24.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Salma Kikwete azidi kuchanja mbuga Mchinga

Mwandishi Wetu, Lindi

Mgombea Ubunge Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Salma Kikwete, ameendelea kufanya mikutano ya kampeni katika kata na vijiji vya jimbo hilo kwa kuwataka wapiga kura kuchagua mafiga matatu kwa kumchagua Mgombea Urais, Dk. John Magufuli, yeye na madiwani wote wa chama hicho ifikapo Oktoba 28, mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Komolo, Kata ya Matimba jana, Mwalimu Salma ambaye pia ni Mke wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, amesema kero na changamoto zote za jimbo hilo zitashughulikiwa na madiwani, yeye pamoja na Rais Magufuli pindi watakapochaguliwa.

“Hizi kero zote tupeni mimi, Dokta Magufuli na madiwani tuzishughulikie na kwa maendeleo ya Mchinga yetu chagua CCM, chagueni mbunge, Rais na madiwani wote wa CCM pia nawaomba wote jitokezeni kwa wingi siku ya Oktoba 28 ili mkapige kura,” amesema Mwalimu Salma.

Pia amesema visima vilivyopo katika maeneo ya jimbo hilo visivyotoa maji vitafufuliwa au vitachimbwa vipya ili kukomesha tatizo la upatikanaji maji unaowasumbua wana Mchinga.

 “Wote tushirikiane kwa kuleta maendeleo kwa sababu hiyo sio kazi ya mbunge peke yake, ikitokea tunatakiwa kufyatua matofali basi tufyatue na sio ohoo hiyo ulisema mwenyewe mbunge au tuchimbe msingi, ohoo hiyo kazi ya mbunge, sio hivyo lazima tujitolee kuleta maendeleo,” amesema Mwalimu Salma.

Kuhusu afya, alisema atahakikisha Kituo cha Afya cha Rutamba kinaboreshwa na Kitomanga inakuwa ni Hospitali ya Wilaya.

“Jimbo letu la Mchinga lina tarafa nne kwa hiyo kituo cha afya lazima tuhangaike nacho kibadilike na kiwe katika hali nzuri kwa sababu kina hali mbaya, ndani ya jimbo letu hatuna hospitali kwa hiyo lazima tuwe na hospitali hata moja, Kitomanga lazima iwe hospitali na lengo letu tarafa zote zinakuwa na vituo vya afya vya kutosha na zahanati za kutosha,” amesema Mwalimu Salma.

Katika hatua nyingine, amesema ujenzi wa barabara itakayopitika kwa mwaka mzima utafanyika kutoka katika eneo la Kibaoni-Matimba-Nangaru hadi Milola.

Pia amewataka wana Mchinga kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kulima kwa wingi ili kuinua maisha ya familia zao na kuinua uchumi wa jimbo zima kwa ujumla wake na itaundwa timu ya wataalamu itakayofanya kazi kwa ushirikiano katika kilimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles