Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
SAKATA la ‘Bunge Live’ limechukua sura mpya baada ya wananchi 11 kufungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiiomba kutoa uamuzi wa kupinga Serikali kutorusha matangazo ya moja kwa moja (Live) ya vikao vya Bunge vinavyofanyika mjini Dodoma.
Wananchi hao waliofungua shauri hilo namba 43, 2016, ni Aziz Himbuka, Perfect Mwasilelwa, Rose Moshi, Penina Nkya, Moza Mushi, Andrew Mandari, Hilda Sigala, Juma Uloleulole, Kubra Manzi, Ray Kimbito na Ben-Rabiu Saanane, ambao wamewakilishwa na mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo.
Wakiwasilisha ombi hilo jana mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na mwenyekiti wao, Jaji Kiongozi Ferdinand Wambari, wakili Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa uamuzi huo umekuja baada ya kuona raia wa kawaida wana haki ya kikatiba ya kuona majadiliano ya vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma chini ya Ibara ya 18(b)(d) na Ibara ya 29(1). Majaji wengine ni Jaji Mfawidhi Seleman Kihiyo na Jaji Ama-Isario Munisi.
Kibatala alidai kuwa awali Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alitoa tangazo la kuzuia kuonyeshwa moja kwa moja kwa matangazo ya vikao vya Bunge vinavyoendelea Januari 23, 2016 na kutaja sababu za kuchukua uamuzi huo kuwa ni pamoja na kupunguza gharama.
Alidai baada ya kutolewa tangazo hilo, wananchi hao waliona linakiuka haki yao ya kikatiba ya kuona majadiliano ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia vipindi vya redio na televisheni.
“Kutokana na hali hiyo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikiuka haki ya kikatiba ya Watanzania, kwa kuzuia matangazo hayo bila ya sababu za msingi na kuiomba mahakama hiyo iielekeze kuyarejesha.
“Matokeo ya kuzuiliwa huko, haki za walalamikaji wakiwamo Watanzania za kufuatilia na kuwasimamia wabunge wao zimezuiliwa kwa vile walalamikaji hao hawawezi kufuatilia vitendo wanavyofanya wawakilishi wao waliowachagua wakiwa bungeni,” alidai.
Kibatala alidai kuwa kutokana na hali hiyo, katazo hilo limeweza kuathiri haki ya kikatiba ya walalamikaji ya kupata taarifa kwa vile hawawezi kuona majadiliano hayo kikamilifu, kwa mfumo bora wa uwazi na uwakilishi, na kwamba sababu zilizotolewa na Serikali za kuzuia matangazo hayo hazijitoshelezi.
Alidai kutokana na hali hiyo, walalamikaji na Watanzania kwa ujumla wana haki ya kikatiba ya kuwakilishwa kikamilifu bungeni, ikiwamo haki ya kuwasimamia wabunge wao kupitia namna wanavyofanya wakiwa bungeni.
“Walalamikaji na Watanzania kwa ujumla wao wana haki ya kupata taarifa kwa masuala ambayo yanaathiri maisha yao na taifa kwa ujumla, ikiwamo haki yao ya kuisimamia Serikali kupitia vikao vya Bunge,” alidai.
Hata hivyo, upande wa walalamikiwa, uliowakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Abubakar Omary ulidai mahakamani hapo kuwa hati ya wito wa mahakama katika shauri hilo waliipata Juni 23, mwaka huu, hivyo uliiomba mahakama hiyo kuwapa muda kwa ajili ya kuipitia na kuwasilisha majibu yao ifikapo Julai 15, mwaka huu.
Jaji Kiongozi Wambari alikubaliana na ombi hilo na kuhairisha shauri hilo hadi Julai 15, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa, na siku hiyo hiyo itaanza kusikilizwa kwa sababu majaji wengine wana vipindi.
Awali, Waziri Nape alitangaza uamuzi wa Serikali wa kusitisha kurusha baadhi ya shughuli za Bunge kwa madai kuwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), limeshindwa kumudu gharama.
Hata hivyo, Serikali ilienda mbali zaidi kwa kuzuia pia vituo binafsi vya televisheni kurusha matangazo hayo, huku TBC1 ikirusha vipindi vya maswali na majibu pekee ikielezwa kuwa uamuzi huo ulipitishwa katika Bunge la 10.
BARAZA LA WADHAMINI
Katika hatua nyingine, Baraza la Wadhamini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Katibu Mkuu wa chama hicho, wamefungua shauri Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuiomba kutengua uamuzi wa Jeshi la Polisi nchini kupiga marufuku mikutano na maandamano ya vyama vya siasa nchi nzima.
Walalamikaji hao wakiwakilishwa na mawakili Peter Kibatala na Omary Msemo, walifungua shauri hilo la madai namba 43, 2016 mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambari.
Wakili Kibatala aliiomba mahakama hiyo kufuta, kutengua zuio la mikusanyiko au mijumuiko ya kisiasa ya vyama vya siasa kwa kipindi kisichojulikana, lililotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), kwa sababu halikuwashirikisha, halikuwapatia haki ya kusikilizwa na ni uonevu, linaua demokrasia nchini, halina mipaka wala sababu za msingi kisheria na kimantiki na limezidi mamlaka ya polisi kisheria.
Katika kesi hiyo, walalamikiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Jeshi la Polisi ambao waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata ambaye alidai mahakamani hapo kuwa walipewa hati ya wito huo Juni 23, mwaka huu.
Wakili Malata aliiomba mahakama hiyo kuwasilisha hati ya kiapo kinzani, Juni 30, mwaka huu, kabla haijakaa na kuanza kusikiliza maombi madogo Julai 1, mwaka huu.
Hata hivyo, Jaji Wambari alidai shauri hilo litaanza kusikilizwa Julai mosi mwaka huu na kwamba wanatarajia uamuzi kutolewa Julai 4, mwaka huu.