25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

UINGEREZA YAMWAGA MABILIONI TANZANIA

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

HAKIKA ni neema. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Serikali ya Uingereza kutangaza kutoa msaada wa Dola za Marekani milioni 450 – zaidi ya Sh trilioni moja, kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Msaada huo ulitangazwa jana Ikulu, Dar es Salaam na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa na Masuala ya Afrika kwenye Ofisi ya Mambo ya Nje na Jumuiya ya Madola ya Uingereza, Rory Stewart, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli.

Stewart alisema fedha hizo zitaelekezwa katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, hususani katika kuinua ubora wa elimu na kuongeza idadi ya watoto wanaopata elimu, kuimarisha miundombinu, hasa barabara na bandari, kuinua kilimo cha kibiashara na viwanda kama vile viwanda vya pamba na nyama.

Pamoja na hali hiyo alimpongeza Rais Dk. Magufuli kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa na hatua zilizochukuliwa kuimarisha elimu.

“Nimetembelea shule moja hapa Dar es Salaam jana (juzi), na nimejionea jinsi sera ya kutoa elimu bila malipo ilivyoleta mabadiliko makubwa katika kuongeza idadi ya wanafunzi, nimezungukia shule, nimezungumza na wazazi na nimezungumza na walimu.

“Idadi ya wanafunzi imeongezeka karibu mara mbili, hili ni jambo kubwa sana kutokea kwa muda mfupi na linaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, elimu ni kila kitu,” alisema Stewart.

Alisema kuwa wananchi wa Uingereza wanaipenda Tanzania na Serikali yao itaendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya uhusiano na ana matumaini kuwa msaada ilioutoa utasaidia kuinua uchumi na maisha ya Watanzania.

Kwa upande wake, Rais Magufuli, alimshukuru Waziri Stewart kwa kuja nchini na alimwomba amfikishie shukrani zake kwa Malkia Elizabeth II na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May kwa msaada mkubwa uliotolewa kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Rais Magufuli alisema Uingereza ndiyo nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa nchini na alimuhakikishia Waziri Stewart kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa nchi hiyo katika maendeleo nchini.

Kutokana na msaada huo, Rais Magufuli ametaka Watanzania waelewe kuwa hatua zinazochukuliwa na Serikali dhidi ya rushwa zina manufaa makubwa kwa nchi  na kwamba fedha zilizotolewa na Uingereza zitasimamiwa vizuri.

“Na ndiyo maana tunawaomba Watanzania waendelee kutuunga mkono katika mapambano dhidi ya rushwa, rushwa ni ugonjwa mbaya sana, tukijisafisha katika rushwa nchi yetu itakwenda mbele.

“Katika juhudi tunazofanya wapo wengine wanalalamika lalamika, lakini matokeo yake ni makubwa na ndiyo maana ndugu zetu Waingereza wanaona.

“Pia nitoe wito kwa Watanzania kulipa kodi, hatuwezi siku zote tukawa tunategemea kodi za kutoka kwa nchi marafiki kama Uingereza, ni lazima tujenge mazingira ya Watanzania kuamini kuwa kulipa kodi ni kitu muhimu katika maendeleo yao,” alisema Rais Magufuli.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Sarah Cooke, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles