MADRID, HISPANIA
NAHODHA wa klabu ya mabingwa watetezi wa klabu bingwa barani Ulaya, Real Madrid, Sergio Ramos, juzi alivunjika pua katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini Hispania.
Wapinzani hao walikutana kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo msimu huu na mchezo huo ulimalizika huku zikitoka bila ya kufungana kwenye Uwanja mpya wa Atletico Madrid, Wanda Metropolitano.
Ramos ambaye alikuwa anaongoza safu ya ulinzi ya Real Madrid, alijikuta akiwa katika wakati mgumu baada ya kuvunjika pua wakati anaokoa mpira wa hatari kwenye eneo la 18 katika dakika ya 36 ya mchezo huo.
Kutokana na hali hiyo, mchezaji huyo anaweza kuwa nje ya uwanja katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya wapinzani wao APOEL, kesho.
Hata hivy,o kocha wa mabingwa hao watetezi, Zinedine Zidane, amethibitisha kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kumkosa mchezaji huyo lakini bado ana kikosi kipana cha wachezaji ambao wanaweza kuziba nafasi iliyo wazi.
“Kuna uwezekano mkubwa wa Ramos kuwa nje ya uwanja katika mchezo dhidi ya APOEL kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni kutokana na kuvunjika pua kwenye mchezo dhidi ya Atletico.
“Madrid ni miongoni mwa timu yenye wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, hivyo wapo wachezaji ambao wataweza kuziba nafasi hiyo, Dani Carvajal yupo kwenye ubora wake na anatarajia kuwa kikosini tena huku akishirikiana na Nacho endapo Ramos anakuwa nje,” alisema Zidane.
Hata hivyo, kocha huyo aliongeza kwa kusema mchezo huo dhidi ya wapinzani wao ulikuwa wa ushindani wa hali ya juu kutokana na ubora wa kila kikosi, bado hawakati tamaa ya kutetea ubingwa.
Matokeo ya mchezo huo wa juzi yanawafanya Real Madrid kuwa nyuma kwa pointi 10, huku wakiwa na pointi 24 baada ya kucheza michezo 12 na kuwafanya washike nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi, wakati huo Barcelona wakiwa vinara na pointi 34, huku Atletico Madrid wakishika nafasi ya nne wakiwa sawa na Real Madrid lakini wakitofautiana kwa mabao.