Na MOHAMED KASSARA
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, ameendelea kuwasha moto, baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-2 ilioupata timu hiyo dhidi ya Royal Antwerp FC.
Samatta alifunga mabao hayo dakika za 76 na 90 na kuisaidia Genk kupata ushindi huo ikiwa ugenini.
Katika mchezo huo, Genk ilitanguliwa baada ya wenyeji wao kupachika mabao mawili, lakini ikasawazisha kabla ya kupata mabao mengine mawili yaliyoifanya iondoke na ushindi.
Ushindi huo uliifanya Genk kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji baada ya kufikisha pointi 33, ilizozipata baada ya kushuka dimbani mara 13, ikishinda michezo 10 na kutoka sare mitatu.
Samatta sasa amefikisha mabao 10 na kuongoza katika chati ya wafungaji, akifuatiwa na mshambuliaji, Ivan Santini wa Anderlecht mwenye mabao tisa.
Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya Taifa Tanzania, Taifa Satrs amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akifunga mabao ambayo yamekuwa yakiiwezesha Genk kupata ushindi.
Makali ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, inasemekana yamezifanya baadhi ya klabu za Englang kumtolea jicho, zikiwemo Everton na West Ham zikitaka kumsajili katika dirisha la majira ya baridi.
Samatta ameifungia Genk mabao 19 msimu huu, mabao 10 akiyapata katika Ligi Kuu ya Ubelgiji, huku mengine tisa akifunga katika michuano ya Europa.
Mshambuliaji huyo alifunga mabao sita katika michezo minne ya kusaka nafasi ya kufuzu michuano ya Europa, kabla ya kuendeleza makali yake kwa kufunga mabao matatu katika michezo mitatu ya hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Pia alithibitisha ubora wake  katika kikosi cha Taifa Stars, baada ya kukiwezesha kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde, matokeo yaliyofufua matumaini ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.
Mchezo huo ulipigwa Oktoba 16 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Samatta alifunga bao moja na kupika jingine lililofungwa na mshambuliaji, Simon Msuva na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L, ikiwa na pointi tano baada ya kucheza michezo minne.
Samatta alijiunga na Genk mwaka 2016, akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) ambayo aliichezea kwa misimu mitano na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, mwaka 2015.
Alitwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka 2015 Â kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani, akiwapiku; Zein Edin Farahat, Roger Assale, Robert Kidiaba, Moudather el Tahir, Mohammed Meftah, Kermit Erasmus, Felipe Ovono, Baghdad Bournedjah na Abdeladim Khadrouf.
Samatta ameichezea Genk mechi 126 katika mashindano yote tangu amejiunga nayo na kuifungia mabao 50.
Katika Ligi Kuu ya Ubelgiji amecheza mechi 98 na kufunga mabao 36, Kombe la Ubelgiji, mechi nane mabao mawili na Europa mechi 20 mabao 14.