura.

Pamoja na hilo, mara baada ya kuapishwa Lissu alisema chini ya uongozi wake itakuwa ni mwisho kwa chombo au mtu yeyote kukitishia chama hicho.

“Ni sisi wenyewe tulioruhusu Serikali ituingilie, iwe ni mwisho. hivyo tuanze mwanzo mpya na turuhusu siku mpya ije.

 “Iwe mwisho sasa kwa chama hiki kutishwa na mtu au chombo chochote, iwe mwisho kwa mawakili kutishwa na kukamatwa ovyo, iwe mwisho kwa mahakimu na majaji kupokea maelekezo.

“Mimi ni mwanachama wa Chadema ni kiongozi, ni mbunge, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, nawahakikishia sitaileta Chadema ndani ya TLS na sitaipeleka TLS ndani ya Chadema.

“Sijagombea kama mwanachama wa Chadema bali nimegombea kama mwanachama wa TLS aliye ndani ya Chadema,”.

Huyo ndiye Lissu ambaye serikali inamuhofia lakini wanataaluma wenzake na wananchi wanamuamini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles