Na Mwandishi Maalumu -Washington DC
MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan, ameitaka Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha, ili kutatua changamoto ya utapiamlo na udumavu wa akili kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kwenye nchi masikini na zinazoendelea.
Wito huo aliutoa juzi mjini Washington Marekani, kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, wakati wa mkutano ulioandaliwa na Rais wa Benki ya Dunia, Dk. Jim Kim, ulioshirikisha mawaziri wa Fedha na wadau wengine kutoka nchi zaidi ya 180 wanaoshiriki mkutano wa mwaka wa Benki hiyo na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Alisema licha ya Tanzania kufanikiwa kupunguza utapiamlo na kiwango cha udumavu kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 kutoka asilimia 42 hadi kufikia asilimia 34, bado idadi kubwa ya watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 2.7 wamedumaa akili, huku wengine laki sita wakikabiliwa na utapiamlo mkali.
“Kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali imepanga kutumia kiasi cha dola milioni 115 sawa na zaidi ya Sh bilioni 254 kukabiliana na tatizo hilo katika kipindi cha miaka mitano kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, kuanzia mwaka 2016/2021,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za mataifa masikini na zinazoendelea ili kuwaokoa mamilioni ya watoto wanaokabiliwa na tatizo hilo kwa kuathiri mustakabali wa watoto kielimu na kimaisha.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Dunia, Dk. Jim Kim, alisema asilimia 43 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanaokadiriwa kufikia milioni 250 katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, wamedumaa na kukabiliwa na utapiamlo mkali.
Dk. Kim aliahidi benki hiyo itatenga fedha kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa kwa ufadhili wake na kushirikisha sekta binafsi, ili lengo la kunusuru watoto katika hali hiyo ya utapiamlo na udumavu wa akili liweze kupatiwa ufumbuzi wa haraka.