21.4 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

POLISI WAPEKUA NYUMBANI KWA LISSU KWA SAA 5

PATRICIA KIMELEMETA NA LEONARD MANG’OH

-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanya upekuzi nyumbani kwa Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa saa 5, baada ya kumshikilia tangu juzi.

Lissu, alikamatwa juzi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati alipokuwa akitoka kwenye kesi ya mwanachama wa chama hicho, Yericko Nyerere, ambayo ni wakili.

Baada ya kukamatwa, alifikishwa Kituo Kikuu cha Kati, Dar es Salaam na kuandikiwa makosa mawili ambayo ni kumkashifu Rais Dk. John Magufuli na uchochezi kuhusu kushikiliwa ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 nchini Canada.

Kutokana na hali hiyo, polisi walikwenda nyumbani kwa Lissu jana asubuhi kufanya upekuzi na walipomaliza walimrudisha kituoni saa 7:53 mchana.

MKONDYA

Alipotafutwa Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar as Salaam, Lucas Mkondya ili kuzungumzia suala hilo, alithibitisha kuendelea kumshikilia Lissu.

Alisema hadi jana, walikuwa wanaendelea na upelelezi kuhusu makosa yanayomkabili.

“Tunamshikilia Lissu tangu juzi. Baada ya kumkamata, askari walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi, walipomaliza wamemrudisha kituoni,” alisema Mkondya.

Alisema anashangazwa na kitendo cha waandishi kufuatilia suala moja la Lissu wakati kuna matatizo mengi kwa wananchi, lakini hayaripotiwi.

“Laiti muda mnaotumia kufuatilia suala la Lissu mngekuwa mnafuatilia matatizo ya jamii, tungejua mambo mengi ambayo tungeweza kuyashughulikia kuliko kuhangaika na suala moja la Lissu,” alisema.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alisema polisi walienda nyumbani kwa Lissu kwa upekuzi na walipomaliza walimrudisha Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa taratibu nyingine za kisheria.

Alisema kutokana na hali hiyo wanasubiri kama kiongozi huyo atapewa dhamana au la kwa sababu sheria iko wazi kuhusu hilo.

Agosti 20, mwaka huu, Lissu alisema ndege ya tatu aina ya Bombardier Q 400 iliyotarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa Juni, mwaka huu, imekamatwa nchini Canada kwa amri ya mahakama kutokana na deni la Dola za Marekani milioni 38.7 (Sh bilioni 87) ambazo Serikali inadawa na mkandarasi iliyemvunjia mkataba wake wa ujenzi mwaka 2009.

Alisema amri hiyo ilitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC), baada ya mkandarasi huyo, Stirling Civil Engineers Ltd kufungua shauri akiishtaki Serikali ya Tanzania kwa kuvunja mkataba wake wa ujenzi wa barabara kutoka Wazo Hill hadi Bagamoyo.

Alisema kutokana na hali hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Agustine Mahiga na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Jack Zoka, walikutana na mdeni huyo ambaye alikubali kuachia ndege hiyo endapo yatafanyika malipo ya awali ya Dola milioni 12.5.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles