30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Vinara wa kuchinja watu wauawa

Simon Sirro
Simon Sirro

NA ASIFIWE GEORGE, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewaua watu wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi.

Watu hao wanadaiwa kuhusika katika matukio ya mauaji mkoani Mwanza na Tanga ambako watu kadhaa waliuawa kwa kuchinjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema  majambazi hao waliuawa jana na juzi Jijini.

Kwa mujibu wa Sirro, mmoja wa waliouawa   ni jambazi sugu aliyefahamika kwa jina la Salum Said (30), mkazi wa Chamazi, Dar es Salaam.

Alisema  inasemekana Said ndiye aliyehusika kuwachinja watu waliokuwa wakisali msikitini jijini Mwanza na kwamba ndiye aliyekuwa kinara wa kundi lililotekeleza mauaji hayo.

“Mtu huyo, ameuawa leo (jana) hapa Dar es Salaam baada ya askari kuzingira nyumba yake iliyopo Buguruni.

“Kabla hajauawa, aligundua kwamba askari wamezingira nyumba yake, hivyo alitokea dirishani ili atoroke, lakini alishindwa na alianza kujibizana na polisi kwa kurusha risasi.

“Baada ya kuona hawezi kupambana na askari waliokuwa wamezingira nyumba yake, alirusha bomu moja la mkono ambalo lililipuka.

“Kwa bahati nzuri, halikumdhuru mtu yeyote   na alipojaribu kukimbia, alipigwa risasi ya moto mguuni na sehemu mbalimbali za mwili wake. Baadaye askari walimchukua na kumkimbiza hospitalini  lakini alifariki dunia akiwa njiani.

“Inasemekana mtuhumiwa huyo baada ya kufanya mauaji msikitini  Mwanza,  alikimbilia Dar es Salaam kwa ajili ya kujificha.

“Lakini, jana asubuhi maeneo ya Buguruni wilayani Ilala, kikosi kazi kilifanikiwa kuzingira nyumba yake,” alisema Kamanda Sirro.

Katika tukio hilo la mauaji ya msikitini Mwanza lililotokea Mei 18 mwaka huu, waliouawa ni Imamu wa msikiti huo, Ferouz Elias, Mbwana Rajab na Khamis Mponda ambaye alikuwa  dereva wa bodaboda.

Kamanda Sirro alisema   mtuhumiwa mwingine wa ujambazi aliyeuawa ni Mohamed Abdallah, maarufu kwa jina la Abuu Seif.

Seif  anadaiwa kuhusika katika mauaji ya watu wanane  katika kitongoji cha Kibatini, mkoani Tanga.

Sirro alisema mtuhumiwa huyo inasemekana alihusika kuua watu wanane mkoani Tanga Juni mosi mwaka huu, pia amekuwa akihusika katika matukio mbalimbali ya ujambazi mkoani humo.

Alisema mtuhumiwa huyo baada ya kutekeleza mauaji mkoani Tanga alikimbilia Dar es Salaam kujificha.

“Kwa hiyo, mtu huyo aliuawa juzi baada ya askari kupata taarifa kutoka kwa msiri mmoja.

“Kabla ya kumuua, askari walizingira nyumba yake iliyoko Kimara na alipogundua kwamba askari wamemzingira, alifyatua risasi hewani kuwatisha askari hao.

“Ieleweke kwamba  kabla ya kumpata huyo mtu  Juni 25 mwaka huu, tulifanikiwa kuwakamata watu wawili walioonekana kufanya mawasiliano ya mara kwa mara na mtuhumiwa Mohamed Abdallah.

“Watu hao ni Saada Abdallah (27), anayeishi maeneo mawili ya Segerea na Malamba Mawili ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Udaktari Muhimbili.

“Mwingine aliyekamatwa ni dereva wa malori wa Kampuni ya Titanic na Islam, Rashid Mangwena (26), mkazi wa Kigogo Mkwajuni.

“Watu hao wawili walipohojiwa walieleza mahali anapoishi Abdallah ambaye alikuwa akitafutwa kwa miaka mitano kwa tuhuma za mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha maeneo mbalimbali nchini.

“Kwa hiyo, baada ya polisi kutambua mahali anakoishi, Juni 25  mwaka huu saa mbili usiku, kikosi maalumu cha polisi kiliandaliwa kwa lengo la kuzingira nyumba ya Sada ambaye alikuwa na mtuhumiwa kwa wakati huo.

“Kabla hatujamzingira, tuliambiwa kabisa kwamba mtu huyo anatembea na bastola wakati wote, kwa hiyo askari walikwenda kwa tahadhari ya hali ya juu,” alisema Kamanda Sirro.

Baada ya askari kuzingira nyumba hiyo, Kamanda Sirro alisema, mtuhumiwa alitoka ndani ya nyumba na kukimbia huku akiwarushia risasi askari.

Alisema askari nao walijibu  mashambulio na   kumjeruhi mtuhumiwa sehemu mbalimbali za mwili  wake.

Baada ya mtuhumiwa huyo kupekuliwa, alikutwa na bastola moja   ya Norinco iliyofutwa namba ikiwa na risasi tatu ndani ya magazine.

“Risasi nyingine 19 zilikuwa kwenye mfuko wa  suruali aliyokuwa amevaa na pia alikuwa na bomu la kurusha kwa mkono.

“Kwa kifupi, mtuhumiwa huyo alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu kutokana na kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha,” alisema.

Aliyataja baadhi ya matukio hayo kuwa ni   jaribio la kuvamia Kituo cha Polisi  Korogwe mwaka 2013 ambako alimjeruhi kwa risasi  polisi mkononi.

“Matukio mengine ni uvamizi wa vituo vya mafuta na uporaji katika maduka ya Tigo Pesa  na M-pesa mkoani Tanga,  mauaji ya watu watano na uporaji wa fedha kwenye duka la mikate mjini Tanga.

“Pia inasemekana alihusika katika tukio la mauaji na uporaji wa silaha katika Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam na mengineyo,” alisema na kuongeza:

“Pamoja na hayo, huyo mtuhumiwa alikuwa  akiwafunidsha vijana 150 mafunzo ya kigaidi  kwenye mapori”.

Ili kukabiliana na matukio ya uhalifu, alisema polisi wanaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliotoroka kutoka mapangoni Tanga.

Wakati huo huo, Kamanda Sirro alisema wamewakamata watuhumiwa wawili, raia wa Uganda wakiwa na vipande 660 vya pembe za ndovu na mashine ya kukatia pembe hizo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Said (54) na Ally Sharif (26). Watuhumiwa hao walikamatwa Juni 26 mwaka huu, maeneo ya  Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam wakiwa katika nyumba ya kupanga.

Kamanda  aliwataka wamiliki wote wa nyumba  kuhakikisha wanakuwa na  picha za wapangaji wao katika mikataba yao  iwe rahisi kuwakamata  wanapofanya uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles