23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, October 12, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Xi: Muungano wa China, Taiwan ni lazima

BEIJING, CHINA

RAIS Xi Jinping amesema muungano kati ya China na Taiwan hauepukiki na harakati za kisiwa hicho chenye mamlaka ya ndani kutaka uhuru wake ni ndoto ya mchana.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 40 tangu kutolewa kwa tamko muhimu juu ya sera ya China kuhusu Taiwan kwenye ukumbi maarufu wa umma mjini hapa jana, Xi alionya kuwa ikibidi hawatasita kutumia nguvu kulinda muungano huo.

“Tuko radhi kuweka upeo mpana kwa ajili ya muungano kwa njia ya amani, lakini kamwe hatutaruhusu aina yoyote ya harakati za kuwania uhuru wa Taiwan,” alisema Xi huku akishangiliwa na wajumbe ukumbini hapo.

China na kisiwa cha Taiwan kilichoko umbali wa kilomita 160 kutoka bara, zilitengana wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1949 baada ya upande wa wapiganaji wa kizalendo ulioshindwa kuamua kuunda Serikali yake kisiwani humo.

Xi amependekeza kufanyika mazungumzo ya pande mbili, ya kuweka mpangilio wa kuzileta pamoja sehemu hizo mbili kwa njia ya amani, akisema watu wa pande zote wanataka kuona zikiungana na kuwa China moja.

Alisema muungano huo unaweza kuwa wa mtindo wa ‘nchi moja-mifumo miwili’ ambao utaheshimu muundo wa kijamii wa Taiwan na mtindo wa maisha wa watu wa kisiwa hicho, wenye kuhakikisha haki na uhuru wao wa kidini, umilikaji wa mali na haki nyinginezo.

“Lakini watu wote wanapaswa kuelewa jaribio lolote la kutangaza uhuru wa Taiwan litaleta janga kubwa kwa watu wa Taiwan,” alionya Rais Jinping.

Haijulikani madai ya kiongozi huyo kuwa watu wa pande zote mbili wana kiu ya kuungana tena imepokewa vipi kisiwani Taiwan.

Ni juzi tu, Rais wa Taiwan, Tsia Ing-wen alitamka bayana, kuwa watu wa kisiwa hicho wanaazimia kuendeleza utawala na uhuru wao wa ndani.

Ingawa kwa wakati huu China na Taiwan zina uhusiano mzuri kibiashara na kitamaduni, Taiwan inayojivunia mfumo wake wa kidemokrasia, haionyeshi shauku ya kujiunga na China iliyo chini ya utawala wa chama kimoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles