29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

“Serikali iimarishe upatikanaji wa Dola mwarobaini wa mafuta” -TAOMAC

*Makamba asema hatua madhubuti zinaelea kuchukuliwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Chama cha Waagizaji na Wasambazaji Mafuta Tanzania (TAOMAC) kimeisihi Serikali kuhakikisha kuwa inaongeza nguvu katika upatikanaji wa Dola ya Marekani ili kurahisisha udhibiti wa uhaba wa mafuta nchini.

TAOMAC imebainsiha hayo Dar es Salaam Agosti 5, 2023 wakati wa kikao kilichokutanisha wadau wa Sekta hiyo ya mafuta na Waziri wa Nishati, Januari Makamba lkikiwa na lengo la kuhakikisha bidhaa hiyo hasa ya Petroli inapatikana kwa uhakika maeneo yote nchini.

Katika kikao hicho, TAOMAC walitoa taarifa ya mwenendo wa biashara ya mafuta duniani na hapa nchini pamoja na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mafuta hususan suala la upatikanaji wa dola ya Marekani.

Akizungumza katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa TAOMAC, Salim Baabde alisema uhaba wa dola za Marekani katika soko la fedha kunasabisha waagizaji kupunguza kiasi cha mafuta wanachoagiza kuepuka kuagiza mzigo na kushindwa kuulipia kwa wakati jambo ambalo linaongeza gharama za uendeshaji wa biashara na kuathiri bei ya mafuta kwa mteja wa mwisho.

“Biashara yetu inafanyika kwa kutumia Dola za Marekani na inapotokea dola inakuwa adimu sokoni inaathiri moja kwa moja bei ya uagizaji ambayo mwisho wa siku inaathiri bei ya mafuta kwa mtumiaji wa mwisho,” amesema Baabde.

Aidha, ameonya kuwa hali inaweza kuzidi kuwa mbaya iwapo changamoto ya upatikanaji wa dola haitatuliwa kwa haraka.

“Tunaiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuhakikisha dola zinapatikana kwa kushirikisha benki za biashara ili kuepuka changamoto hii kukua zaidi na kuleta athari kubwa,” amesisitiza Baabde.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAOMAC, Raphael Mgaya alimhakikishia Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuwa pamoja na changamoto hiyo wao wataendelea kuagiza mafuta ingawa kwa gharama kubwa ili kuhakikisha nchi inaendelea kupata nishati hiyo muhimu katika hali ya uhakika na endelevu.

“Tutaendelea kuhakikisha tunalinda dhamana tuliyopewa na Serikali ya kuhakikisha nchi inakuwa na mafuta wakati wote hata kama ni kwa gharama kubwa,” amesema Mgaya.

Vile vile wamemshukuru Waziri Makamba na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa ushirikiano ambao wamekuwa wanautoa kwa tasnia hasa katika vipindi vigumu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali pamoja na kuelimisha umma kuhusu biashara ya mafuta ili kukabiliana na upotoshaji mkubwa hasa mitandaoni kuhusu biashara hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba amewashukuru kwa ushirikiano walioutoa katika kuhakikisha kwamba nchi inapata mafuta muda wote.

Makamba pia alieleza kwamba mlango wake uko wazi wakati wote kwa ajili ya mashauriano.

“Sisi hapa wizarani filosofia yetu ni ile ya open door ambapo yeyote anakaribishwa kwa ajili ya mashauriano na majadiliano. Serikali inaelewa changamoto ambazo sekta inakabiliana nazo kwa sasa na hatua madhubuti zimeendelea kuchukuliwa,” amesema Makamba.

Waziri wa Nishati, January Makamba.

Aidha, Makamba amesisitiza umuhimu wa wadau ikiwemo TAOMAC kuendelea kushikamana na kushirikiana ili kuhakikisha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika kwa ajili ya ustawi wa nchi na watu wake.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishna wa Petroli na Mafuta, Michael Mjinja, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile na wataalamu kutoka Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles