MAKAMU wa Rais, Samia Hassan Suluhu ameahidi kuchangia mifuko 200 ya saruji na mabati 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika shule ya sekondari ya Askofu Anthony Mayalla wilayani Kwimba.
Aliahidi mchango huo wakati akiweka jiwe la msingi katika   mabweni ya wasichana katika shule hiyo  kuunga mkono jitihada zinazoonyeshwa na shule hiyo za kuwaokoa watoto wasichana dhidi ya vishawishi mbalimbali vinavyokatisha masomo yao.
“Naahidi kuchangia mifuko ya saruji 200 ambako 100 itatoka ofisi yangu na 100 itatoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa (Mwanza) na mabati 100 lakini pia Mbunge (Richard Ndassa) na wewe uchangie mabati 100,” alisema.
Shule ya Askofu Mayalla inahudumia wasichana ambao walikumbwa na matatizo ya mimba za utotoni na kukosa karo.
Akizungumzia changamoto mbalimbali zinazoikabili shule hiyo, Katibu wa Askofu wa Jimbo Kuu la Mwanza, Moses Mapela, alisema  kubwa   ni upungufu wa vyumba vya madarasa, mabweni, maktaba, ukosefu wa gari la shule, uzio, kompyuta na udhibiti wa nidhamu shuleni hapo.
“Shule yetu ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa na wanafunzi 68 lakini hivi sasa tunao wanafunzi 456 walimu 18 na wafanyakazi 15 na tuna mpango wa kuanzisha kidato cha tano na sita.
“Lengo kuu la shule yetu ni kuwapatia fursa ya kurudi shule na kuendelea na masomo watoto wa kike waliokosa fursa hizo kwa kupewa mimba ama kukosa karo,” alisema.
Ujenzi wa bweni hilo unatarajiwa kukamilika Januari mwakani kama wadau watajitokeza kusaidia na linatarajiwa kugharimu Sh milioni 157 na tayari limeshatumia Sh milioni 27 huku likitegemewa kuchukua wanafunzi wa kike 120 kwa wakati mmoja.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2010 na aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mwanza, Marehemu Anthony Mayalla.
 Kutoka Sengerema,  ANNA RUHASHA anaripoti kuwa  Samia alifungua bweni la wasichana la Chuo cha Utabibu wilayani Sengerema   lenye thamani ya Sh milioni 655 lililojengwa na Kanisa Katoliki.
Samia aliiomba taasisi hiyo kujenga kituo cha afya mkoani Geita  kupunguza mzingo wa wingi wa wagojwa wanaotafuta huduma katika hospitali ya mkoa wa geita na hospitali jirani ya teule ya Wilaya ya Sengerema DDH.
Mkuu wa chuo hicho Dk. Dickson Materu  alisema ujenzi wa bweni hilo ni katika mpango  wa   jimbo wa mwaka 2011/2016 ambako mradi huo utaongeza idadi ya watalaamu wa afya ya msingi hapa nchini na kuboresha utoaji wa huduma ya tiba katika taifa.
Askofu wa Jimbo la Geita, Mhashamu Flavian Mtinda Kassala aliiomba Serikali kuangalia namna ya kuzipatia msamaha wa kodi ili kuhakikisha wanaondokana na changamoto wanazokabiliana nazo katika kuendesha taasisi hiyo ambayo inafanya kazi na serikali.