25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Simba kazini, Yanga kuipoteza Azam

Simba-vs-Yanga-2MSHAMU NGOJWIKE, DAR ES SALAAM NA OSCAR ASSENGA, TANGA

TIMU ya  Simba leo inashuka dimbani kufungua pazia la mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuikaribisha African Sports ya Tanga katika  Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba, ambayo inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 33, inahitaji kupata matokeo mazuri ili ipunguze wingi wa pointi walizopitwa na vinara wa ligi hiyo, Yanga na Azam, ambao wana pointi 39 kila moja, zikitofuatiana wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba wanaingia katika mchezo huo ikiwa chini ya kocha Jackson Mayanja, ambaye amechukua mikoba ya Dylan Kerr.

Timu hiyo imekuwa na historia nzuri ya kushinda dhidi ya African Sports ambapo katika mzunguko wa kwanza ilichomoza na ushindi wa bao 1-0 katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa ushindi huo wa Simba uliiwezesha timu hiyo kuvunja mwiko wa kutopata matokeo katika uwanja huo, ambapo kwa mara ya mwisho walishinda 1-0 dhidi ya Coastal Union mwaka 2012.

Simba wataingia uwanjani ikiwa na ingizo jipya la wachezaji Daniel Lyanga, Novat Lufungo na Brian Majwega.

Katika mchezo mwingine, Yanga watakuwa ugenini kuikabili Coastal Union katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na huenda ikaanza kuwapoteza mahasimu hao wanaolingana kwa pointi 39, Azam FC.

Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans Van Der Pluijm, ameonekana kuandaa
kombinesheni ambayo itamwezesha kupata ushindi kwenye mechi hiyo dhidi ya Coastal Union.

Hatua hiyo inatokana na kitendo cha kocha huyo kuwapa mazoezi maalumu
wachezaji Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Amisi Tambwe na Oscar Joshua, ambao walipewa nafasi kubwa kwenye mazoezi ya jana katika Uwanja wa Mkwakwani.

Licha ya kombinesheni hiyo, Pluijm alitumia muda mrefu kuzungumza na kiungo wa timu hiyo, Haruna Niyonzima, akijaribu kumpa majukumu mazito ya kuhakikisha anatumia vizuri nafasi atakazozipata ili kupata ushindi.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Pluijm alisema kuwa kwa upande wake  ana asilimia kubwa ya ushindi ili waweze kujihakikishia kukaa kileleni mwa ligi hiyo.

“Kwanza namshukuru Mungu tumefika salama mkoani Tanga, lakini niseme kuwa tulichokifuata ni pointi tatu muhimu na hilo halina ubishi, niwatake wapenzi na mashabiki wa Yanga wajitokeza kwa wingi kuja kuangalia namna timu yao itakavyoifunga Coastal Union,” alisema Pluijm.

Kwa upande wake, Kocha wa Coastal Union, Ally Jangalu, alisema kuwa baada ya kukabidhiwa kikosi cha timu hiyo amekiimarisha kukabiliana na timu yoyote itakayokuja mbele yao, kwani ugonjwa uliokuwa ukiikabili timu hiyo ya ubutu wa kufunga mabao sasa umekwisha.
“Nisema kuwa tangu nikabidhiwe kikosi hiki tumefanya mazoezi mazito na yale ya kati kwa misingi ya kuhakikisha timu inarudisha makali yake ya miaka ya nyuma na hili limeanza kuonekana kwa baadhi ya michezo yetu ya Ligi Kuu na sasa tumeiva,” alisema Jangalu.

Michezo mingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo ni pamoja na JKT Ruvu ambao wataikaribisha Majimaji katika  Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, wakati Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa Stand United Uwanja wa Manungu, Turiani, mkoani Morogoro.

Nayo Mwadui FC ya Shinyanga itapepetana na Toto Africans ya Mwanza katika  Uwanja wa Mwadui Complex,  mkoani Shinyanga, wakati Kagera Sugar itacheza dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Kambarage.

Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mchezo mmoja ambapo Mgambo Shooting itakuwa mwenyeji wa Ndanda FC katika Uwanja wa Mkwakwani, mkoani Tanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles