29.2 C
Dar es Salaam
Friday, May 3, 2024

Contact us: [email protected]

Lugalo yakimbiza NBC Tanzania Open 2021

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

KLABU ya gofu ya Lugalo imefanya vizuri katika mashindano ya gofu ya NBC Tanzania Open 2021 baada ya wachezaji wao kuibuka washindi kwenye vipengele mbalimbali, huku ikitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Katika michuano hiyo iliyomaliza jana, mchezaji chipukizi wa  Lugalo, Isihaka Daudi ameibuka kidedea kwa kutwaa ubingwa wa jumla, akizima ufalme wa nahodha wa timu ya Taifa, Victor Joseph wa  Dar Gymkhana ambaye ameshika nafasi ya pili.

Isihaka amepata ushindi huo kwa kupiga mikwaju 272, wakati Victor wa amepiga mikwaju 298, huku mshindi wa tatu naye kutoka Lugalo Richard Massawe akipiga mikwaju 316 kwa mashimo 72.

Mshindi wa pili wa NBC Tanzania Open 2021, Victor Joseph akikabidhiwa kombe na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Abdallah Possi, kushoto ni Mwenyekiti wa TGU, Chriss Martin, wengine ni Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Michael Mstaafu Michael Luwongo na Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara ndogondogo wa benki ya NBC.

Mashindano hayo yamefanyika kwa siku tatu na kumalizika jana Desemba 5, 2021 yakishirikisha klabu za Tanzania kwenye viwanja Gofu Lugalo, Dar es Salaam.

Katika ‘division A’ mshindi wa kwanza ni Baraka Samweli kwa mikwaju 286, akifuatiwa na Zakaria Edward mikwaju 289, namba tatu ni Nicholas Chitanda alipiga mikwaju 292, wote wa Lugalo.

Kwa upande wa watoto (Juniors) waliocheza viwanja 36, mshindi wa kwanza ni K Angelo kwa mikwaju 132, wa pili Ibrahimu Juma mikwaju 134,  huku  mshindi pekee wa ‘gross’ akiwa ni  Rahimu Ally mikwaju 324 wote wa Lugalo.

Wachezaji wa kulipwa kwa mashimo 72, namba moja ni Frank Mwinuka(Lugalo) alipiga mikwaju  mikwaju 294, wa  pili Hassan Kadio (Dar Gymkhana) mikwaju 300,  wa tatu Bryson Nyenza (Lugalo) mikwaju 302, wa nne ni Nuru Mollel (Arusha) mikwaju 308 wa tano ni Isack Wanyeche (Kili Gofu) aliyepiga mikwaju 309.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Abdallah Possi, akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo jana Desemba 5,2021 kwenye viwanja vya Gofu Lugalo.

Kwa wachezaji wazee (senior men) namba moja ni A Kiarie mikwaju 155, akifuatiwa na  Alfred Kinswaga wa Dar Gymkhana mikwaju 162.

Kwa upande wa wanawake katika mikwaju ya jumla (net), mshindi wa kwanza kwa mikwaju 144 ni Joyce Odira (Lugalo), wa pili  Rehema Athumani (Dar Gymkhana) mikwaju 148, huku gross mshindi  akiwa mmoja, Angel Eaton(Lugalo) mikwaju 163.

Akizungumzia ubingwa huo,Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Lugalo, Brigedia Jenerali Michael Mstaafu Michael Luwongo, amesema ubingwa wa Isihaka ni heshima kubwa kwao kwa sababu ni mafanikio ya mradi wa watoto.

Mshindi wa kwanza wa Juniors, K Angelo akipokea zawadi kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa TGU, Kanali David Luoga(kushoto) na Meneja wa Klabu Lugalo, Luteni Kanali Frank Kaluwa.

“Mshindi aliyeshinda leo(jana) kwenye kombe hili kubwa la NBC Tanzania Open 2021, ni kijana  aliyekulia hapa na kujifunzia gofu hapa na leo hii tunamuona jinsi alivyoburuza watu, kwangu mimi amenipa heshima kubwa sana, nitakaa na kamati yangu ya klabu  ili tumtafutie zawadi ya ziada.

“Hiyo ni zawadi ya kutupa heshima sisi Wanalugalo Golf Club, kwa hiyo ndugu yangu Isihaka Daudi leo nakupa wadhifa wa uheshimiwa  katika klabu hii kwa sababu  hili kombe ndiyo mara ya kwanza lipo hapa,” ameeleza.

Naye mgeni rasmi wakati wa kufunga mashindano hayo, akizungumza katika hafla ya kutoa zawadi kwa washindi jana usiku, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Abdallah Possi, amesema amevutiwa na mchezo huo, huku akiahidi kuanza kucheza.

Mshindi kwa wachezaji wa kulipwa, Frank Mwinuka akiwa amesimama na hundi aliyopewa kama zawadi.

Aidha Dk. Possi ameipongeza klabu ya Lugalo kutokana na mtindo inaotumia kuendeleza mchezo wa gofu hasa kuibua vipaji vya watoto.

Pia ameipongeza benki ya NBC kwa mapinduzi iliyoyafanya katika michezo hadi kufikia kudhamini mashindano ya gofu, pamoja na kuwa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

“Michezo ni uwekezaji naomba muendelee hivi hivi, mmefanya mapinduzi makubwa, pia nimefarijika kuona kundi kubwa la watoto wanaocheza gofu na hata bingwa wa mwaka huu nimembiwa ameanzia  Juniors.

Katibu Mkuu wa TGU, Boniface Nyiti akimkabidhi zawadi mshindi wa gross, Angel Eaton kwa wanawake

“Pia niwapongeze TGU (Chama cha Gofu Tanzania), na vyama vyote kwa kuendeleza mchezo huu, Serikali tunathamini sana mchezo wenu na ningeomba tukutane hivi karibun ili tupange mikakati,” amesema Dk. Possi.

Amesema Serikali ipo tayari kuwatafutia TGU, eneo la kujenga kiwanja cha gofu na kuutaka uongozi wa chama hicho kuwasilisha maombi haraka.

Naye Mwenyekiti wa TGU, Chriss Martin, ameiomba Serikali kudhamini timu ya Taifa ya mchezo huo ili kufanya vizuri katika mashindano ya Kimataifa.

Nuru Mollel wa Arusha Gymkhana akiwa ameshika hundi ya sh laki nane baada ya kukabidhiwa kama zawadi ya mshindi wa nne kwa wachezaji wa kulipwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara ndogondogo wa benki ya NBC ambao ndiyo wadhamini wa michuano hiyo, Elibariki Masuke, amesema wamefurahi jinsi mashindano yalivyoendeshwa na kuwafanya wavitiwe kuendelea kudhamini mchezo huo.

“Ni mara yetu ya kwanza kudhamini gofu, kwa kweli, mashindano yamekuwa mazuri sana, yamekutanisha wachezaji wengi tunaahidi kuendelea kudhamini gofu,” amesema Masuke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles