27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Seif azidi kuitesa CCM Zanzibar

maalim-seifNa Is-haka Omar, Zanzibar

SIKU chache baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, kuelezea rafu zilizofanywa wakati wa uandikishaji wapiga kura, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimemtaka kufuta ndoto za kuwa rais na badala yake ama ajipange kufanya biashara au shughuli nyingine za kumwingizia kipato.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Kwa Mabata Magogoni, Wilaya ya Magharibi Unguja, jana uliotaka kuvurugika kutokana na mawe kuanza kurushwa na wanaosadikiwa ni wafuasi wa CUF, kabla ya Jeshi la Polisi kutuliza hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kutokana na historia ya usaliti aliyokuwa nayo Seif katika visiwa vya Zanzibar, hawezi kuwa rais na afute ndoto hizo kwa kuacha siasa na afanye biashara.

Alisema CCM haiwezi kufanya dhambi ya kuitoa Ikulu ya Zanzibar kwa mtu mwenye sera na misimamo ya ubaguzi dhidi ya ndugu zake wa damu na anayekesha akihubiri utengano badala ya ushirikiano.
“CCM tumemshinda Seif kwa awamu nne na mara hii bado anajipa matumaini kwa kung’ang’ania kugombea, basi tunamwambia kabisa kuwa kipigo cha mara hii haji tena juu kisiasa.

“Nampa ushauri wa bure kwamba sera na misimamo yake haina maslahi wala tija kwa Wazanzibari, ndiyo maana hawamkubali, hivyo akatafute biashara mapema afanye lakini siyo siasa,” alisema Vuai.

Alisema Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, ni kiongozi aliyejaa tamaa na uroho wa madaraka, hivyo kwa dalili hizo hafai kuwa rais na anaweza kuisaliti nchi kwa maslahi yake binafsi.

Alimwambia ana kawaida kila ukikaribia Uchaguzi Mkuu anatengeneza mipango ya kuanzisha vurugu za kuharibu uchaguzi kwa makusudi, ili ionekane ameonewa mbele ya taasisi za kimataifa, jambo ambalo halijengi demokrasia ya ushindani wa kisiasa.

“Visiwa vya Zanzibar havitoki mikononi mwa CCM na tumejipanga hata majimbo yote tuliyowaazima CUF tunayarudisha kwetu, kwa kuwa tumekupeni uhuru mmeshindwa kuutumia vizuri.
“Ushindi wa chama hicho unatokana na wingi wa kura katika visanduku na wala si wingi wa mashabiki,” alisema Vuai.

Akizungumzia historia ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), alisema imetokana na busara za CCM kwa kuamini kuwa mfumo huo ilikuwa ni njia pekee ya kumaliza uhasama na chuki za kisiasa Zanzibar, lakini imekuwa tofauti na matarajio ya wengi kwa kuwa viongozi wengi wa CUF wameisaliti serikali hiyo.

Alisema baada ya viongozi wa CCM kutathimini mwenendo wa SUK, wamebaini CUF hawakuwa na nia ya kujenga umoja, bali walikuwa na dhamira ya kutengeneza ngazi ya kuwafikisha katika malengo yao kuipora CCM madaraka, jambo lililowashinda hadi sasa.

Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye pia ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, aliwataka Wazanzibari kuepuka kubebeshwa historia mbovu zinazoashiria uvunjifu wa amani.

Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, alisema kitendo cha Wazanzibari kutoiunga mkono ni sawa na mtu kuyasaliti maisha yake na vizazi vijavyo.
“Lazima wananchi mjue kwamba katiba inayopendekezwa si mali ya CCM, CUF, Chadema, ADC wala TLP, bali ni Katiba ya wananchi wote, hivyo ni muhimu kufanya uamuzi utakaofaidisha vizazi vyenu na vijavyo,” alisema Kificho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles