26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta, Ulimwengu kutua leo

Mbwana Samatta na Thomas UlimwenguNA WINFRIDA NGONYANI, DAR ES SALAAM

WACHEZAJI Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, wanatarajia kutua nchini leo tayari kujiunga na kambi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kwa ajili ya kuivaa Misri katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2017 (Afcon), utakaochezwa Jumamosi wiki hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji hao wanakuja kuiongezea nguvu Stars katika mchezo huo ambao utaamua taifa litakalofuzu kuingia katika fainali za Afcon mwakani kutoka kundi G, ambapo Misri tayari wana pointi saba, wakati Taifa Stars ina pointi moja hivyo kuifanya Stars kuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kuwa inawafunga Misri.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema wachezaji hao wameshaanza safari ya kuja nchini na wanatarajia kuwasili jijini Dar es Salaam mapema leo.

“Pia timu ya Misri inatarajiwa kuwasili nchini kesho (leo), tayari tumeshawasiliana na ubalozi wa Misri nchini ambao umeridhishwa na mapokezi yetu, hivyo timu ikifika tu jijini itaelekea moja kwa moja katika Hoteli ya Kilimanjaro Kempinski,” alisema.

Aidha Lucas alisema mchezo huo utachezeshwa na waamuzi kutoka Gabon na kuwataja kuwa ni pamoja na mwamuzi wa kati Meye Bastrel, akisaidiwa na Vinga Theophile na Mihondou Gauther.

Lucas alisema mara baada ya kuwasili viongozi wa timu ya Misri watakuwa na mkutano maalumu na waandishi wa habari katika ofisi za shirikisho hilo, mkutano utakaowajumuisha makocha wa pande zote mbili kueleza walivyojiandaa dhidi ya mchezo huo.

Stars inavaana na Misri ikiwa na matumaini ya kupata matokeo mazuri baada ya kufanya vizuri katika mchezo wake na Harambee Stars uliofanyika Jumapili katika Uwanja wa Moi Kasarani, Nairobi nchini Kenya ambapo Stars ilitoka sare na timu hiyo.

Katika hatua nyingine, Lucas alisema timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Rwanda mchezo utakaochezwa Juni 17 mwaka huu mjini Kigali.

“Twiga Stars imealikwa mjini Kigali, mchezo utakuwa wa kirafiki ukiwa na lengo la wenyeji wetu kujipima nguvu, kwani wao wanajiandaa na kufuzu fainali za Afrika kwa upande wa Wanawake,” alisema Lucas.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles