NA BEATRICE KAIZA,
MSANII wa muziki wa Bongo fleva, Salim Mohamed ‘Sam wa Ukweli’, amesema sababu zilizomfanya kukaa kimya kwa muda mrefu ni kutokana na kubanwa na mkataba.
Akizungumza na MTANZANIA, alisema baada ya kutoka Emotion Record alijiunga na Al jazeera Entertainment, lakini alishindwa kuwa huru kufanya kazi zake kutokana na kubanwa na mkataba ambao aliusaini.
“Nilitaka kuvunjwa mkataba na lebo ya Al jazeera kutokana na kuona hakuna kazi iliyokuwa inafanyika, hivyo nilitaka kuwa huru lakini ilishindikana na niliambiwa nilipe Sh milioni 100 kama nataka kutoka kwenye lebo hiyo, hali hiyo ilinifanya nikae kimya kwa muda mrefu,” alisema Sam wa Ukweli.
Aliongezea kuwa kwa sasa mkataba umekwisha na yuko huru kufanya kazi na mtu yeyote na anatarajia kuachia ngoma, kwa sasa anatamba na wimbo wake ujulikanao ‘Kisiki’ na kuwaomba mashabiki zake kumpokea kwa moyo mmoja kwa kurejea tena kwenye tasnia ya muziki.