27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Prof. Juma: Jaji Mmila atakumbukwa kwa utendaji kazi

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, amemwelezea marehemu Jaji Bethuel Mmilla kuwa alikuwa mchapakazi na atakumbukwa kwa utendaji kazi wake wa kujitoa na ushirikiano.

Mwili wa Mmilla, aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, umezikwa jana nyumbani kwake Goba Michungwani, Dar es Salaam baada ya kuagwa katika viwanja vya Karimjee, baadaye kufanyiwa ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mwenge, Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Jaji Mmilla aliyefariki usiku wa Septemba 24, Jaji Mkuu alisema wasifu wa marehemu ni mfano mzuri wa namna alivyowatumikia zaidi walio wengi kuliko alivyojitumikia kwa masilahi yake binafsi au ya familia yake.

“Wasifu wake unaonyesha kuwa kila kituo katika utumishi wake wa Mahakama, amekuwa ni wa kutumikia, anayetoa na asiye wa kutumikiwa,” alisema Jaji Mkuu.

Alisema uamuzi alioutoa utabaki kuwa mfano wa mambo yote aliyoyaamini na kuyatekeleza kwa vitendo.

Jaji Mkuu alisema marehemu atakumbukwa pia kwa ucheshi na utani wake wa mara kwa mara ambao uliwasaidia waheshimiwa majaji wa rufaa kusahau angalau kidogo maswala magumu ya kisheria na kimaamuzi.

Aliwashukuru madaktari na wahudumu wote wa Hospitali ya Jeshi Lugalo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wale wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), wakiongozwa na Profesa Mohamed Janabi kwa kuwa karibu na marehemu.

Akitoa salamu kwa niaba ya majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Augustine Mwari alimwelezea marehemu Jaji Mmilla alikuwa  kiongozi mwenye ushirikiano mkubwa na wenzake na aliyekuwa akiwatia moyo katika kazi mbalimbali za utoaji haki.

Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk. Rugemeleza Nshalla aliwashauri majaji na mahakimu kuandika hukumu zenye mguso chanya katika maisha ya watu na utawala wa sheria.

“Marehemu Jaji Mmilla aliandika hukumu nyingi ambazo zitatumika kama rejea kwa wanafunzi wanaosoma sheria nchini, mahakimu na majaji,” alisema Dk. Nshalla.

Aliwaasa familia ya marehemu kwa kuwashauri kuishi kwa kupendana na kushirikiana ili kuyaenzi mazuri aliyoyafanya marehemu Jaji Mmilla.

Mazishi ya Jaji Mmilla yalihudhuriwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dk. Eliezer Feleshi, majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, wadau mbalimbali na watumishi wa Mahakama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles