27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA WANAFUNZI WETU KUKOSA UDADISI

 

Na Christian Bwaya,

UDADISI ni uwezo wa kuhoji mazoea. Udadisi ni kiu ya kujiuliza maswali yanayolenga kutafuta majibu ya changamoto zilizopo. Mtu mdadisi lazima atakuwa na uchunguzi ndani yake. Haiachi akili yake itulie. Haridhiki na majibu yaliyozoeleka. Mdadisi hupembua taarifa kumwezesha kuelewa ujumbe uliojificha kwenye taarifa hizo.

Kwa hakika udadisi una nafasi muhimu katika kuleta maendeleo katika jamii. Ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili jamii yetu kwa kiasi kikubwa unategemea na uwezo wa raia kujiuliza na kusaka majibu ya maswali ya msingi.

Dhima kuu ya elimu iliyo bora ni kuzalisha raia wenye sifa ya udadisi. Hawa ni raia wanaofikiri kwa bidii, wanaohoji mazoea, wasioridhishwa na majibu yaliyozoeleka, wanaotumia muda mwingi kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.

Mambo kadhaa yanaweza kuchangia upatikanaji wa elimu yenye sifa hizo. Kwanza, ni mitalaa yenye ubora. Mitalaa ni mkusanyiko wa mambo yote, ndani na nje ya darasa, yanayomwezesha mwanafunzi kupata maarifa na ujuzi unaomsaidia kujitambua kibinafsi na kuitambua jamii anamoishi.

Mtalaa ni mwongozo wa jumla, wenye malengo mapana ya kumwuumba raia mwenye sifa fulani zinazokidhi mahitaji ya jamii husika. Kimsingi, mtalaa ni mtamanio ya jumla ambayo, ili yawe na maana, lazima yakutane na vipaji binafsi vya mwanafunzi kumsaidia kutambua wajibu alionao katika jamii sawa sawa na vipaji alivyonavyo.

Pamoja na ukweli kuwa mtalaa unahitaji kumwekea kijana mazingira ya kutambua vipaji vyake na nafasi aliyonayo katika jamii, ni vigumu mtalaa kukidhi mahitaji mahususi ya kila mtu. Ni hivyo kwa sababu, kama tulivyodokeza hapo juu, mtalaa kwa asili yake hubeba malengo mapana yanayoifikiria jamii kwa ujumla wake.

Ubora wa mtalaa wa nchi yetu umekuwa ukilalamikiwa. Hata hivyo, upungufu uliopo hauhalalishi ukosefu wa udadisi miongoni mwa vijana wetu. Pamoja na changamoto kadhaa, bado mtalaa wa nchi yetu ni moja wapo ya mitalaa bora barani Afrika. Kinachokosekana ni namna gani malengo na maudhui yaliyoanishwa kwenye mtalaa huo yanatafsirika katika maisha halisi ya mwanafunzi.

Hapa ndiko uliko umuhimu mkubwa wa mtu anayeitwa mwalimu. Kazi kuu ya mwalimu ni kutafsiri malengo hayo mapana yaliyoainishwa katika mtalaa na kuyahusianisha na mazingira halisi anayoishi mwanafunzi. Bila mwalimu, mwanafunzi ataishia kupata maarifa na ujuzi wa jumla usiomsaidia kuona mchango wake mahususi katika jamii. Mwalimu, kwa nafasi yake, ndiye anayebeba dhamana ya kujenga udadisi kama tutakavyoona mbeleni.

Ili mwalimu aweze kufanya kazi hiyo nyeti lazima awe na sifa fulani. Sifa ya kwanza na muhimu ni kuelewa malengo mapana ya mtalaa. Tunahitaji mwalimu mwenye weledi na ari ya kumjengea mwanafunzi uwezo wa kudadisi.

Haitoshi kuwa na mtaala mzuri kwa maana ya kuwa na malengo mazuri yanayogusa matatizo halisi ya jamii. Tunahitaji kuwa na utaratibu mzuri wa kusimamia utekelezaji wa mtalaa tukilenga kumsaidia mwanafunzi kujenga shauku ya kujifunza, kiu ya maarifa na njaa ya kudadisi. Mazingira wezeshi, ambayo kimsingi yanafahamika, ni suala la lazima. Tunazungumzia miundo msingi, zana za kujifunzia na kufundishia.

Aidha, katika kutathmini ufanisi wa mchakato huo wa ujifunzaji, unahitajika upimaji makini. Hapa tunazungumzia mitihani inayopima uelewa wa wanafunzi. Ili mitihani iaminike kuwa na ubora, lazima itoe taswira inayokadiria uwezo halisi alionao mwanafunzi. Mitihani inayotolewa na Baraza la Mitihani inakidhi viwango hivyo. Hata hivyo, ubora wa elimu wanayopata wahitimu hawa wenye vyeti halali umeendelea kuwa changamoto.

Makala inayofuata inalenga kuonesha namna gani mwalimu mwenye sifa anaweza kubeba jukumu la kuratibu mchakato wa ujifunzaji unaoibua udadisi ndani ya wanafunzi kwa kutumia mitalaa hii hii katika mazingira haya haya.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles