23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA WASICHANA WA CHIBOK KUWARUDIA ‘WAUME’ ZAO

WAKATI habari zilipoibuka kuwa baadhi ya wasichana wa shule wa Chibok, waliotekwa na kundi la Boko Haram mwaka 2014, walikataa kurudi nyumbani pamoja na kundi la wasichana 82 walioachiwa Mei mwaka huu, dunia iliona ugumu wa kuamini taarifa hizo.

Hata wakati ilipotolewa video ya Boko Haram ikionesha wasichana waliovalia hijabu na kujihami kwa bunduki aina ya Kalashnikov, wakisikika kuwa wana furaha katika maisha yao mapya, kitu ambacho kilitosha kuwaaminisha watu. Baadhi walisema ni wazi wasichana hao wamelazimishwa kutamka hivyo.”

Lakini kwanini msichana yeyote, mwanamke yeyote angekuwa tayari kubakia au kumrudia mwanamume anayehesabika kuwa katili kiasi hicho?

Lakini, bado baadhi ya wasichana hawa waliookolewa na Jeshi la Nigeria kutoka mateka wako tayari kwa hiari kurudi katika maficho ya Boko Haram ya msitu wa  Sambisa uliopo kaskazini mashariki mwa Nigeria ili kuishi na watu hawa wasio na utu.

Januari, mmoja wa waandishi waliofuatilia sababu za baadhi ya wasichana hawa kutamani maisha yale ya msituni, alikutana na Aisha Yerima (25), ambaye alikuwa ametekwa na Boko Haram zaidi ya miaka minne iliyopita.

Wakati akiwa matekani, aliolewa na kamanda ambaye alimteka kiakili kwa mahaba, zawadi za thamani na nyimbo za mapenzi za Kiarabu.

Maisha yaliyomzuzua katika msitu wa Sambisa alieleza kuwa yalikatishwa ghafla na kuibuka kwa Jeshi la Nigeria mapema 2016, wakati, ambao mumewe alikuwa ameenda uwanja wa mapambano na makamanda wengine.

Wakati mwandishi huyo alipomhoji Aisha kwa mara ya kwanza, alikuwa anashikiliwa na serikali kwa miezi nane ili kumrekebisha.

Na alikamilisha program ya kumrudisha katika hali ya kawaida ya kiakili chini ya mtaalamu wa saikolojia Fatima Akilu.

Akilu ni mkurugenzi mtendaji wa Neem Foundation na mwasisi wa program ya kiserikali ya kurekebisha watu walioharibiwa akili kwa kuingizwa itikadi kali.

“Kwa sasa naona vitu vyote, ambavyo Boko Haram walituambia vilikuwa uongo,” Aisha alisema. “Sasa, wakati ninapowasikiliza redioni, nacheka.”

Lakini Mei mwaka huu, ikiwa ni chini ya miezi mitano baada ya kukabidhiwa kwa familia katika jiji la kaskazini mashariki la Maiduguri, alirudi katika maficho ya Boko Haram.

Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Dk. Akilu amefanya kazi na wapiganaji wa Boko Haram wakiwamo makamanda, wake na watoto wao na mamia ya wanawake waliookolewa kutoka matekani.

“Namna wanawake wanavyotendewa na Boko Haram huko matekani inategemeana na aina ya kambi, ambayo mwanamke alikuwamo. Inategeana pia na kamanda anayeendesha kambi husika,” alisema.

“Wale waliotendewa vyema ni wale walio tayari kuolewa na wapiganaji wa Boko Haram au ambao walijiunga na kundi hilo kwa hiari yao, lakini wakiwa si wengi. Sehemu kubwa ya wanawake hao hawakufurahia maisha ya raha waliyokuwa nayo wachache kama Aisha.”

“Aisha alijigamba kuhusu idadi ya watumwa waliokuwa chini ya usimamizi wake katika msitu wa Sambisa, heshima aliyopokea kutoka kwa makamanda wengine wa Boko Haram na ushawishi mkubwa aliokuwa nao dhidi ya mumewe. Na amewahi kuambatana naye mara moja katika mapambano.

“Wanawake hawa, ambao kwa sehemu kubwa hawakuwah kufanya kazi, hawakuwa na mamlaka wala sauti katika jamii wanakotoka, lakini ghafla wakajikuta wakisimamia kundi la wanawake kati ya 30 na 100.

Chini yao, wanawake hawa pia waliwafanyia kazi na kuwatuma huko na kule,” Dk. Akilu alisema.

“Utaona ugumu wa wasichana hawa teule walioishi maisha ya ‘peponi’ wanaporudi uraiani, ambako wanakosa ule uhuru waliobahatisha kuwa nao kule mafichoni.”

