32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Samia atoa onyo kwa majangili  

ELIYA MBONEA na SHOMARI BINDA- SERENGETI

WANANCHI wanaoishi maeneo jirani na Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba na maeneo yaliyohifadhiwa wametakiwa kukaa mbali na maeneo hayo, kwa sababu filimbi ya ulinzi wa kijeshi imepulizwa.

Onyo hilo lilitolewa jana eneo la Fort Ikoma, Serengeti, mkoani Mara na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alipozindua mfumo wa ulinzi wa Jeshi Usu la Uhifadhi utakaotumiwa na taasisi za uhifadhi. Kuanza kutumika kwa mfumo huo sasa kutatekeleza azma moja ya Serikali ambayo ni kuhakikisha usalama wa maeneo yaliyotengwa kwa uhifadhi wa wanyamapori na misitu.

Taasisi za Serikali zitakazohusika na mfumo wa jeshi hilo ni Shirika la Hifadhi za Wanyamapori (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa).

Akizungumza katika uzinduzi huo, alisema Serikali inapoingia katika mfumo mpya wa kusimamia maeneo yaliyotengwa ya wanyamapori na misitu ni matarajio yao kwamba ujangili utakwisha kabisa.

Alisema taarifa za kiintelijensia zinaonyesha silaha na risasi zinaingizwa nchini na watu wenye nia mbaya kutoka nchi jirani.

“Jeshi Usu lipo tayari kwa kazi, kipyenga kimepigwa baada ya onyo hili wananchi wasiilaumu Serikali, nawaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuchukua hatua haraka za kuelimisha wananchi,” alisema na kuongeza:

“Wananchi wanaoishi maeneo jirani na hifadhi nawaagiza kuheshimu sheria za nchi, kuacha kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, kuingiza mifugo maeneo yaliyohifadhiwa.”

Pia aliliagiza jeshi hilo kukabiliana na changamoto ya ugaidi ambayo bado haijagusa moja kwa moja sekta hiyo ya utalii, lakini taswira ya nchi ilitiwa doa.

“Jiwekeni tayari kuhakikisha maeneo yetu ya hifadhi hayatumiki kama maficho ya magaidi kwa kuhakikisha kunakuwa na usalama wa hali ya juu katika malango wanayoingilia wageni.

“Katika sehemu wanazolala na hata zile wanazofanyia utalii ndani ya hifadhi zetu kwa lengo la kuwalinda watalii wasidhurike na vitendo vya kigaidi,” alisema.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa usalama katika hifadhi hizo, Serikali iliona ulazima wa kutengeneza Bodi za Taasisi za Uhifadhi zenye sura ya kijeshi, ukianzia Bodi ya Tawa, Tanapa na wanajeshi miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya NCA.

“Hii ni kuonyesha Serikali imejizatiti kuhakikisha ujangili wa wanyamapori unakwisha na si kupungua tu na maeneo yanayohifadhiwa hayatumiki kama maficho ya magaidi na waharibifu wa mazingira,” alisema Mama Samia.

Alizitaja baadhi ya faida zinazotarajiwa na Serikali kutokana na kuanzishwa mfumo huo ni kuimarika kwa nidhamu, ukakamavu, uadilifu miongoni mwa watumishi wa jeshi hilo.

Alisema jambo hilo litaongeza ubora katika utendaji na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za Serikali katika ulinzi wa maliasili zilizopo maeneo yote yaliyotengwa.

Alitaja faida nyingine kuwa ni kuboreka kwa hifadhi, mapori ya akiba na vivutio vya utalii vilivyopo ndani yake na hivyo kuvutia watalii wengi na hata kuongezeka kwa idadi ya siku zao kukaa hifadhini na matokeo yake kuongeza pato la taifa.

Kuhusu uchumi, alisema takribani asilimia 80 au zaidi ya watalii wanaofika nchini hutembelea maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za wanyamapori.

“Hii imefanya utalii kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya kuliingizia taifa fedha za kigeni kwa asilimia 25 na pato la taifa kwa asilimia 17 pamoja na kutoa ajira rasmi na zisizo rasmi.

Kuhusu faida ya kijamii, alisema Tanapa imekuwa ikichangia katika miradi ya maendeleo inayoanzishwa na wananchi wanaioshi katika vijiji pembezoni mwa hifadhi za Taifa.

“Mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 Tanapa ilichangia shilingi bilioni 8.03 katika miradi mbalimbali ya huduma za jamii, ikiwamo elimu, afya, ufugaji usambazaji wa maji na miundombinu.

“Tawa kwa upande wao wamekuwa wakirudisha sehemu ya mapato yatokanayo na wanyama waliowindwa pamoja na utalii wa picha ambapo tangu mwaka 2017/2018 walirudisha shilingi bilioni 13.3,” alisema.

Samia alisema sababu hizo na baadhi ya faida za uhifadhi kwa jamii ndizo zilisababisha kubadili mfumo wa uendeshaji maeneo yaliyotengwa kwa wanyamapori na kubadili mfumo wa uendeshaji maeneo hayo kutoka kuwa kiraia kuwa wa kijeshi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Mazingira, Nape Nnauye, alisema uamuzi huo umeonyesha nia ya dhati ya kulinda uhifadhi itakayokuwa faida kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunaamini oparesheni zitakazofanywa na Jeshi Usu zitazingatia sura ya kibinadamu, Bunge tupo tayari kushirikiana nanyi katika mambo ya kisera na kibajeti,” alisema Nnauye.

Nao wakuu wa Tawa, Tanapa na NCA kwa nyakati tofauti, walisema kukamilika kwa uzinduzi huo kumeashiria kuanza kwa jukumu zito kwa mamlaka hizo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles