Christian Bwaya
KILA mwaka mpya unapoanza, ni kawaida kwa watu wengi kuweka maazimio fulani ya kutekeleza. Wapo ambao huazimia kubadili tabia wasizozipenda.
Wengine huazimia kuanzisha mwenendo mpya wa maisha wanayoyatamani. Wengine hufikiria kutekeleza malengo fulani ya kijamii na kiuchumi yatakayobadili maisha yao kwa mwaka unaoanza.
Ingawa ukweli ni kuwa mwaka unapoanza kinachobadilika huwa ni tarehe tu, watu huwa na imani kuwa wanaingia kwenye zama za maisha mapya. Imani hiyo huambatana na jitihada za kujaribu kubadili maisha yao yaendane na zama hizo mpya. Wanasema, ‘mwaka mpya na mambo mapya.’
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa maazimio mengi yanayowekwa wakati mwaka unapoanza, huishia tarehe za mwanzoni mwa Januari. Msisimuko wa mipango mipya, maisha mapya, zama mpya, huishia mwaka ukiwa bado mpya. Baada ya hapo maisha hurudi kule kule yalikotoka.
Tafiti zinasema asilimia kati ya 8 na 10 tu ya watu wanaoweka malengo ya mwaka mpya, ndio hutekeleza malengo hayo kufikia mwisho wa mwaka. Maana yake asilimia kati ya 90 na 92 huwa wanaweka maazimio yasiyotekelezeka.
Katika makala haya, tunajadili kwa nini maazimio mengi mazuri hufa kabla hayajaanza kutekelezwa.
Mihemko ya kuanza mwaka
Kuingia mwaka mpya ni jambo la kusisimua. Watu wengi hutafakari namna watu wengi walivyoshindwa kuuona mwaka mpya. Kwamba ‘wamejaaliwa’ huwafanya wajione kama watu wenye wajibu fulani wa kubadili mtindo wao wa maisha yaendane na mwaka wanaouanza.
Msisimko huu, kwa hakika huwa ndio msingi wa maazimio mengi yanayowekwa wakati wa kuingia mwaka mpya. Kwa bahati mbaya maazimio yanayoongozwa na msisimko wa namna hii hayawezi kuleta matokeo yoyote ya maana.
Malengo yasiyopimika
Sambamba na kuweka maazimio katika hali ya msisimko, watu wengi huweka malengo yasiyopimika. Haya ni yale malengo makubwa yanayopendeza masikioni lakini hayana namna ya kutathmini utekelezaji wake.
Kwa mfano, mtu anaweza kuwa na malengo ya kufanikiwa kwa mwaka unaoanza. Lakini unapomuuliza anamaana gani anapokusudia kufanikiwa, anakwambia basi tu anataka kufanikiwa.
Lengo hili la kufanikiwa, ni pana mno kwa sababu utekelezaji wake hauwezi kupimwa. Na kwa sababu ni vigumu kupima utekelezaji wake, ni rahisi lengo hili kupoteza uzito wake siku chache baada ya kuazimiwa.
Kupuuzia mambo madogo
Utekelezaji wa malengo mengi ni matokeo ya mabadiliko ya tabia. Huwezi kutekeleza lengo la kuweka akiba kila mwezi kama huwezi kubadili tabia ya kufanya matumizi yasiyopangiliwa. Kwa mfano, inawezekana huwezi kuweka akiba kwa sababu unakuwa mwepesi wa kuwapa watu fedha usizokuwa nazo. Unatoa usicho nacho kwa sababu huna uwezo wa kusema hapana.
Kadhalika, huenda unaishiwa kwa sababu una tabia ya kununua vitu usivyovihitaji. Hata unapokuwa huna fedha unatafuta furaha kwa kununua vitu fulani. Usipoweza kubadili tabia hizi, huwezi kutekeleza malengo unayojiwekea.
Vile vile, watu wengi huwa hawafikirii namna mambo makubwa yanavyochangiwa na mambo madogo madogo. Na kwa sababu hawaoni mchango wa mambo madogo katika mambo makubwa, ni rahisi kupuuza mambo hayo ambayo kimsingi ndiyo yanayosaidia kuleta mabadiliko makubwa.
Kwa
mfano, mtu anayetaka kuacha pombe, anafikiri kile anachotaka kukipata, yaani kuacha
pombe lakini hafikirii mchango wa mazingira yanayoambatana na unywaji wa pombe.
Mazingira haya, kwa mfano, ni pamoja na kukaa katika maeneo
yanayo hamasisha unywaji wa pombe na hata kuambatana na wanywaji wa
pombe.
Unapoishi na walevi ni vigumu kubadili tabia unayotaka kuiacha. Kuachana na tabia
waliyonayo watu wako wa karibu ni sawa na kuwapinga. Si watu wengi wanaweza kukubali
kuwapinga watu wao wa karibu.
Hofu ya kushindwa
Watu wengi hawapendi kujisikia hatia. Wanapoona hawawezi kufanya kitu fulani wanatafuta namna ya kukwepa hatia yao. Mara nyingi, hatia hukwepwa kwa kuwabebesha lawama watu wengine. Hii ni hulka ya mwanadamu.
Ili uweze kutimiza malengo yako, unahitaji kuwa na kifua cha kuvumilia hatia. Katika safari ya kutimiza malengo, unaweza kufika wakati kile unachokiishi kinaonekana kwenda kinyume kabisa na kile unachokitamani. Usiruhusu kukata tama na kuamua kuachana na malengo yako. Unahitaji kuendelea kusimamia kile unachokiamini hata kama uhalisia unakuwa kinyume.
Kwa mfano, badala ya kuamua kuendelea kunywa pombe kwa sababu tu umerudia tabia hiyo baada ya jaribio la kuacha kwa juma moja, usikate tamaa. Kubali kujisikia hatia, na azimia kuendelea kujitahidi kujizuia.
Kama ulilenga kuanza mazoezi kila siku asubuhi na unajikuta umeshindwa kufanya hivyo kwa siku kadhaa, hatia isikufanye uachane na mpango wako. Kuwa na kifua cha kuvumilia hatia na amua kusonga mbele na mpango wako. Hiyo inaitwa nguvu ya maamuzi.
Kukata tamaa, mara nyingi, hutokana na imani kuwa unapolenga kutekeleza jambo, basi lazima ulitimize kwa asilimia 100. Hakuna malengo hufikiwa kwa asilimia hizo. Kubali kufanikiwa hata kwa asilimia 10 na uendelee mbele. Kuwa na maamuzi yanayoweza kuvumilika. Usikate tamaa.