23.6 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Bijagos: Visiwa tajiri wa maliasili vyenye maradhi lukuki

Na Mwandishi Wetu

BIJAGOS ni kundi la mkusanyiko wa visiwa 88 vilivyopo katika pwani ya Bahati ya Antlantiki ya Taifa la Guinea Bissau, magharibi mwa Afrika.

Mkusanyiko huo uliundwa na delta ya kale ya Rio Geba na  Rio Glande na vina eneo la ukubwa wa kilomita mraba 12, 958.

Hata hivyo, ni visiwa 20 pekee, ambavyo hukaliwa zaidi na watu ikiwamo cha Babuque, ambacho ndiko makao makuu ya kiutawala na ndicho chenye wakazi wengi zaidi.

Vina wakazi 30,000 wanaotumia lugha na mila zao pekee katika maisha yao ya kila siku.

Wasafiri  wanaozuru visiwa hivyo vya mbali barani Afrika hutarajia kwenda kujionea mandhari ya kipekee ya fukwe za kale na misitu asilia.

Lakini uzuri wa visiwa hivyo hauishii hapo, kwani pia vinatumika kama maabara asilia kutokana na mazingira ya kipekee ambayo ni mwafaka kufanyia utafiti wa baadhi ya magonjwa hatari ya duniani.

Pia wakazi wanaishi karibu na wanyama pori na viboko wa kipekee waishio katika maji ya bahari na kasa wakubwa.

Lakini visiwa hivi vya kupendeza na kimbilio la watafiti wengi wa tiba, vinakabiliwa na magonjwa ya kila aina ambayo yanatishia maisha ya wenyeji.

Wakati wastani wa umri wa kuishi nchini Guinea-Bissau kwa sasa ni miaka 60, katika visiwa vya Bijagos uko chini mno hata kwa wastani wa viwango vya Afrika. Kwa sababu hiyo, idadi kubwa ya wakazi wake ni vijana inaaminiwa kuwa chini kidogo.

Kutokuwapo kwa miundombinu na mawasiliano katika visiwa hivyo, ambavyo wakazi wake ni wakulima na wavuvi kumevifanya viwe nyuma kimaendeleo na kutochangamsha sekta ya utalii, ambavyo ingevibeba vilivyo iwapo hali hiyo ingerekebishwa.

Kama tulivyoona, licha ya kuwa maabara ya asili duniani, inakabiliwa na magonjwa yanayozisumbua jamii za visiwani humo, ikiwamo Malaria, ugonjwa wa macho wa trachoma, matende na minyoo.

Hata hivyo, visiwa hivyo huenda vina siri ya kukabiliana na magonjwa hayo ipasavyo.

Watafiti wa tiba wamekuwa wakifanya kazi katika visiwa vya Bijagos kwa miaka kadhaa kubaini ikiwa wanaweza kuangamiza baadhi ya magonjwa katika visiwa hivyo.

Hii ni kwa sababu visiwa hivyo vinahudumu kama maabara asilia kutokana na uhalisia wake.

Japo hali hiyo inafanya maisha ya kila siku kuwa ngumu inasaidia katika juhudi za kuangamiza magonjwa yanayoviandama.

Maji yanayotenganisha visiwa hivyo yanatumika kama kinga asili na hilo husaidia kulinganisha mbinu tofauti za kudhibiti magonjwa bila hatari ya kuharibu majaribio katika maeneo mengine ya utafiti.

Katika maeneo ya bara, watu wanaweza kuingia na kutoka sehemu zinazofanyiwa majaribio ya tiba, hali ambayo inafanya kuwa ngumu kubaini chanzo na athari ya magonjwa hayo.

Japo kuna visiwa vingi duniani, ni vichache vinakaribiana na hii inasaidia watafiti kufanya kazi tofauti lakini vikiwa mbalimbali ni bora zaidi kwa sababu uwezekano wa majaribio ya utafiti kuharibiwa ni mdogo.

Watafiti kutoka Chuo cha London nchini Uingereza kinachoshughulikia masuala ya usafi na tiba ya dawa za tropiki (LSHTM) awali kilikuwa kinaangazia ugonjwa wa macho wa trachoma.

Ugonjwa huo unawakabili watu milioni 1.9 dunia na ni moja ya hali ambayo inasababisha upofu unaoweza kutibiwa.

Trachoma unaweza kuambukizwa kupitia mikono iliyogusa macho ya mgonjwa, nguo zake au kupitia nzi aliyekalia jicho la mgonjwa.

Mazingira ya ugonjwa huo huwaathiri zaidi watu wanaoishi katika mazingira machafu na umeathiri mataifa 42 duniani.

Kuna wakati mmoja kulishuhudiwa visa ambapo kila mtoto katika vijiji vya kisiwani walikabiliwa na ugonjwa huo.

Dk. Anna Last kutoka taasisi ya LSHTM aligundua maeneo yaliyokuwa katika hatari ya ugonjwa wa trachoma kabla ya kutibu jamii nzima kwa kutumia antibiotic ili kukomesha mzunguko wa maambukizi.

Ugonjwa wa trachoma, ambao ni chanzo cha hali inayosababisha kupofuka macho si tatizo pekee linalowakabili watu katika visiwa vya Bijagos.

Kuna magojwa mengine kadhaa ambayo yanashughulikiwa, miongoni mwao ni malaria ambao unasambazwa na mbu.

Dalili za awali za malaria, ambao huua karibu nusu milioni duniani kila mwaka ni kuwa na homa kali kuumwa na kichwa kabla ya hali hiyo kugeuka kuwa mbaya zaidi.

“Ukizingatia viwango vya ugonjwa wa malaria katika visiwa hivyo – ambapo mmoja kati ya kila watu wanne wanaugua malaria, tulibaini kuwa mbu ni wazuri sana kwa kusambaza ugonjwa huo,” anasema na kuongeza:

“Kitu cha kushangaza ni kuwa tuligundua baadhi yao hawadhuriwi na dawa ya kuua wadudu. Hii inamaanisha njia maarufu zaidi ya kudhibiti malaria ambayo ni matumizi ya vyandarua vya kujikinga na mbu au kupuliza dawa ya wadudu huenda hazifanyi kazi.”

Dawa mpya ya kukabiliana na mbu inatarajiwa kufanyiwa majaribio maalumu kwa ajili ya visiwa hivyo, ambayo inalenga mbu na vimelea vya malaria ili kupunguza muda wao wa kuishi.

Tiba za sasa zilikuwa zinalenga kukabiliana na vimelea vya malaria ndani ya mwili wa binadamu.

Katika awamu hii ya majaribio, visiwa vyote vitapewa kifaa maalumu cha kudhibiti viwango vya vitu kama kitanda na vyandarua vya mbu.

Katika baadhi ya visiwa pia kutatolewa dawa kama njia ya kukabiliana na zingine hazitapewa dawa.

Kundi la wenyeji wa kisiwani limepewa mafunzo ya utabibu ikiwamo kutoa sampuli ya damu na kuchunguza kama ina viini vya malaria.

Pia wamejifunza jinsi ya kubaini mbu wanaosambaza malaria pamoja na kuandaa wataalamu wa kwanza wa wadudu wanaoitwa entomologist, katika visiwa hivyo.

Yote tisa kumi ni kwamba utafiti huu utawasaidia watu wanaoishi ndani na nje ya visiwa vya Bijagos.

“Kila utafiti unatusaidia kujifunza mengi kuhusiana na ugonjwa wenyewe na jinsi ya kuutibu, hali ambayo inaimarisha tafiti za siku zijazo,” anasema Dk. Anna.

Aidha, tafiti zinazofanyika visiwani humo zinaweza kuendeshwa haraka zaidi kutokana na uwezo wa kudhibiti mazingira kwa ujumla.

Tunaweza kuona kile kinachoathiri eneo maalumu hali ambayo inaweza kuwanufaisha watu wote kwa njia rahisi.

Mradi huu wa LSHTM unatarajiwa kuendelea katika visiwa vya Bijagos kwa miaka mingine mitano.

Matokeo ya tafiti zake huenda yakatumiwa kukabiliana na magonjwa hatari kama vile malaria katika maeneo mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,070FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles