22.3 C
Dar es Salaam
Saturday, July 13, 2024

Contact us: [email protected]

Sakata la Dangote kaa la moto

aliko-dangote

Na Waandishi Wetu -DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Kiwanda cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara kuripotiwa kwamba kimesitisha uzalishaji, watu mbalimbali wakiwamo, wanasiasa, wachumi na wachambuzi wameibuka na kuishangaa Serikali namna inavyoshughulikia suala hilo.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu jana, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT -Wazalendo) alisema suala la Dangote halikupaswa kufikia hatua hiyo kwani linatoa picha mbaya kwa wawekezaji waliopo na wanaotarajiwa kuja nchini.

Alisema kama Serikali inataka kuendelea na ajenda yake ya maendeleo ya viwanda ni lazima iboreshe namna yake ya ushirikiana na wawekezaji.

“Ukitazama kwa umakini utaona Dangote anakomeshwa kwa sababu ya hisia kuwa kuna wanasiasa wa awamu ya nne wanaubia naye, mawazo ya husda na chuki ndiyo yanayoongoza uamuzi wa baadhi ya watu serikalini, haifai kabisa, yanayotokea ni sawa na mtu ambaye wakati wa baridi anachoma moto nyumba yake ili aote moto.

“Serikali iache utoto, ishughulike na suala hili ili uzalishaji uendelee, lakini pia isikilize kilio cha wenye viwanda kuhusu gharama za uzalishaji kwa sababu ni kubwa mno, ruzuku kwa wazalishaji ni muhimu ili kuzalisha ajira isibishane kwa sababu ya ubishi, ” alisema Zitto.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk. Dalali Kafumu, amesema anashangazwa na hali tete inayojengeka kati ya Serikali na kiwanda hicho.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Kafumu alisema mvutano huo unaweza kuathiri taswira ya uwekezaji nchini na kuiomba Serikali ikae na mwekezaji huyo ili kumaliza tofauti zao.

Dk. Kafumu ambaye ni Mbunge wa Igunga (CCM) alikuwa akitoa maoni yake binafsi, ambapo ameonekana kuguswa na sakata hilo na kusema kuwa haoni busara za Serikali katika kumaliza mzozo huo zaidi ya ubabe.

Alisema kamati yake haijui chochote kuhusiana na mzozo huo na kueleza kuwa amezungumza na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, akutane na kamati yake ili wabunge watoe ushauri wao kunusuru kiwanda hicho.

“Kwa maoni yangu binafsi, kwa namna tunavyoona kwenye vyombo vya habari, hapa kunatatizo, Dangote ni mwekezaji mkubwa suala hili linahitaji utulivu katika kulishughulikia.

“Inavyoonekana wakati mwekezaji huyu anakuja, kulikuwa na makubaliano na Serikali iliyopita labda masuala ya misamaha, masuala ya kodi, bei nafuu ya gesi na mengine.

“Sasa leo kumwambia tu usitumie makaa ya nje lazima utumie ya ndani, sawa inawezekana lakini mnajuaje kama huyu mtu ana mikataba na huko anakotoa hayo makaa?

“Dangote ni mwekezaji mkubwa, ana viwanda vingine huko duniani akifunga kiwanda chake hasara itakuwa ya kwetu. Serikali hii imejielekeza kwenye uchumi wa viwanda, leo unaposikia msuguano kama huu unapata shida kuelewa inakuwaje?,” alihoji.

Kafumu aliendelea kusema. “Mawaziri wanasema Serikali haipaswi kulaumiwa isipokuwa Dangote mwenyewe, wanasema alipewa kibali cha kuvuta gesi hakuvuta, tujiulize kwanini hakuvuta?

“Mara hakusaini mkataba wa kununua makaa ya mawe, ujiulize kwa nini hakusaini? Serikali ikae na Dangote wazungumze, kwa namna hii ni kama Serikali inafunga urafiki na mwekezaji huyu, jambo ambalo si zuri,” alisema Dk Kafumu.

Waziri Kivuli

Naye Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, Anthony Komu alisema anasikitishwa na mwenendo wa sakata la Dangote, kwani linapaswa kushughulikiwa haraka ili kulinda maslahi mapana ya Taifa.

“Tuna tatizo kubwa juu ya ukweli wa jambo hili kutoka serikalini, kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa, Serikali imekuwa ‘difensive’ mno, nadhani kwa hali hii hatuwezi kwenda kabisa. Siku zote tunaambiwa mambo yanakwenda vizuri sasa iweje tushuhudie  hali hii.

“Kwanza Watanzania wengi watapoteza ajira, unafuu wa upatikanaji wa saruji utapotea kama zamani, ulipaji kodi utashuka, bei ya saruji itapanda mara dufu… haya yote ni mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa kina,”alisema Komu.

Profesa Semboja

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) Profesa Hajji  Semboja alisema katika kipindi hiki ambacho serikali iko kwenye mchakato wa kuanzisha viwanda, wanapaswa kushirikiana na wawekezaji wanaokuja nchini akiwamo Dangote na kuangalia matatizo yanayojitokeza na kuyafanyia kazi.

“Kiwanda hicho ni kikubwa ambacho kimezalisha ajira na saruji ambayo inauzwa kwa gharama nafuu hata mwananchi wa kawaida anaweza, hivyo serikali wanapaswa kukaa pamoja na kuangalia tofauti zilizopo na kuzifanyia kazi.

TPDC

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Mhandisi  Kapuulya Musomba alisema taarifa zilizotolewa na uongozi wa Dangote juzi hazina ukweli wowote.

“Kama TPDC tunapenda kukanusha taarifa zinazoenezwa na Kampuni ya Dangote pamoja na washirika wake kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kudai kuwa tumeshindwa kukiuzia gesi asilia kwa bei rahisi na kwamba ndiyo moja ya sababu ya kusimamisha uzalishaji wake,” alisema.

Alisema TPDC hufuata kanuni na utaratibu wa kupanga bei ya gesi asilia kulingana na aina ya mteja na kwamba wateja wamegawanyika makundi tofauti kama vile wateja wa viwandani, majumbani, magari, pamoja na wazalishaji umeme.

Alisema bei elekezi ambayo inapendekezwa na TPDC ni lazima iridhiwe na ipitishwe na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ndipo ianze kutumika na si mtu binafsi kujipangia bei yake.

Alisema TPDC hufuata kanuni na utaratibu wa kupanga bei ya gesi asilia kulingana na aina ya mteja na kwamba wateja wamegawanyika kufuatia makundi tofauti kama vile wateja wa viwandani , majumbani, magari, pamoja na wauzalishaji umeme.

“Dangote kama mtumiaji wa viwandani amekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na TPDC  kuhusu bei ya gesi asilia , ambapo kiwanda chake kimeomba kupewa gesi  kwa bei ambayo hapa kwetu ni kidogo, kiasi hicho cha bei ndicho kinacholipwa kwenye kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.

Akifafanua zaidi, Kaimu Mkurugenzi huyo wa TPDC alisema Dangote alikuwa anataka auziwe gesi hiyo kwa Dola za Marekani 4.7.5 na baadaye akakataa akitaka ishuke zaidi ingawa bei iliyopo kwa sasa ni Dola za Marekani 5.1.4 kwa kipimo cha energy jambo ambalo alisema halitawezekana.

“Dangonte amekuwa akibadilika badilika ambapo alianza na Dola milioni 2 akaja 4 na hii ya mwisho alitaka iwe hiyo ya Dola za Marekani 4.7.5 na bei hizi zinaitwa Dola chini ya kipimo ambapo kitaalamu inajulikana kama   MMBTU.

Kuhusiana na utumiaji wa makaa ya mawe ambayo yanazalishwa hapa nchini, Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi John Shija alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha viwanda vyote vinavyozalisha saruiji nchini vitumie makaa ya mawe yanayozalishwa na Mgodi wa Ngaka uliopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Lengo la serikali kufanya hivyo ni kulinda mgodi huo ambao unatija kwa Watanzania wote na tayari baadhi ya viwanda vinavyozalisha saruji hapa nchini vimeshaingia mkataba na mgodi huo isipokuwa Dangote.

“Lakini mpaka sasa upande wa kiwanda cha Dangote wako kimya hawajasema chochote kuhusiana na hili, hivyo tutaangalia ni hatua gani zaidi za kuchukua iwapo tutakosa ufumbuzi wa baadhi ya viwanda kutotumia makaa ya mawe yanayozalishwa hapa nchini,” alisema.

Kuhusu ubora wa makaa hayo, alisema kila kiwanda kina aina yake ya matumizi na kusema kuwa mgodi wa Ngaka una maabara ambayo inatumika kupima makaa hayo kwa ubora unaostahili kinyume na inavyoelezwa kuwa hayafai.

Utajiri wa Dangote

Kinara huyo wa utajiri barani Afrika mwenye umri wa miaka 58 anashika nafasi ya 51 duniani akiwa na Dola za Marekani bilioni 15.4 nyuma ya James Simons mwenye utajiri 15.5 bilioni.

Dangote amejipatia ukwasi huo kupitia uwekezaji katika uzalishaji wa saruji, sukari na maua ambapo uwekezaji wake wa hivi karibuni aliufanya katika nchi za Cameroon, Ethiopia, Zambia, nyumbani kwao Nigeria and na hapa Tanzania.

Pia amewekeza katika nchi za Benin, Senegal, Ghana, Afrika Kusini na Togo, huku kampuni yake ikizalisha mara 30 zaidi ya kipimo cha tani za metriki kwa mwaka na akitegemea kuzalisha mara mbili ya hapo ifikapo 2018.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles