25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Rai Yatolewa kwa Wadau wa Utoaji Haki

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Wilbert Martin Chuma, ametoa rai kwa wadau wote wa Haki pamoja na wananchi kushiriki ipasavyo katika mnyororo wa utoaji haki ili kufikia lengo la utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati kwani haki huinua taifa.

Chuma ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akieleza mafanikio ya Mahakama kwa kipindi cha miaka 60 ya uhuru (1961-2021).

“Kila mtu ana nafasi yake katika kufikiwa kwa haki, kwahiyo kama mwananchi unatakiwa kutoa ushahidi ili kesi iweze kumalizika mapema, kama wewe unahusika na upelelezi kamilisha upelelezi kwa wakati ili shauri liweze kusikilizwa mapema na kama wewe ni mdau yeyote unayehusika na mnyororo huu wa utoaji haki kwa namna moja ama nyingine kila mtu sasa atekeleze wajibu wake,” amefafanua Chuma.

Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Wilbert Martin Chuma.

Aidha, ameongeza kuwa, Mahakama pekee haiwezi kufanikiwa katika mnyororo wa Utoaji Haki Nchini, hivyo Mahakama ya sasa imezidi kuimarisha ushirikiano na wadau wa Mahakama ili kuhakikisha haki inafikiwa na Wadau wanapata haki kwa wakati.

Akibainisha baadhi ya mafanikio ndani ya Mahakama kwa miaka 60 ya Uhuru, Mhe. Chuma amesema kuwa, kumekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya Mahakama ikiwemo uanzishwaji wa Mfumo wa Ufunguaji na Ushughulikiaji wa Mashauri, Matumizi ya Tehama katika Shughuli za Kimahakama, Uwepo wa Mahakama inayotembea (Mobile Court), Mahakama Mtandao (Paperless Court), Uwepo wa Vituo Jumuishi (IJC’s), na Kuimarisha Ushirikishwaji wa Wadau wa Utoaji Haki.

“Mahakama ya sasa imepiga hatua kubwa katika nyanja ya TEHAMA, mifumo mbalimbali imeanzishwa kwa lengo la kuimarisha huduma za utoaji haki nchini, mifumo hiyo ni pamoja na; Mfumo wa Usimamizi wa Mashauri (JSDSII) unaosaidia kupata taarifa zote za mashauri yanayofunguliwa kila siku, Mfumo wa Maktaba Mtandao (e-library) unaosaidia kupata taarifa na machapisho ya maamuzi ya Mahakama, Mfumo wa TanzLII inayosaidia kuona maamuzi ya mashauri, Mfumo wa TAMS unaowezesha kupata taarifa kamili za Mawakili ili kuepusha udanganyifu na Mfumo wa kielektroniki wa kupokea malalamiko ambao unawawezesha wananchi kutoa mrejesho wa ubora wa huduma za kimahakama na yote hii ni kuongeza uwazi na uwajibikaji.

“Mwaka 2018, ilianzishwa huduma ya Mahakama inayotembea katika Mikoa miwili, Mkoa wa Dar es Salaam na Mwanza ambapo hadi kufikia mwezi Oktoba 2021 jumla ya mashauri 1,611 yalifunguliwa, mashauri 1,537 yalimalizika na mashauri 74 yalikuwa yakiendelea na usikilizaji, matumizi ya mfumo huu umesaidia kupunguza muda wa kusikiliza mashauri kutoka siku 120 hadi siku 30 na kupunguza gharama kwa wananchi,” amefafanua Chuma.

Aidha, ameongeza kuwa, mafanikio mengine ni kuimarishwa kwa huduma za Mahakama na kuhakikisha Wananchi wanapata huduma za Kimahakama za ngazi zote katika jengo moja ( One stop center) ambapo kumekuwa na ofisi za wadau ikiwemo RITA, BENKI, POLISI katika Vituo Jumuishi ambayo inasaidia kupunguza mzigo kwa mwananchi kutembea umbali mrefu kuifuata huduma ya HAKI.

“Takwimu za Mashauri ya Mirathi, Ndoa na Talaka katika Kituo Jumuishi cha Utoaji haki cha Temeke ni kama ifuatavyo; Mahakama Kuu ina jumla ya Mashauri 97 (Mirathi 79 na Ndoa na Talaka 18) ambapo kati ya hayo yasiyosikilizwa ni Mashauri 15 ( Mirathi 8 na Ndoa na Talaka 7), Mahakama ya Wilaya ina jumla ya Mashauri 367 (Mirathi 161 na Ndoa na Talaka 206) ambapo kati ya hayo yasiyosikilizwa ni Mashauri 59 ( Mirathi 51 na Ndoa na Talaka 8) na Mahakama ya Mwanzo ina jumla ya Mashauri 1,041 (Mirathi 720 na Ndoa na Talaka 321) ambapo kati ya hayo yasiyosikilizwa ni Mashauri 126 ( Mirathi 115 na Ndoa na Talaka 11),”amefafanua Chuma.

Mbali na hayo, Chuma amesema kuwa matarajio ya Mahakama ni kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa miaka Mitano ( 2020/21 -2024/25) unaoambatana na Programu ya Maboresho hususan Mpango wa huduma ya utoaji haki inayowalenga wananchi yaani Citizen Centric Justice Service Delivery.

Pia kuhakikisha Mahakama inafikia malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na mipango mingine ya Umoja wa Mataifa ili kusogeza huduma karibu na mwananchi na kuboresha mazingira ya kazi na Miundo mbinu ya Mahakama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles