27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

DAKTARI: POMBE UHARIBU THAMANI YA MAZIWA YA MAMA

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM


SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) linapendekeza  kipindi cha mwaka sifuri hadi miezi sita ni cha muhimu mno kwa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee.

WHO linapendekeza baada ya kipindi hicho mama huweza kuanza kumpatia chakula kiasi mtoto wake hatua kwa hatua.

Linapendekeza kwamba umri wa kunyonya kwa mtoto ni hadi angalau miaka miwili au muda mrefu zaidi kulingana na jinsi mama anavyoweza.

Wataalamu wa Lishe wanasema zipo faida nyingi ambazo mtoto huzipata kupitia maziwa ya mama yake, husaidia kupunguza uwezekano wa kifo cha ghafla hasa kwa watoto  wachanga.

Maziwa huwaongeza uwezo kiakili, hupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya kuambukiza, homa na saratani mbalimbali kama vile saratani ya damu.

Aidha, husaidia kupunguza hatari ya mwanzo wa ugonjwa wa kisukari wa mtoto, hupunguza hatari ya pumu, hupunguza matatizo ya meno na hupunguza uwezekano wa kupata matatizo ya kisaikolojia.

Wanasema kunyonyesha kuna faida nyingi kwa mama pia ikiwamo kumjenga kiafya na kwamba husaidia mfuko wa uzazi (Uterasi) kurejea katika hali yake ya kawaida kabla ujauzito.

Kitendo cha mama kumnyonyesha mtoto wake husaidia pia kupunguza kuvuja damu baada ya kujifungua na husaidia mama kurudi kwa uzito wake kabla ya ujauzito na humpunguzia hatari ya kupata saratani ya matiti baadae katika maisha yake

Ulevi na unyonyeshaji

Licha ya umuhimu huo mkubwa wa kipindi cha unyonyeshaji, wapo baadhi ya wanawake ambao wamejenga tabia ya kunyonyesha watoto wao huku wakiwa wamelewa.

Hivi karibuni, rafiki yangu alinialika nyumbani kwake, kulikuwa na sherehe ndogo ambayo aliiandaa kwa ajili ya kuzindua nyumba yake.

Rafiki yangu huyo amejenga nyumba yake jirani na nyumbani kwetu huku maeneo ya Mbezi Luis jijini Dar es Salaam, katika sherehe yake hiyo alialika pia majirani zake wengine wengi, kwa pamoja tulijumuika kufurahi.

Siku hiyo kulikuwa na kila aina ya chakula na vinywaji, kila mmoja alikula na kunywa kile alichokipenda sambamba na  muziki, tulikula na kucheza, kwa hakika tuliburudika.

Kulikuwa na watu wa jinsi zote na rika mbalimbali, miongoni mwa wageni hao walikuwapo pia wakina mama ambao walikuwa na watoto wadogo wakiwamo waliopo  katika umri wa kunyonya.

Kati ya wanawake hao, mmoja (jina linahifadhiwa) ndiye ambaye alinivutia kumtazama na kumfuatilia kwa ukaribu kuliko wengine wakati wote wa sherehe hiyo.

Mama huyo alikuwa amekuja na mtoto wake mwenye umri wa kati ya miezi minane na mwaka mmoja hivi.

Wakati wote wa sherehe mama huyo alikuwa akinywa pombe bila kujali jukumu maalumu linalomkabili la kumnyonyesha mtoto wake.

Mama huyo alikunywa pombe kiasi cha kuliwa mno lakini bado aliendelea kumnyonyesha mtoto wake kila alipolia na kuhitaji kunyonya, jambo hilo lilinishangaza.

Nilizidi kumfuatilia mama huyo, kadiri muda ulivyosonga mbele ndivyo alivyozidi kulewa, aliendelea kunyonyesha mtoto wake bila wasiwasi wowote.

Baada ya muda fulani alipomaliza kumnyonyesha mtoto Yule alipitiwa na usingizi, alilala kwa muda mrefu mno kuliko hapo awali tangu tulipofika katika sherehe ile.

Sherehe ile iliisha saa moja jioni, kila mmoja alirudi nyumbani kwake, lakini binafsi nilibaki nikitafakari juu ya mama na mtoto wake yule.

Kikubwa nilichokuwa nikijiuliza, je kuna madhara gani ambayo mtoto yule atayapata katika maisha yake kutokana na tabia ya mama yake, kulewa kupita kiasi na kumnyonyesha.

Niliamua kuchukua hatua na kumtafuta Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Plaxeda Swai ambaye anaeleza kwa kina ndani ya makala haya.

Vipindi muhimu

Daktari huyo anaanza kwa kueleza vipindi muhimu ambavyo mwanamke anatakiwa kujiepusha na ulevi kwamba ni miezi mitatu kabla ya kubeba ujauzito, wakati wa ujauzito na kipindi cha unyonyeshaji.

“Wengi hawajui na ama wanapuuza vipindi hivi muhimu, mwanamke anapaswa kujiepusha na unywaji pombe miezi mitatu kabla ya kubeba ujauzito, kuepuka pombe kipindi chote cha ujauzito na kipindi cha unyonyeshaji ili kumlinda mtoto wake,” anasema.

Anasema  mwanamke anapoacha matumizi ya pombe kabla na wakati wa ujauzito humuepusha mtoto wake anayemtarajia kuzaliwa akiwa ameathirika ubongo.

“Mwanamke akinywa pombe kabla na wakati wa ujauzito (hasa wakati wa ujauzito), ile pombe huenda moja kwa moja kuathiri ubongo wa mtoto na madhara yake hujitokeza wakati wa kipindi cha ukuaji wake,” anasema.

Anachotakiwa kufanya

Anasema kwa kawaida mama hutakiwa kumnyonyesha mtoto wake kuanzia kipindi cha mwaka sifuri hadi miezi sita bila kumpatia chakula au kinywaji cha aina yoyote.

“Ni kipindi muhimu kwa mtoto, na chakula pekee anachokitegemea kwa ajili ya ukuaji wake ni kunyonya maziwa ya mama yake,” anasema.

Anaongeza “Sasa ikiwa huyu mama ananyonyesha huku akiwa amelewa kuna athari kubwa mno ambayo mtoto wake huyapata ambayo wakati mwingine hujitokeza baada ya muda fulani.

Dk. Swai anasema mama anayenyonyesha huku akiwa ametumia kilevi anamuweka mtoto wake kwenye hatari ya kuathirika afya ya ubongo na kupata tatizo la mtindio wa ubongo.

“Kumbuka, awali nimeeleza kwamba mtoto hutegemea kula na kunywa kila kitu kutoka kwa mama yake akiwa tumboni, hivyo mama akinywa pombe huenda moja kwa moja kwa mtoto naye huipokea na kuinywa.

“Unywaji pombe ni hatari kwa mjamzito, mjamzito haruhusiwi kutumia kilevi cha aina yoyote, pombe huathiri afya ya mtoto aliyepo tumboni, kuna uwezekano mkubwa mtoto akazaliwa akiwa na hitilafu kuanzia mfumo wa fahamu, kuzaliwa na uzito mdogo, kichwa kidogo na madhara mengine mengi,” anabainisha.

Wakati wa unyonyeshaji

“Mtoto huyo anapokuwa amezaliwa, iwapo mama yake ni mlevi basi mtoto huendelea kunywa pombe kupitia maziwa ya mama yake, na hivyo huzidi kuathirika zaidi,” anasema.

Anaongeza “Wanawake wajue kwamba unapotumia kilevi cha aina yoyote ile, kilevi hicho huenda hadi kwenye maziwa yake na mtoto hupokea kilevi hicho kupitia maziwa ya mama yake pindi anaponyonya, ni hatari kwa afya yake.

“Wapo wanaofikiri kwamba madhara hujitokeza wakati wa ujauzito pekee na wanapojifungua hawajali wakati wa kunyonyesha wanaendelea kutumia vilevi, wanalewa tu, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mtoto,” anasema.

Anasema ni hatari kwa mama anayenyonyesha kutumia vilevi kwani humuathiri mtoto wake kwa namna moja au nyingine.

Mtoto hunyonya pombe

Daktari huyo anasema mama anapolewa na kumnyonyesha mtoto wake, mtoto huyo naye hulewa kwani hupata kilevi kupitia maziwa ya mama yake.

“Ile pombe anayokuwa amekunywa mama huenda kwenye maziwa yake, mtoto huipokea pindi tu anaponyonya, ni hatua mbaya mno na ni hatari kwa afya ya mtoto husika, kwa sababu kilevi kile huenda kuathiri afya ya ubongo wake,” anasema.

Daktari huyo anasema madhara yake ni kwamba mtoto husika huwa kwenye hatari kubwa ya kupata tatizo hilo la mtindio wa ubongo katika maisha yake.

“Jambo la msingi ni kwamba wanawake wawe makini na wasijiepushe na unywaji wa pombe (kilevi) aina yoyote ile miezi mitatu kabla ya ujauzito, kipindi chote cha ujauzito na kipindi chote cha unyonyeshaji ili kumlinda mtoto,” anashauri.

Majanga mengine

Daktari huyo anasema pamoja na kuathiri maziwa ya mama , vilevi vina athari nyingine nyingi kwa watumiaji wa jinsi zote mbili.

“Matumizi ya vilevi kupita kiasi hasa vile vikali ni hatari kwa afya ya mtumiaji kwa sababu huweza kumsababishia muhusika matatizo mengi na hatimaye wengi huishia kupata kifafa katika maisha yao,” anabainisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles