Nora Damian na Esther Mnyika, Monduli
Rais Samia Suluhu Hassan amesema ukomavu mkubwa wa kisiasa ulioonyeshwa na Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Edward Lowassa ni somo kwa Watanzania wanaotaka kumuenzi.
Akizungumza leo Februari 17,2024 wakati wa mazishi ya kiongozi huyo yaliyofanyika nyumbani kwake Kijiji cha Ngarash Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, amesema kutofautiana mitazamo kunaweza kutokea bila kutikisa misingi ya utaifa.
“Lowassa alichipukia na kulelewa na CCM lakini alipofanya maamuzi ya kuhamia chama kingine aliendelea kunadi sera zake na kuifafanua dhana ya safari ya matumaini bila kumtukana, kumkejeli wala kumzushia mtu uongo.
“Tunapata somo kubwa sana la siasa za kujenga hoja, kuheshimiana, kusameheana na siasa za kuleta maendeleo. Huo ni ukomavu mkubwa wa kisiasa na ni njia nzuri ya kuchukua kama tunataka kumuenzi Lowassa na vitendo vyake.
“Alichotufundisha ni kwamba tunaweza kutofautiana mitazamo, misimamo na sera bila kutukanana, kulumbana wala kutikisa misingi ya utaifa na mshikamano wetu na bado tukaelewana.
“Sifa hii ndiyo iliyomfanya kujulikana kama mtu ambaye aliweza kutunza urafiki wake na wengi, siku zote ni lazima taifa tuliweke mbele zaidi ya itikadi za vyama vyetu,” amesema Rais Samia.
Aidha amesema lowassa alikuwa mlezi aliyelea na kukuza wanasiasa vijana wengi ambao wanaendelea kulitumikia taifa.
“Sifa hii ya ulezi na kuongoza vijana katika maisha yao ya kisiasa ilimjengea umaarufu na mapenzi makubwa miongoni mwa wengi, na ndiyo maana alichosema mdogo wangu Freeman (Mwenyekiti wa Chadema) yale matokeo ya zile kura ni kwa sababu hii.
“Alijenga umaarufu mkubwa sana yeye mwenyewe binafsi lakini pia tungeyasema sisi usingepata la kusema,” amesema Rais Samia.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amesema Lowassa alikuwa na karama ya kuunganisha makundi mbalimbali wakati wote.
“Alikuwa na unyenyekevu mkubwa sana, alileta kasi ya ukuaji wa demokrasia katika nchi yetu, yeyote aliyefanya kazi na mheshimiwa Lowassa aliishia kuwa rafiki yake. Alikuwa hana mipaka ya kikabila wala kiimani, alimfanya kila mtu kuwa rafiki yake,” amesema Mbowe.
Akitoa salamu za Bunge, Spika Dk. Tulia Ackson, amesema kupitia maisha ya Lowassa viongozi wajifunze kutenda matendo mema ili waweze kukimbiliwa na kila mtu.
“Tunajifunza nini kutoka katika maisha ya Edward Lowassa je, sisi ni maua ya namna gani…tunayo nafasi ya kuchanua kama maua yenye kutoa harufu nzuri yanayoweza kukimbiliwa na kila mtu,” amesema Dk. Tulia.
Awali Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa, ambaye aliongoza ibada ya mazishi ameiasa jamii kupatana na kupenda kuwa karibu na Mungu.
“Siku zetu si nyingi huwa tunachanua kama ua lakini vilevile tunakatwa, tuishi maisha mazuri ili nasisi tuweze kumaliza mwendo wetu vizuri, tuwe na jambo la kushuhudiwa na kusemwa vizuri,” amesema Dk. Malasusa.
Mtoto wa Lowassa, Fredrick ameishukuru serikali kwa kuwa karibu na familia kipindi chote baba yao alipokuwa akiumwa.
“Baba alifanyiwa operesheni ndogo yakatokea yaliyotokea, tukatafuta ‘second option’ ikaonekana hakuna haja ya kwenda nje lakini mheshimiwa rais akatoa fedha zake tumuwahishe baba Afrika Kusini wakati mipango ya serikali inaendelea. Tunakushukuru sana mheshimiwa rais umekuwa mama mlezi wa upendo wa familia yetu,” amesema Fredrick.
Lowassa alifariki Februari 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu, ameacha mjane na watoto watano.