27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Sera, sheria ya wenye ulemavu kupitiwa upya

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

SERIKALI ina mpango wa kupitia upya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 ili iweze kuendana na wakati.

Akizungumza wakati wa kufunga kongamano la maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani, Ofisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia wenye ulemavu, Joyce Maongezi, amesema tayari Serikali imetenga fedha kufanya mapitio hayo.

Kongamano hilo lililoandaliwa na Shirika la Habari la Kimataifa la Internews lilishirikisha watu wenye ulemavu, mashirika yanayofanya kazi na watu wenye ulemavu na waandishi wa habari.

“Tumekwishaanza kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, tunaendelea kupokea kwa ajili ya kuboresha sera na hatimaye tutaboresha na sheria ya watu wenye ulemavu…na yenyewe kidogo ina mapungufu,” amesema Maongezi.

Amesema pia wanatengeneza kanzidata ya wahitimu mbalimbali wenye ulemavu ili zinapopatikana fursa iwe rahisi kuwaunganisha hasa kwa kada zingine tofauti na ualimu.

Wakichangia mada kuhusu ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya kijamii iliyowasilishwa na Mkufunzi kutoka Internews, Temigunga Mahondo, baadhi ya washiriki wamesema janga la Uviko – 19 limeleta athari kwa watu wenye ulemavu kwa sababu sehemu nyingi mazingira si rafiki.

“Mimi nategemea mkalimani lakini hospitali hakuna mkalimani, unakuta daktari amevaa barakoa hata kumsoma midomo yake inakuwa vigumu, au unakwenda benki unakuta mfanyakazi amevaa barakoa kwahiyo lazima nimwambie aandike ndiyo niweze kupata huduma,” amesema Joyce Jumbe ambaye ni kiziwi.

Joyce Jumbe akichangia mada katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Watu Wenye Ulemavu Duniani lililoandaliwa na Shirika la Habari la Internews. Kushoto ni Mkalimani wa Lugha ya Alama, Beatrice Chiluka.

Naye Paul Yohana ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (Shivyawata), amesema sera bado hazijawekwa katika mazingira rafiki ambayo yanamwezesha mtu mwenye ulemavu kufahamu haki zake katika kuifikia huduma anayoihitaji.

Aidha katika mapendekezo ya washiriki hao yaliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Shirika la Vijana wenye Ulemavu (YoWDO), Rajab Mpilipili, wameshauri mikopo inayotolewa kwa taasisi za elimu ya juu iwe ruzuku kwa watu wenye ulemavu ili kuwahamasisha wengine kusoma kwa bidii na kufikia elimu ya juu.

“Watu wenye ulemavu wamekuwa wakijitahidi kufikia ‘level’ ya elimu ya juu na wengi wakimaliza kupata ajira inakuwa ngumu kwao hivyo kushindwa kulipa mkopo,” amesema Mpilipili.

Mapendekezo mengine ni kwa Serikali kuandaa istilahi zinazohusiana na Uviko – 19 ili iwe rahisi kufikisha mawasiliano kwa viziwi, mwongozo wa ajira kwa watu wenye ulemavu ufanyiwe marekebisho, msamaha wa matibabu kwa wenye ulemavu wasimudu gharama za matibabu, wajawazito wenye ulemavu waruhusiwe kwenda na mtu anayemwamini wanapokwenda kujifungua na kutengwa bajeti ya kutosha ya visaidizi kwa wenye ulemavu.

Awali Mratibu wa Mafunzo kutoka Internews, Shaban Maganga, amesema waliandaa kongamano hilo kuhakikisha wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika jambo lolote lile.

“Kumekuwa na mtazamo potofu katika jamii mtu akiwa na ulemavu anaonekana hawezi kufanya chochote jambo ambalo si sahihi, tukiangalia kaulimbiu inavyoelekeza tunahimiza wapewe kipaumbele katika chanjo na mambo mbalimbali,” amesema Maganga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles