Na Jonas Mushi na Tunu Nassor, Dar es Salaam.
LICHA ya kutimiza miaka 51 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, imeelezwa mambo matatu bado hayajatekelezwa ndani ya muungano.
Mambo hayo, ni pamoja na masuala ya kodi, mahusiano ya kifedha na usajili wa vyombo vya moto.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano), Samia Suluhu Hassan alisema pamoja na mafanikio ya Muungano bado mambo hayo hayajapata ufumbuzi wa kudumu kwa kipindi kirefu.
Alisema mambo hayo yapo kwenye sekretarieti inayoshughulikia kero za muungano na yanaendelea kujadiliwa na mwafaka ukifikiwa Serikali itatoa tamko.
“Tumepiga hatua kuatatua migogoro iliyokuwapo baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamuri ya Muungano juu ya kero za Muungano. Tumeafikiana kwenye baadhi ya mambo ambayo tayari yamewekwa kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini bado tunaendelea kujadili kuhusu masuala ya kodi, mahusiano ya kifedha na usajili wa vyombo vya moto,” alisema Suluhu.
Alisema Katiba Inayopendekezwa, imeondoa utata wa baadhi ya mambo ya Muungano na kuyapunguza kutoka 22 hadi 16.
Akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya wafanyabiashara kulipa kodi mara mbili, alisema hakuna mtu anayelipa kodi mara mbili na badala yake wanalipa fedha ambazo ni tofauti ya kodi ya Zanzibar na Tanzania Bara.
“Kinachofanyika ni kwamba Zanzibar tunalipa kodi kwa makadirio ya chini tofauti na bara, kila bidhaa ina kiwango chake ikitoka visiwani kuja bara tunaangalia ulilipa kiasi gani kule na kiasi kinachobaki unakilipa Tanzania bara,” alisema.
Alisema bado sheria za uendeshaji Serikali zinatofautiana kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hivyo kuleta mkanganyiko katika uamuzi.