28.4 C
Dar es Salaam
Thursday, February 22, 2024

Contact us: [email protected]

SAMPULI MKOJO WA MANJI YAZUA MVUTANO

 

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

SAMPULI ya mkojo wa mfanyabiashara Yusufali Manji, imeibua utata baada ya wakili wake kudai mahakamani kuwa unaweza kuwa wa askari polisi.

Wakili huyo, Hudson Ndusyepo alisema mkojo huo si wa Manji kwa sababu mkemia aliyechunguza hakuingia chumba maalumu wakati sampuli hiyo ikichukuliwa.

Ndusyepo alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya shahidi wa tatu katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili mfanyabiashara huyo, mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dominician Dominic kuieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu matokeo ya uchunguzi wa mkojo wa Manji, kuwa yalionesha alikutwa na kemikali aina ya benzodiazepines na morphine.

Akitoa ushahidi wake, mkemia huyo alidai kuwa chembechembe zilizokutwa katika mkojo wa mfanyabiashara huyo, zinaweza kupatikana kwa mtu aliyetumia dawa za kutuliza maumivu makali ama dawa za kupata usingizi, kwamba inategemea maelekezo ya daktari.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis, shahidi huyo alidai kuwa alifanya uchunguzi wa sampuli ya mkojo wa Manji Februari 9, mwaka huu.

Swali: Februari 9, 2017 saa tano asubuhi kuna kitu chochote ulifanya?

Jibu: Nikiwa natimiza wajibu wangu wa kupima sampuli mbalimbali, walikuja askari na watuhumiwa kutoa sampuli ili tupime kama kulikuwa na chembechembe za dawa za kulevya.

Swali: Unakumbuka majina ya hao watuhumiwa?

Jibu: Walikuwa watuhumiwa wengi, lakini nawakumbuka Mchungaji Josephat Gwajima na Yusufali Manji, wengine siwezi kuwakumbuka.

Swali: Nani alimleta mtuhumiwa kupima?

Jibu: Koplo Sospether ndiye alimleta Manji, nilimpa askari kasha la plastiki ambalo nilibandika namba ya maabara 367/2017.

Swali: Sampuli hiyo iliwasilishwa na fomu namba ngapi?

Jibu: Iliwasilishwa na fomu namba 001.

Swali: Baada ya kupokea sampuli ya mkojo wa Manji ulifanyaje?

Jibu: Nilifanya uchunguzi wa awali kwa kutumia kifaa kiitwacho Biaquik mult panel urine test.

Swali: Ulipata matokeo gani?

Jibu: Nilikuta kuna chembechembe za Benzodiazepine, chembechembe hizi zinaweza kuonekana kwa mtu anayetumia dawa za maumivu ama kutia usingizi kama hapati usingizi, inategemea na maelekezo ya daktari.

Swali: Katika uchunguzi wa pili ulitumia nini?

Jibu: Nilitumia mashine iitwayo HPLC.

Swali: Ulipata majibu gani?

Jibu: Ili kupata majibu tunachukua sampuli linganishi, sampuli ya mkojo nilikuta ina morphine, morphine inaweza kupatikana kutokana na matumizi ya heroin, dawa za kumaliza maumivu makali ama dawa za usingizi.

Hata hivyo, aliongeza kwamba heroin ikitumika ndani ya dakika 60 ukipima haiwezi kuonekana kwani inakuwa kitu kingine.

Alipomaliza kutoa ushahidi huo, alihojiwa na Wakili Ndusyepo kulingana na ushahidi aliotoa.

Wakili: Shahidi unaweza kufanya uchunguzi wa sampuli ya mtuhumiwa bila Mkemia Mkuu kujua?

Jibu: Hapana.

Wakili: Barua ya Mkemia Mkuu ya Aprili 12, mwaka huu ilijibu kuwa Manji hakufikishwa kwa mkemia.

Jibu: Kule ilikuwa Yusuf Alli Manji na hiyo Yusufali Manji.

Wakili: Tuiachie mahakama itaamua… Benzodiazepine umesema zinatolewa na madaktari kwa wagonjwa wao kwa kutuliza maumivu. Je, zinakatazwa?

Jibu: Hazijakatazwa ila zinadhibitiwa.

Wakili: Ni kweli Benzodiazepine ziko katika kundi la dawa za kulevya?

Jibu: Hapana.

Wakili: Katika uchunguzi wa pili, viashiria ulivyovikuta ni matibabu gani yanasababisha kupewa dawa zinazoweza kutoa matokeo kama hayo?

Jibu: Mtu mwenye maumivu makali hupewa morphine kusaidia kupunguza maumivu, lakini daktari anaweza kufafanua zaidi.

Wakili: Unaweza kujua dawa gani ambazo ndani yake hupelekea morphine?

Jibu: Dawa za kupunguza maumivu.

Wakili: Uwepo wa morphine yenye matokeo ya heroin katika mkojo inaweza kuwa si kwa kutumia dawa za kulevya?

Jibu: Inakuwepo heroin, lakini huwezi kujua alitumia kwa matibabu au kwa dawa ya kulevya.

Wakili: Ulikuwapo katika chumba maalumu wakati sampuli ya mkojo ikichukuliwa?

Jibu: Sikuwepo, niliandaa mazingira ya askari kuchukua, mimi nilibakia nasubiri nje. Nilipokea sampuli kutoka kwa askari.

Wakili: Unajuaje kama sampuli ya mkojo ilikuwa ya askari au Manji?

Jibu: Sampuli niliyopokea ilikuwa ya Manji.

Baada ya maswali hayo, Wakili Vitalis aliifahamisha mahakama kwamba Jamhuri wamefunga ushahidi kwa mashahidi hao watatu.

Hakimu Mkeha alisema atatoa uamuzi kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu ama la kesho.

Awali Jamhuri walidai mahakamani kwamba wangekuwa na mashahidi wasiozidi 10 katika kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin.

Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Februari 16, 2017 ambapo anadaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9, 2017 katika eneo la Upanga Sea View Ilala alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles