28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wafuasi wa CUF waandamana Zanzibar

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam

KUNDI  la vijana lilikusanyika katika ofisi za makao makuu ya Chama cha Wananchi (CUF) zilizopo Mtendeni, Zanzibar na kufunga barabara, wakimtaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad atoe mustakabali wa Zanzibar.

Tukio hilo lilitokea jana ambapo wafuasi hao walifika Mtendeni saa tano asubuhi wakati Maalim Seif akiwa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani wakitoka katika ziara ya kuangalia wagonjwa Wilaya ya Mjini.

Vijana hao walifunga barabara na hakukuwa na shughuli yoyote iliyoweza kuendelea huku wakipaza sauti wakimtaka Maalim Seif ateremke chini wampe ujumbe uliowafanya wafike hapo.

“Tuna maswali yetu tunamhitahi Maalim atujibu, tunakuomba Maalim njoo utusikilize,” zilisikika sauti za vijana hao.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Bimani alisema wakiwa ofisini juu walisikia sauti na vijana wengi wakiwa wamezingira eneo hilo wakimtaka Maalim.

“Tukiwa ofisini tulisikia shangwe nyingi, pale nje vijana walikuwa wengi, nilishuka kuwasikiliza wakaniambia haja yao Maalim.

Bimani alisema, muda mfupi Maalim Seif aliteremka chini na kuwafuata vijana hao ambao walifurika eneo hilo huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.

Mabango hayo yaliandikwa. “ UN mnataka ushahidi gani tena wakati dunia ilishuhudia uchaguzi ulivyovurugwa, kura zetu zimeishia wapi wakati tulipiga kura na kukuchagua wewe,” liliandika bango moja.

Wakizungumza na Maalim Seif, vijana hao walisema ni muda mrefu umepita wanataka kujua hatima ya nchi yao na ahadi aliyowapa ya kuwataka wawe wavumilivu wakati suala la haki yao likiwa linashughulikiwa.

“Sisi tuna yetu ndio yaliyotuleta hapa tunataka kujua hatima ya kura zetu na ile ahadi uliyotuambia tutulie, sasa tunataka kauli yako wewe ndio kiongozi wetu Maalim,” alisema kijana mmoja.

Akitoa majibu, maalim Seif aliwaambia ni kweli aliwaahidi vijana hao watulie wakati suala la kudai haki yao likiwa linafanyiwa kazi na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu.

“Ninachoamini kwamba haifiki mwaka 2020 haki itapatikana na wale ambao wanawavunja moyo wanafanya hivyo kwa kujua kwamba juhudi zinafanyika na hatua zitachukuliwa.
“Bado dunia ipo nanyi na wanaendelea na jitihada za kupatikana suluhu ya kudumu, nawaomba vijana mzidi kuwa watulivu kwani haki haipo mbali na wala haitopotea,” alisema.

Maalim Seif aliwaahidi vijana hao kwamba hajachoka kusimamia suala hilo ikifika mahali atawaita kuwapa majibu alipofikia.

Kwa upande wa vijana ambao walikuwa kimya wakimsikiliza, waliahidi kuendelea kuwa watulivu na watiifu kwa chama na viongozi wao.

Vijana hao walimwahidi Maalim Seif kuwa hawatavunjika moyo juu ya mambo yote yanayopita kwani wanaamini Mungu yupo pamoja na wao na hawatomvumilia yoyote mwenye nia ama azma ya kuwarejesha nyuma katika juhudi zao za kuendeleza amani ya nchi.

Vijana hao waliahidi kuwa watakilinda chama hicho kwa gharama yoyote na kuhakikisha wanapambana na yoyote yule anaetaka kuuvunja umoja wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles