27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

MVUMILIVU HULA MBOVU

MAMBO mengi ni jinsi unavyojipanga na uamuzi wako. Jinsi unavyojiamini kwamba utatimiza malengo yako na jinsi utakavyofanikiwa. Mafanikio yakiwa endelevu ni kwamba wewe haujatetereka katika malengo yako na unaweza kurudia mara zote kile ulichokianza mara ya kwanza.

Wengi wanaogopa kitu kigeni na hasa kama wanaona hiki kitu geni kinaleta mashindano ya namna fulani au wakiona kwamba ile sehemu waliyoshika inaweza kupotea. Huo ni ubaguzi.

Ubaguzi uwe ni wa kidini, kijiografia. kiitikadi, kiuchumi au sababu nyingine yoyote, haiwezi kusaidia kuimarisha ushirikiano wa kijamii na uelewa, haiwezi kuongeza ushirikishwaji wa jamii na mshikamano, kuvumiliana, kuheshimu ujenzi na ujenzi wa miundombinu kwamba moyo mshikamano wa jamii. Na badala yake hujenga chuki juu ya chuki usio na uzalishaji.

Diaspora wanataka kuwa sehemu ya jamii hii lakini urasimu mwingi kwa masuala ya msingi inawakwamisha. Sasa inaonekana kwamba urasimu huu unanyang’anya au unaweka mipaka kwa Diaspora kushiriki katika maendeleo ya nchi yetu.

Kuwa mpole nchi hii ni kutokufahamu haki zako, wakati mwingine inabidi upige kelele kwa kistaarabu usikilizwe wahenga, wagweno na wandamba husema “Mvumilivu hula mbivu” lakini kwa mfumo ambao unaonekana kwa takribani ambazo zinajitokeza mara kwa mara mie naona wakati mwingine ‘Mvumilivu hula mbovu 

Zungumza na watu upate viatu ni  njia nzuri ya kuchukua. Usipozungumza na kuandika na kujadiliana na wengine hakuna ambalo litapatikana na viatu utavikosa. Suala moja ambalo Diaspora wanaweza kuliangalia na kitu ambacho kinanisikitisha sana ni kuona watu ambao wanaomba mitaani.  Hii inaonyesha nchi kuwa na hali gani. Kama kuna baadhi ya wananchi wake wanaomba, hasaa wazee, vilema na watoto kuna mahali tumekosea.

Hii nchi si kwamba haina uwezo wa kuwaangalia vilema na wazee wake, uwezo upo, malengo yapo tunaanguka kwenye mipango, utendaji na utekelezaji. Ni jukumu la nani kuona kwamba huduma za kuhakikisha kwamba hawa ambao hawajiwezi wanapata nafuu na kuwezeshwa kuishi maisha ya kawaida. 

Tukijipanga hili suala halitakuwapo kabisa, halitakiwi kuwapo. Sisi kama wazawa na hii namaanisha wote ambao tunaishi ndani na nje ya Tanzania kweli tumeshindwa kujipanga na tumeshindwa kuunda mfumo ambao utaweza kuwahudumia vilema, wazee na watoto wanaoomba mitaani? Suala hili linaweza kutatuliwa kama katika hii changamoto ya kijamii inaangaliwa si kama tatizo moja la kipekee ila kama mfumo wa kimaisha ambao unagusa sehemu zote za jamii.

Ni wajibu wa jamii kujipanga na kuorodhesha mahitaji yao hasa kwa upande wa vilema na wazee. Je, kuna vilema wangapi? Wazee wangapi? Wanaishi wenyewe? Au nyumbani kwa jamaa na ndugu ? Wana mtandao gani? Nakadhalika nakadhalika. Picha ikipatikana ni rahisi kutengeneza mazingira ambayo yatarahisisha upokeaji wa huduma hizo na kusambaza na pia mfumo endelevu utaandaliwa ili hii sehemu ya jamii isiende mbali ili kupata huduma hizo.

Jamvi la jamii likiimarishwa basi ni vigumu wazee na vilema wetu kuanguka chini mpaka kuanza kuomba na kutoka mbali na jamii yake. Haya masuala ni muhimu kuangalia kama uhamaji wa vijana na watu wenye nguvu kukimbilia mijini kwa sababu ya ukosefu wa kazi au sababu zingine kama elimu, huduma za hospitali, maji na huduma nyingine za kijamii.

Mpango maalumu ukiwekwa ambao unaangalia mahitaji kuanzia ngazi ya chini na kwenda juu utatuwezesha kutengeneza huo mfumo ambao utasaidia kuleta huduma inayohitajika kwa wakati na ambao utahusu matakwa ya hiyo jamii. Chombo ambacho na hizi ni fikra ambazo wanadiaspora wataunga mkono sana, ni kusaidiana na Diaspora kuangalia hilo swali. Je, ni mchango gani Diaspora wanaweza kutoka hapo na ni mfumo gani utafaa?

Diaspora wakiwezeshwa na kuingizwa katika jamii zetu kama ni sehemu ya jamii yoyote Tanzania, wataweza kusaidia sehemu nyingi sana. Mtandao ambao Diaspora wanao nje utaweza kutumika katika kutatua masuala ya kijamii na hasa haya ya ombaomba. Ushauri wangu, tusipuuze jinsi Diaspora wataweza kuchangia katika changamoto hii, uwezo wa hilo kundi ni mkubwa na ukishirikiana na vikosi chanya basi matatizo mengi yatapungua na miradi mingi itaanzishwa na wengi kutoka kwenye ngazi za chini wataweza kuanzisha miradi midogo midogo ambayo itawatoa kutoka kwenye hali duni.

Hapa ni kutafuta mfumo ambao utawezesha wana Diaspora kushirikishwa katika maendeleo ya nchi. Nguvu ya mtu mmoja haitoshi kunahitajika ushirikiano na uelewa kwamba hapa wote tupo pamoja. Diaspora wakibaguliwa kwa sababu wao wanaishi nje ya Tanzania hapa tunapoteza rasilimali kubwa sana.

Ujuzi, uzoefu na hata kiuchumi. Tanzania ni nchi ya amani na upendo Diaspora wapokelewe kama wawekezaji wengi wa ndani. Milango ifunguliwe na wachukuliwe kama inavyostahili. Diaspora ni ndugu zenu, watoto wenu, baba zenu wajomba zenu, dada zenu na kwa ujumla ni wazao na vizazi vya Tanzania.

Ukisha fahamu hilo, basi ni kujipanga tu na kutekeleza uliyoyalenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles