MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta amefuzu vipimo vya afya na kusaini mkataba wa kuichezea KRC Genk ya nchini Ubelgiji hadi mwaka 2020.
Meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo, alisema jana kuwa amepewa taarifa kwamba mchezaji huyo amefuzu vipimo na kusaini mkataba huo na mchana wa jana alitambulishwa rasmi.
Alisema hatua hiyo imekuja baada ya mmiliki wa TP Mazembe, Moise Katumbi, kukubaliana na dau ambalo watatoa Genk, hivyo ametoa baraka za mchezaji kusaini mkataba wa miaka minne.
“Samatta ameshasaini mkataba wa miaka minne hapa tayari, sasa ni mchezaji wa Genk na atajiunga na timu mara moja,” alisema Kisongo.
Alisema Samatta alitambulishwa jana katika mazoezi ya timu hiyo ikijiandaa na mechi yao ya ligi dhidi ya Kortrijk inayochezwa leo katika Uwanja wa Cristal Arena.
Katumbi amekubali mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania ajiunge na KRC Genk, badala ya Nantes na Marseille za Ufaransa zilizokuwa zinamwania pia.
Samatta na Genk wanataka kukimbizana na muda ili kuwahi kabla ya dirisha dogo la usajili halijafungwa, angalau mapema Februari aanze kucheza Ubelgiji.