Na MWANDISHI WETU
RUSHWA ni janga ambalo linazuia nchi nyingi duniani kupunguza umaskini uliokithiri, kupunguza vifo vya watoto wachanga na hata kupambana na magonjwa makubwa kama VVU/Ukimwi. Kama haitakabiliwa kikamilifu, inauwezekano mkubwa wa kuzui kufikia Malengo ya Maendeleo ya Milenia.
Rushwa ni uhalifu dhidi ya maendeleo, demokrasia, elimu, ustawi, afya ya umma na haki – mambo haya yote ni nguzo za ustawi wa mwanadamu.
Siku hizi rushwa haifijichi tena, hasa kwa mataifa ambayo viongozi wake hawako makini katika kuidhibiti.
Huu ni uhalifu mkubwa unaodhoofisha jamii, kuangamiza
maisha na kuchochea kukosekana kwa maendeleo.
Suala la msingi katika kupambana na rushwa ni kuingiza sekta binafsi katika
utekelezaji wa mikakati ya kupambana na rushwa.
Yaani sekta binafsi zinapaswa kutokubaki nyuma ya serikali. Kwamba, wafanyabiashara
lazima pia wazuie rushwa katika ngazi zao na kuondoa hongo katika zabuni na
mchakato wa manunuzi.
Kampuni zinatakiwa kutodanganya na kuwa wazi kutathminiwa kulingana na kanuni
ya 10 ya Mkataba wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa. Kanuni hii inasema:
“Wafanyabiashara wakabiliane na rushwa ya aina yoyote ile, ikiwa ni pamoja
na udanganyifu na hongo.”
Wakati fedha za umma zinapoibwa kwa ajili ya maslahi binafsi, ina maanisha kwamba
kutakuwa na rasilimali chache kujenga shule, hospitali, barabara na mitambo ya
kusafishia maji.
Wakati misaada ya kigeni ikielekezwa katika akaunti binafsi za benki, maana
yake miradi mikubwa ya miundombinu inasimama.
Vijana Afrika wanakabiliwa na uwezekano wa kutoa hongo zaidi
Vijana wa Afrika wana uwezekano mkubwa zaidi wa kutoa hongo kuliko watu wazima.
Shirika la Kimataifa la Kukabiliana na Ufisadi, Transparency International, linasema vijana wa Afrika wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 34 wana uwezekano mkubwa wa kutoa rushwa kuliko watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 55.
Katika kipimo chake cha kiwango cha ufisadi duniani cha mwaka huu, utafiti wake pia umefichua kwamba watu maskini zaidi wana uwezekano mara mbili zaidi wa kutoa rushwa na wanao uwezekano mkubwa pia wa kuwa waathiriwa wa hongo inayosababishwa na tabia ya urasimu kuliko matajiri.
Utafiti huo wa kila mwaka ambao ni wa mwaka wa 10 sasa, unasema barani Afrika, Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wapo juu zaidi ambapo asilimia 75 ya watu wake wanaokabiliwa na ufisadi waliwalipa polisi hongo.
Ripoti hiyo pia inasema raia wa kigeni nao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika kuchochea na kushiriki ufisadi barani Afrika na hivyo kuhujumu maendeleo ya kudumu ya kikanda.
Transparency International, linasema kampuni mbalimbali hutoa hongo ili kupata mikataba kama vile ya haki ya uchimbaji wa madini, mikataba ya ujenzi wa miradi mikubwa na mingineyo.
Pia linasema kwamba matokeo ya utafiti wake yametokana na mahojiano ya ana kwa ana yaliyofanyika Septemba 2016 na Septemba 2018, kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kimaendeleo Barani Afrika –Afrobarometer.
Tanzania yaongoza mapambano dhidi ya rushwa Afrika
Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti rushwa, ugonjwa wa Malaria, Ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hadi vijijini.
Ushindi huu ulipatikana baada ya kamati maalumu ya maendeleo ya afya kufanya ukaguzi katika nchi za Afrika na kuona mwenendo wa utoaji wa huduma za afya, ambapo Tanzania iliibuka kidedea.
Baada ya ushindin huo, Februari waka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema nchi za Bara la Afrika zimeitaja Tanzania kuwa ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika mapambano dhidi ya saratani ya rushwa.
Akitoa muhtasari wa yaliyojiri katika Mkutano wa 32 wa Wakuu wa nchi za Afrika (AU) uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Waziri Mkuu ambaye alimuwakilisha Rais Dk. John Magufuli katika mkutano huo alisema katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, Serikali barani Afrika zimesisitizwa kupambana na wala rushwa, ambapo Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi zilizopiga hatua katika mapambano hayo.
Mbali na kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, pia ripoti ya kamati maalumu iliyoundwa kuhusu masuala ya afya inaonesha Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri.
Waziri Mkuu alisema Tanzania imefanya vizuri katika kusimamia na kudhibiti ugonjwa wa Malaria, mapambano dhidi ya Ukimwi pamoja na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hadi vijijini.
“Imetupa faraja kwa sababu ukaguzi uliofanywa na kamati maalumu ya maendeleo ya afya, iliyotembelea nchi za Afrika kuona mwenendo wa utoaji wa huduma za afya imeonesha kwamba Tanzania tupo katika kiwango kizuri.”
Waziri Mkuu alisema mafanikio hayo yamekuja baada ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, kuthamini zaidi sekta ya afya nchini.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema viongozi hao walizungumzia kuhusu mwenendo wa biashara kwa kutumia anga, bahari na biashara za nchi kavu ambazo zinafanywa na Bara la Afrika na Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zilikubaliana na uundwaji wa “Mkataba wa Korido ya Biashara.”
Alisema viongozi hao wametakiwa kuimarisha biashara na Serikali imetoa fursa ya wazi kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuwekeza na kwamba Tanzania iko tayari kuungana na mataifa yatakayofanya biashara nchini Tanzania.
Katika mkutano huo, viongozi wa Umoja wa Afrika walikutana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali kuhusu biashara, wakimbizi na usalama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, alisema licha ya changamoto zote zinazolikabili Bara la Afrika, bara hilo limeacha milango yake wazi kwa wakimbizi hivyo, alizitaka nchi za Ulaya ambazo zimefunga milango yake kwa wakimbizi zijifunze kutoka kwa Afrika. Guterres aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa 32 wa viongozi wa nchi wanachama za AU ambao kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ilikuwa nı ‘Wakimbizi na waliorejea makwao.’ Kiongozi huyo wa AU aliongeza kuwa Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto kuu tatu ambazo ni amani na usalama, maendeleo endelevu pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa.