24.1 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

CONTE AWAPIGIA MAGOTI CHELSEA

LONDON, ENGLAND


KOCHA wa klabu ya Chelsea, Antonio Conte, amewapigia magoti wachezaji wake na kuwaomba wapambane katika michezo iliyobaki ya ligi kuu ili kuweza kutwaa ubingwa msimu huu.

Katika msimamo wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea inaongoza ikiwa na pointi 75 baada ya kucheza michezo 32, huku wapinzani wao Tottenham wakiwa na pointi 71, hivyo kocha huyo anaamini ushindani ni mkubwa na chochote kinaweza kutokea kama wachezaji wake watakosa umakini.

Awali Chelsea ilikuwa inaongoza ligi huku ikiwa mbele kwa pointi 10, lakini kutokana na kushindwa kufanya vizuri katika baadhi ya michezo ikimfanya ashuke taratibu, huku Tottenham akizidi kusonga mbele.

Hata hivyo, timu hizo zilishuka dimbani juzi katika mchezo wa Kombe la FA hatua ya nusu fainali, ambapo Chelsea ilionesha ubabe wake na kufanikiwa kushinda mabao 4-2 na kuifanya timu hiyo itangulie fainali.

Kutokana na kiwango ambacho Chelsea walikionesha kwenye mchezo huo, Conte amewataka wachezaji hao kuendelea kufanya hivyo katika michezo iliyobaki ya ligi kuu ili kuweza kutwaa ubingwa msimu huu na kuandika historia mpya.

“Kikubwa ambacho Chelsea wanatakiwa kukifanya katika michezo iliyobaki ni kujituma kama walivyofanya katika mchezo dhidi ya Tottenham hatua ya nusu fainali katika Kombe la FA na kufanikiwa kupata ushindi mkubwa.

“Wachezaji wangu walionesha ushindani wa hali ya juu kwa kuwa mchezo huo ulikuwa muhimu sana kwetu kuweza kuingia hatua ya fainali, furaha ya mashabiki ni kuona tumefika fainali na kutarajia ubingwa wa michuano hiyo.

“Kwa kasi na uwezo ambao wachezaji wameonesha katika mchezo huo wa FA, ni vizuri wakaendelea kufanya hivyo katika michezo mingine ya ligi kuu ili kuendelea na rekodi yetu.

“Wengi wanaangalia jinsi gani tutaweza kutwaa ubingwa msimu huu, ninaamini kama wachezaji wangu wataendelea kuonesha uwezo ule, ni lazima tutachukua ubingwa wa ligi kuu, ushindani ni mkubwa ila wachezaji wangu hawataniangusha,” alisema Conte.

Hata hivyo, kocha huyo amewataka mashabiki kuendelea kuisapoti timu yao katika mchezo wa kesho wa ligi kuu dhidi ya Southampton ili timu hiyo iweze kufanya vizuri.

“Kesho tunashuka dimbani na moja kati ya timu bora sana katika michuano ya ligi kuu, hivyo ni muda wa mashabiki kuendelea kuisapoti timu yao iweze kupata ushindi na kujiweka pazuri katika msimamo,” aliongeza.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,644FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles