29.3 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Nkurunziza: Nitapambana

pierreNa Waandishi Wetu, Bujumbura na Dar

RAIS Pierre Nkurunziza wa Burundi ameonya kuwa atalipa kisasi kwa yeyote atakayefanya mashambulizi nchini kwake.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa siasa za Burundi wanasema kauli hiyo inailenga nchi ya Rwanda, kwa kuwa Nkurunziza amesema vita yoyote itapiganwa upande wa pili wa mpaka.

Nkurunziza jana amepokelewa kwa shangwe alipowasili Bujumbura, ambao ni mji mkuu wa nchi hiyo akitokea nyumbani kwao mkoani Ngozi, huku akiendeshwa katika gari lililo wazi upande wa juu na raia walimlaki kwa shangwe na vigelegele.

Kupokelewa kwa Nkurunziza kumemaliza utata wa jaribio la mapinduzi lililotangazwa hivi karibuni na Jenerali Godefroid Niyombare.

Kupitia neno la mwisho la tamko lake lililopo katika tovuti yake jana, alisema amefurahi jinsi Warundi wenzake walivyompokea.
“Watu hawaruhusiwi kuchochea moto,” alisema Nkurunziza.

Shirika la Haki za Binadamu limeonya kuhusu ulipaji kisasi dhidi ya waliojaribu kufanya mapinduzi nchini humo.

Msemaji wa Shirika hilo, Rupert Coleville, jana alisema liko makini na kuendeleza kilichotokea siku mbili zilizopita.
Redio zote binafsi zimefungwa, huku ya taifa pamoja na zile za dini zikiwa hewani.

Nkurunziza aliwasili Ikulu ya nchi hiyo akiwa na msafara mrefu wa magari, huku njiani akilakiwa na wafuasi wake waliokuwa wakicheza na kushangilia.
Hata hivyo, bado kuna utata iwapo hali ya nchi hiyo itarejea kama kawaida.

Picha kutoka vyanzo mbalimbali vya habari zimewaonyesha wafuasi wake waliovalia sare na bendera za Taifa hilo wakiandamana kwa shangwe kumpokea.
Mapinduzi hayo yalitangazwa na Jenerali Niyombare Mei 13, mwaka huu, wakati Nkurunziza akiwa katika mkutano wa viongozi wa Afrika Mashariki uliofanyika Dar es Salaam.
Baada ya mkutano huo, ilielezwa kuwa Nkurunziza alirejea nchini kwake, lakini ndege yake haikuweza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bujumbura na kwenda kusikojulikana.
Hata hivyo, vyanzo vya habari vilisema Rais huyo alijificha nchini Tanzania na alichukuliwa na helikopta kutoka Ngara mkoani Kagera na kuelekea Mkoa wa Ngozi, nchini Burundi.
Hata hivyo, taarifa za Rais huyo kubebwa na helikopta zimekanushwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alipozungumza na MTANZANIA Jumamosi.

“Ninachokueleza ni kwamba Rais Nkurunziza aliondoka siku ile ile baada ya kutolewa taarifa za kupinduliwa, ninachofahamu aliondoka na ndege yake kurudi nchini mwao na kwa sababu ya matokeo ya nchini mwao hakuweza kuhudhuria mkutano uliokuwa ukiendelea,” alisema Rweyemamu.
Alisema taarifa zinazoendelea kwamba alitumia usafiri wa helikopta hawezi kuzizungumzia.
“Andika kwamba Salva amesema, Nkurunziza aliondoka kwa ndege yake siku ile ile, hayo mengine kwamba ameondoka sijui na helikopta, amelala wapi, amelala na nani siyo ya kwetu, hizo habari nyingine achana nazo,” alisema Rweyemamu.
Wakati jaribio la mapinduzi likikwama, majenerali watatu wa Jeshi la Burundi waliojaribu kuipindua Serikali ya Nkurunziza wamekamatwa.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limemkariri msemaji wa Nkurunziza, Gervais Abayeho, akisema ingawa wanajeshi hao walikamatwa, lakini kiongozi wao, Jenerali Niyombare bado yuko mafichoni.
Alisema miongoni wa waliokamatwa, yumo Waziri wa zamani wa Ulinzi, Jenerali Cyrille Ndayirukiye.
“Kama itajulikana wapo miongoni mwa viongozi wa mapinduzi watalazimika kukutana na mkondo wa haki,” alisema Abayeho.

Naye Waziri wa Usalama, Gabriel Nizigama, alisema makamishina wawili wa polisi na maofisa kadhaa wamekamatwa baada ya mapigano katika nyumba moja ya jenerali walikokuwa wamejificha.
Mapema, Jenerali Niyombare aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kuwa yeye pamoja na wenzake wanakwenda kujisalimisha na kuongeza kuwa:
“Natumaini hawatatuua”.
Akizungumzia mapambano dhidi ya wanajeshi waasi, Mkuu wa Jeshi, Jenerali Prime Niyongabo, alisema idadi ya askari wanaounga mkono mapinduzi imeshindwa.
“Jumatano jioni tuliongea na kuwapa nafasi ya kurudi jeshini kuepuka umwagaji damu. Lakini walijaribu kushambulia vituo vya redio jana na jeshi lilijibu shambulizi.
“Tumeboresha mipango yote nchini. Burundi ni nchi ya kidemokrasia. Jeshi haliingilii siasa. Tuna wajibu wa kufuata Katiba.”
Tayari askari watano wameuawa Alhamisi wiki hii katika mapambano hayo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Bujumbura.
Nizigama alikanusha taarifa kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakipigwa wakati wa kukamatwa kwao na walikamatwa kwa njia ya kawaida ya haki za binadamu.
Alisema viongozi wa mapinduzi na wasaidizi wao wanapaswa kuliambia taifa hilo kwamba mapinduzi yalishindwa na kuomba msamaha kwa matendo yao.

UCHAGUZI PALEPALE
Katika ujumbe wake kupitia Mtandao wa Twitter, Nkurunziza alisema: “Nalishukuru Jeshi na Polisi kwa uzalendo. Zaidi ya yote nawashukuru Waburundi kwa uvumilivu.”
Pia Msemaji wake alikiri uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa.

Lakini kiongozi wa kundi la kiraia, Gordien Niyungeko, linalopinga hatua ya Nkurunziza kuwania muhula wa tatu amewataka raia nchini humo kuendelea na maandamano.
Niyungeko aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa maandamano yao hayahusiani na jaribio la mapinduzi.
WAKIMBIZI WAONGEZEKA
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limetoa idadi mpya ya wakimbizi katika mabano kuwa hadi jana wakimbizi katika nchi zilizokaribu na Burundi walikuwa Tanzania (70,187), Rwanda (26,300) na Kongo (9,183).
Habari hii imeandikwa na Agatha Charles na Elizabeth Mjatta

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles