Na Elizabeth Joachim
Makumbusho ya Taifa na Nyumba ya Utamaduni imeanzisha mradi wa mapambano dhidi ya mimba za utotoni utakaokuwa ukitumia sanaa.
Mradi huo unalengo la kutoa elimu kwa watoto walio chini ya miaka 18 ukilenga wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waepukane na mimba za utotoni.
Msemaji wa mradi huo, Sixmund Begashe amesema mradi huo uliozinduliwa Septemba 28 utafanyika katika mikoa mitatu ukiwemo Dar es Salaam, Tabora na Shinyanga.
Begashe amesema Oktoba 11-21 mradi huo ulifanyika katika mkoa wa Shinyanga na Novemba 11-20 Mwaka huu utamalizia katika mkoa wa Tabora.
“Sisi kama Makumbusho ya Taifa tumeona ipo haja ya kuelimisha jamii juu ya changamoto hizi ili kuwaepusha watoto wadogo na janga hili la mimba kwa sababu jitihada zinazofanywa na Serikali kuipeleka nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025 ili jitihada hizo zisije zikakosa viongozi watakaoendeleza hayo mazuri”amesema Begashe.
”Kulingana na takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) mwaka 2017, Tanzania ni nchi ya Tatu kwa nchi za Afrika Mashariki kwa kuwa na viwango vya juu vya mimba na ndoa za utotoni baada ya Sudani Kusini na Uganda,” amefafanua.