LONDON, ENGLAND
UONGOZI wa klabu ya Crystal Palace umedai unaguswa na uwezo wa beki wao, Mamadou Sakho ambaye anakipiga katika kikosi hicho kwa mkopo akitokea Liverpool.
Mchezaji huyo alitolewa kwa mkopo mara baada ya kutuhumiwa kutumia dawa ambazo hazitakiwi michezoni, hivyo Crystal Palace wakamsajili mchezaji huyo kwa mkopo tangu Jaunari 31, mwaka huu.
Kutokana na mchango wake wa kuipigania timu hiyo, uongozi umedai kuwa upo kwenye mipango ya kutaka kumsajili moja kwa moja mchezaji huyo mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Kocha wa klabu hiyo, Sam Allardyce, amedai kuna uwezekano mkubwa wa mchezaji huyo kupewa mkataba wa moja kwa moja kama atakuwa tayari kukaa ndani ya kikosi hicho.
“Kwa kipindi hiki Sakho amekuwa akionesha kiwango cha hali ya huu, ni wazi kwamba amejitengenezea soko katika klabu mbalimbali, lakini ni maamuzi yake kama atakuwa tayari kubaki au kuondoka, lakini klabu ipo kwenye mipango ya kutaka kumsajili moja kwa moja,” alisema Allardyce.