Mbali ya kupoteza mamlaka walizokuwa nazo msituni wanaporudi uraiani, sababu nyingine Dk. Akilu anaamini zinaweza kusababisha wanawake waamue kurudi kwa Boko Haram ni pamja na unyanyapaa ikiwamo kutoka kwa jamii.

Kwamba jamii inawachukulia kama wakuja kwa sababu ya ushirika wao na wanamgambo na maisha magumu wanayokutana nayo katika jamii ukizingatia hawakujiandaa na maisha hayo isitoshen shule ilikatishwa zamani.

“Kuwaondoa fikra za itikadi kali ni sehemu moja tu ya hili. Kuwachangamana tena katika jamii ni sehemu ya hiyo. Baadhi yao hawana vitu vya kuwasaidia kimaisha,” Dk. Akilu alisema.

Hivi karibuni, niliitembelea familia ya Aisha, ambayo bado iko katika mshtuko na majozi ya kwa ondoko lake hilo na ina wasiwasi na ustawi na maisha yake.

Mama yake, Ashe, alikumbuka ‘wake’ saba wa zamani wa Boko Haram aliowajua, wote marafiki wa binti yake, ambao waliurudia msitu wa Sambisa muda mrefu kabla ya binti yao.

“Kila wakati mmoja wao anapotoweka, familia yao ilikuja katika nyumba yetu kumuuliza Aisha iwapo alisikia kutoka kwa binti yao,” alisema. “Hicho ndicho nijuacho.”

Baadhi ya wanawake wamekuwa wakiwasiliana na Aisha baada ya kurudi kutoka Boko Haram. Dada yangu mdogo, Bintu alikuwepo wakati wa mawasiliano ya simu mara mbili hivi.

“Walimwambia aje na kuungana nao, lakini alikataa,” Bintu alisema. “aliwambia kwama hakutaka kurudi.”

Tofauti na baadhi ya wake wa zamani wa Boko Haram niliokutana nao, ambao aidha huhaha kukabiliana na hali ngumu ya kiuchumi au kukabiliana na unyanyapaa, hivyo maisha ya Aisha yalionekana kuwa katika mkondo huo.

Alikuwa akijipatia fedha kutokana na kununua na kuuza mavazi ya kiutamaduni mara kwa mara kuhudhuria matukio ya kijamii na kuweka picha zake mwenyewe katika mitandao ya jamii na alikuwa na mlolongo wa wanaume waliojitokeza kutaka kumposa.

“Mmoja wanaume hao anaishi Lagos. Alifikiria kumkubalia huyo,” anasema mama yake.

Lakini kila kitu kilienda halijojo wakati Aisha alipopokea simu nyingine kutoka kwa wanawake, ambao walirudi kutoka msituni, wakimfahamisha kuwa ‘mume’ wake wa  Boko Haram kwa sasa anaishi na mwanamke ambaye alikuwa hasimu wake!.

Kuanzia siku hiyo Aisha ambaye kwa kawaida yu mchangamfu na mwenye kujichanganya akageuka mpweke.

“Aliacha kutoka au kuzungumza au kula,” Bintu alisema. “Daima alikuwa mwenye huzuni.”

Wiki mbili baadaye, aliondoka nyumbani na hakurudi. Baadhi ya nguo zake hazikuonekana. Simu yake ilizimwa. Aliondoka na mtoto wake wa miaka miwili aliyezaa na kamanda katika msitu wa Sambisa, akimwacha yule mkubwa ambaye alizaa na mwanaume mwingine kabla hajatekwa.

Asta, mke mwingine wa  Boko Haram alimwambia kuwa amesikia wanawake wengi wamerudi katika kundi hilo lakini yeye hana mpango huo.

Hata hivyo, msichana huyo mwenye umri wa miaka 19-alieleza jinsi ‘alivyom-miss’ vibaya mumewe, na namna anavyotamani kumsikia na kuungana naye.

Lakini anasisitiza kuwa hatorudi msituni hata kama mumewe huyo atataka afanye hivyo.

“Bali nitamwambia aje kuishi nasi na kuisha maisha ya kawaida,” alisema.

Lakini kitendo cha Aisha, kutamani na mtu anayempenda kunaweza kuwa na nguvu zaidi kuliko hisia kwamba kundi alilo ‘mumewe’ linaendesha mauaji ya maelfu ya watu kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kukimbiza mamilioni wanaohaha kurudia maisha ya kawaida wakiwa katika makambi ya wakimbizi.

Makala haya yametafsiriwa na Mwandishi Wetu Joseph Hiza kutoka BBC.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles